The House of Favourite Newspapers

Mandela awapongeza Mugabe, Weah ashtushwa na Trump!

Mandela.

MKEKA ni msafi kupindukia! Hakuna nzi wala mdudu yoyote niliyemuona akithubutu kusogelea eneo hilo.

Tumekaa kwa utulivu mkubwa na macho yangu yanatazamana na kiongozi huyu shupavu mwenye busara nyingi.

Ndiyo, niko na Nelson Mandela. Sikumbuki nilikutana naye vipi, lakini nilijikuta nikiwa nimekaa huku mkononi nikiwa na kalamu na kijitabu kidogo cha kutunzia kumbukumbu (Note book).

Mzee wa watu hataki maneno mengi zaidi ya kuongea pointi! Hapa chini ni mahojiano yangu na Mandela, ambayo yalifanyika kwa Lugha ya Kiingereza na hapa nimeyatafsiri.

Weah.

Mimi: Mzee mbona umetulia sana? Kulikoni!

Mandela: Unataka nianze kupayukapayuka nini? Tufanye mazungumzo tumalize nikapumzike, akili inayofanya kazi sana haina muda wa kubwabwaja, jifunze hilo.

Mimi: (leo nimepatikana), sawa mzee lakini ni kwa nini hatukuona mwili wako kwenye jeneza? Ulizuia wewe muda mfupi kabla ya kuondoka?

Mandela: Sijui chochote kuhusu hilo! Ina maana sikuagwa kwa heshima zote?

Trump.

Mimi: Kuondoka kwako duniani kulikuwa gumzo! Shughuli zote zilisimama na hata waliokuwa maliwato walisitisha walichokuwa wanafanya, kifupi mzee ulitisha, uliagwa lakini hakuna mahali popote mwili wako ulionekana kwenye jeneza!

Mandela: Walikosea tu kufanya hivyo, ilikuwa lazima niagwe kawaida kama wengine. Sawa, nini kinaendelea kwa sasa huko duniani?

Mimi: Mambo ni mengi mno. Rais wa Tanzania kwa sasa ni Dk. John Pombe Magufuli, Mugabe hayuko tena madarakani, Marekani iko chini ya Utawala wa yule mfanyabiashara maarufu duniani, Donald Fred Trump na Hellen Johnson Sirleaf ameshakabidhi nchi kwa George Opong Weah, naamini unamkumbuka. Libya kuna machafuko na ishu ya biashara ya utumwa imezua gumzo, Kagame ameongezewa tena muda wa kutawala Rwanda na Jumapili iliyopita alikuwa nchini Tanzania, Yoweri Museven yupo sana pale Uganda!

Mandela: Dah! Tuanze na Mugabe, ilikuwaje? Amestaafu mwenyewe au kulikuwa na shinikizo la Umoja wa Mataifa?

Mimi: Unajua alianza msuguano na aliyekuwa makamu wake, Emmerson Mnangagwa, kwa sababu mkewe alikuwa na ugomvi naye, alimfukuza kazi na mwanasiasa huyo akakimbilia nchini kwako kujihifadhi, lakini jeshi la nchi hiyo halikukubaliana na kitendo hicho, lilimuweka kizuizini na kumtaka aachie madaraka na alifanya hivyo ingawa kwa shingo upande na hivi tunavyozungumza yuko nchini Malyasia kwa binti yake ambaye anatarajia kupata mtoto wa pili.

Mandela: Nisimulie kidogo kuhusu Museven, yupo kivipi?

Mimi: Hadi sasa, ameitawala Uganda kwa zaidi ya miaka 20, amebadilisha Katiba ambayo inaondoa ukomo wa umri kwa mtu kugombea urais na mihula ya kukaa madarakani, maana yake Museven anaweza kuendelea tu kuwania urais katika vipindi vingine.

Mandela: Kwa nini imekuwa hivyo, wanataka ili iweje?

Mimi: Sijui bwana, kila nchi inakuwa na sheria zake. Usisahau pia, mkewe Janeth, ni Waziri wa Elimu nchini humo.

Mandela: (anashusha pumzi ndefu na kutingisha kichwa), aisee! Haya bwana. Nimpongeze Mugabe kwa uamuzi wake wa kuachia madaraka ingawa haikuwa kwa ridhaa yake, pia umesema George Weah ameshinda urais wa Liberia, amepambana sana huyo kijana, tangu akiwa mchezaji wa mpira wa miguu na kutuletea heshima ya kipekee miaka ile ya 90 kwa kuchaguliwa Mchezaji Bora wa Dunia, nawapongeza sana kwa ujumla. Trump ni rais? Dah! Anasemaje?

Mimi: Jamaa ana maneno yake hayo…watoto wa mtaani wanasema ni kiboko ya shombo. Hivi karibuni alisema Afrika ni kama kuzimu na iko kwenye giza totoro, maneno yamechafua sana hali ya hewa.

Mandela: Duh! Kauli kama hizo wakati mwingine si nzuri sana, zinaweza kusababisha tafran kama watu watazipokea kwa jazba, anyway niache nikapumzike, huyu Trump asije akafanya nikakosa usingizi bure na mimi nikimuwaza sana, ushauri wangu kwa marais wa Afrika wasiotaka kuondoka madarakani, malipo yao watayapata, ni vyema wakajisahihisha mapema kabla jua halijazama.

Wakati nataka kumuuliza swali la mwisho, nashtushwa na mlio wa jogoo aliyekuwa jirani na dirisha la chumbani kwangu, nagundua kumbe nilikuwa naota haikuwa mahojiano halisi. Ndoto hizi bwana!

Kwa maoni na ushauri nicheki kwa namba hizi; 0679 65 96 33.

 

 

NA BRIGHTON MASALU |

 

SAA TISA USIKU KITANDANI KWANGU

Comments are closed.