The House of Favourite Newspapers

Maonesho ya TANTRADE za Kutikisa Desemba Hii

0

Aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dr. John Pombe Magufuli pamoja na serikali yake, alihimiza kuwepo kwa uchumi wa viwanda huku hamasa zaidi ikitolewa kwa wazawa kujenga viwanda hivyo nchini!

 

Lengo kubwa la mpango huo lilikuwa ni kuzalisha ajira, kupunguza gharama za uagizaji bidhaa nje na kuongeza pato kupitia kodi na hivyo kuipaisha Tanzania katika uchumi wa kati!

 

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kutambua umuhimu wa jitihada hizo za Hayati Magufuli, imeandaa maonesho ya sita ya bidhaa za viwanda vya Tanzania yanayopangwa kufanyika kuanzia Desemba 3 hadi 6, 2021 katika Viwanja vya Maonesho ya Kibiashara ya Kimataifa maarufu kama Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

 

Maonesho hayo yatafanyika sambamba na Sherehe za Miaka 60 ya Uhuru, ikiwa ni miaka sita tangu Hayati Magufuli alipotoa maelekezo kwa TanTrade kuandaa maonesho ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania kama moja ya mikakati ya utekelezaji wa sera ya uchumi kupitia viwanda na kuchangia kuingia katika uchumi wa kati.

 

Kauli mbiu ya maonesho hayo ni ‘Tumia Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania’ (Buy Tanzania, Build Tanzania), ikihamasisha Watanzania kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini ambapo matokeo yatakuwa upatikanaji wa soko la uhakika na endelevu kwa manufaa ya Watanzania.

 

Sera imara za Hayati Magufuli katika uchumi wa viwanda zilichochea kuanzishwa kwa viwanda vingi nchini katika maeneo mbalimbali na hivyo kufanya kuwe na umuhimu wa kuwahimiza wananchi kuwa wazalendo wa kutumia bidhaa zitokanazo na viwanda hivi vya ndani ili kujenga uimara na kukua kwa viwanda hivyo kutokana na soko la uhakika lililopo nchini!

 

Maonesho haya yamebeba malengo mapana kama vile kuendelea kuhamasisha Watanzania kutumia bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini ili kujenga uchumi imara, kuwaunganisha wenye viwanda na wazalishaji mbalimbali wa malighafi na huduma nyingine zinazohitajika viwandani na kuwaunganisha wenye viwanda na wasambazaji wa teknolojia ya viwanda.

 

Malengo mengine ni kuwakutanisha wenye viwanda na taasisi za uwezeshaji biashara ili kujadili namna ya kuepuka changamoto zinazoleta vikwazo vya uzalishaji na biashara pamoja na kuendelea kuzitambua bidhaa mpya zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini ili Watanzania waendelee kuzitumia!

 

Mwananchi wa kawaida ndiyo kiungo muhimu katika maonesho haya kwani ndiyo mlaji, mnunuzi na mtumiaji  wa bidhaa hizi zitokanazo na viwanda vya ndani, hivyo kujitokeza kwa wingi kwa wananchi kunatajwa kuwa ndiko kutakakoleta tija zaidi ya maonesho haya kuwafikia wateja wengi zaidi nchini!

 

Aidha, ushiriki wa viwanda vingi zaidi vya hapa nchini ndiyo dira ya kufanikisha usemi wa Tumia bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania kwa sababu viwanda vishiriki ndivyo vitakavyotoa fursa na hamasa zaidi kwa Watanzania kupenda bidhaa  zinazozalishwa nchini, hivyo kuzinunua na hatimaye kujenga Tanzania imara.

 

Kwa sasa Tanzania ina zaidi ya viwanda 4,500 vilivyopo mikoa mbalimbali, hivyo ushiriki wao kwa madhubuti utachangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya bidhaa za viwanda nchini!

 

Kulingana na tathimini ya ushiriki katika maonesho hayo ya mwaka 2016 hadi 2020 kumekuwa na ongezeko kubwa la viwanda vishiriki ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo viwanda 417 pekee vilihudhuria wakati hadi kufikia mwaka 2020 viwanda 596 vilishiriki!

 

Ukiachana na changamoto zinazoyakumba maonesho hayo kama vile ushiriki mdogo wa viwanda ukilinganisha na idadi ya viwanda vilivyopo nchini, maonesho hayo yamepata mafanikio makubwa kama kujenga jukwaa ambalo wadau wa sekta ya viwanda wanakutana na viongozi mbalimbali.

 

Jukwaa hili huongozwa na Waziri wa Viwanda na Biashara ambapo waziri huwaalika  viongozi wakuu kutoka wizara mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto ambazo zimekuwa kero kwa wenye viwanda.

 

Mafanikio mengine ni kuunganisha wenye viwanda na wauzaji wa malighafi , wanunuzi wa bidhaa za viwandani, taasisi zinazotoa huduma mbalimbali (kama fedha  na ushauri wa kitaalamu) kupitia maonesho pamoja na mikutano ya kibiashara.

 

Pia maonesho hayo yamerahisisha kutoa mafunzo kwa washiriki yenye kusudi la kuwajengea uwezo na uelewa wa pamoja katika masuala mbalimbali ya kisera, mikakati na matarajio ya masoko ya ndani na nje.

 

Washiriki katika maonesho hayo ni wamiliki wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, kampuni zinazotoa teknolojia ya mashine za uchakataji na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, taasisi mbalimbali zinazojihusisha na ubunifu, taasisi za uwezeshaji biashara pamoja na wananchi wa kawaida!

 

Sambamba na maonesho hayo ya bidhaa za viwanda, pia kutakuwa na mambo mbalimbali yatakayochagiza maonesho hayo kama Tamasha la Christmas Shopping Festival ambapo kutakuwa na bidhaa mbalimbali zitakazouzwa kwa bei ya promosheni zikiwemo simu na laptop sambamba na viburudisho kama nyama choma pamoja na  vinywaji vya kila aina!

 

Pia kutakuwa na kijiji cha wasanii ambapo wasanii mbalimbali maarufu nchini Tanzania wataonekana laivu na kubadilishana mawazo na watembeleaji wa maonesho haya.

 

Sambamba na hayo, pia kutakuwepo na klabu mashuhuri za mpira nchini zikiwemo Simba, Yanga na Azam huku mastaa wa kusakata kabumbu wakijumuika na watembeleaji wa maonesho ya bidhaa hizo za viwanda.

 

Pia, kutakuwa na michezo ya watoto, ushiriki wa makampuni ya promosheni, ushiriki wa bodi ya filamu pamoja na COSOTA na BASATA. Kwa wamiliki wa viwanda au taasisi zitakazopenda kushiriki maonesho hayo ya aina yake, wanaweza kuwasiliana na waandaaji wa maonesho hayo kwa kupiga simu namba 0754 265 822.

Leave A Reply