The House of Favourite Newspapers

Mapya Kigogo Polisi Aliyehukumiwa Kunyongwa!

DAR ES SALAAM: HII ni habari njema! Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Naemi Sillayo ameibua mapya baada ya kusema Tanzania imefikia pazuri katika harakati na kuiondoa adhabu ya kifo inayowakabili Watanzania 480.

 

Miongoni mwa wanaosubiri adhabu hiyo ya kunyongwa ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Polisi, Salender Bridge, Christopher Bageni.

 

Akizungumza hivi karibuni kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya kupinga adhabu hiyo yaliyofanyika kwenye kituo hicho, Kijitonyama, Dar, Sillayo alisema sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 14 ya mwaka 1999 inasema kila mtu ana haki ya kuishi hivyo adhabu ya kunyongwa inapingana na sheria hiyo.

 

Aliendelea kusema lengo la adhabu ni kumpa mkosaji nafasi ya kujirekebisha na si kumkomesha lakini katika adhabu ya kifo haimpi mtu nafasi ya kujirekebisha.

 

“Ubaya mwingine wa adhabu hiyo ni kwamba hata ikibainika mtu alinyongwa kimakosa hakuna nafasi ya kumuachia katika adhabu hiyo kwa kuwa anakuwa ameshafariki,” alisema Sillayo.

 

TUJIKUMBUSHE

Bageni na wenzake walidaiwa kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa dereva wa teksi wa Manzese.

 

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Urafiki, Mratibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Ahmed Makelle na Rajabu Bakari.

 

Walidaiwa kutenda makosa hayo Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande, uliopo wilayani Kinondoni baada ya kuwakamata wafanyabiashara hao Sinza, walipokuja Dar es Salaam kuuza madini.

 

Stori: Richard Bukos.

Comments are closed.