The House of Favourite Newspapers

MASHINDANO YA ‘TULIA TRUST’ KUKUTANISHA MIKOA BARA, VISIWANI

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na  mashindano ya ngoma za jadi ambapo mchakato  utaanza Septemba 20 hadi 22 mwaka huu huko Rungwe-Tukuyu mkoani Mbeya.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.
Akifafanua jambo juu ya mashindano hayo.

 

 

TULIA Trust waandaaji wa mashindano ya ngoma za jadi nchini yenye kauli-mbiu ya “Tuuenzi Utamaduni Wetu” wanatarajia kuanza mchakato wa mashindano hayo kwa mwaka 2018 wakihusisha mikoa yote nchini na visiwani Zanzibar.

 

Akizungumza na vyombo vya habari,  Mratibu wa mashindano hayo ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson,  ameeleza kuwa wako tayari kwa ajili ya zoezi hilo litakalofanyika kuanzia Septemba 20 hadi 22 mwaka huu huko Rungwe-Tukuyu mkoani Mbeya.

 

Ameeleza kuwa lengo la mashindano hayo ni kuuenzi utamaduni wetu na kuionyesha dunia wana utamamaduni wao na wameanza katika ngoma za jadi ila wataenda mbali zaidi katika  nyanja nyinginezo kama vile lugha, chakula na mavazi.

 

Aidha ameeleza kuwa wanashirikiana na serikali katika kupunguza umaskini,  hivyo walengwa waone ngoma ni  kazi ambayo itawaongezea kipato.  Ameeleza kuwa kwa mwaka huu wamelenga kuwa na vikundi 108 vitakavyokutanisha washiriki takribani 2,200 ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo vikundi 63 vilihusishwa, na 2017 kulikuwa na vikundi 89.

 

 

Amesema washindi wa miaka hiyo miwili walipewa zawadi mbalimbali kama vile fedha taslimu, pikipiki na ile ya kuendelezwa kimasomo katika chuo cha Sanaa Bagamoyo katika ngazi mbalimbali na hadi kufikia sasa takribani washiriki 30 wamepata fursa hiyo.

 

 

Kuhusu mafanikio  Dkt Tulia ameeleza kuwa washiriki watapata zawadi mbalimbali na kuwezeshwa zaidi, na amesema kuwa hadi sasa wana mkataba na hoteli za kitalii ambazo ngoma za jadi hutumbuiza na mafanikio yaliyotia moyo zaidi ni yale ya kikundi cha Bujora Dance kutoka jijini Mwanza kuwakilisha taifa nchini India katika miji mitatu na kurudi na ngao ya  ushindi nchini.

 

 

Kuhusu utaratibu wa kuwapata washiriki hao, Dkt Tulia ameeleza kuwa watashirikiana  na maofisa utamaduni kote nchini katika mchakato wa kupata washindi hao, aidha ametoa wito kwa makampuni ya simu kuwasaidia wananchi hao kupitia nyimbo zao ili waweze kupata kipato.

 

Comments are closed.