The House of Favourite Newspapers

Maskini Mama Wa Lulu Diva

0

Jina la Lulu Abbas Silangwa au Lulu Diva linapotajwa, wengi watamtambua, hasa vijana wanaohusudu muziki wa Bongo Fleva na sinema za Kibongo.

Lulu Diva amejipatia umaarufu kutokana na ndoto yake ya kuwa mwanamuziki bora na muigizaji anayebobea.

 

“Tangu nikiwa binti, nilikuwa na ndoto kubwa za kufikia makubwa katika utu uzima wangu. Kwa mfano nilikuwa nataka kuwa mwanamuziki mkubwa na muigizaji. Hiki ndicho ambacho nimeanza kukifikia,” anasema Lulu Diva.

Kwa mujibu wa Lulu Diva, safari yake kufika hapo alipo haikuwa rahisi hata kidogo.

 

Anasema kuwa, maisha yake ya utotoni yalikuwa ya kawaida wakati huo baba yake mzazi akiwa hai, lakini mambo yalibadilika baada ya baba yake kufariki dunia. Cha kwanza kilichokwenda kombo ni uwezo wa mama yake mzazi kumsomesha.

“Wakati baba yangu alipoaga dunia nilikuwa naingia kidato cha pili, ilibidi mama atafute mdhamini ambaye alikuwa anaishi Dar es salaam wakati tukiishi Tanga, kwa hiyo ilinibidi nitoke Tanga hadi Dar na kuendelea na masomo,” anasema Lulu Diva.

 

Anasema jitihada zake zilimwezesha kuchaguliwa kushika nyadhifa za uongozi wa wanafunzi huku akijihusisha mno na mambo ya sanaa.

 

Baada ya kumaliza sekondari, kama mtoto wa pekee kwa mama yake ilimlazimu aanze kusaka ajira. Alipata kazi kama mhudumu wa baa moja jijini Dar.

Haikuwa rahisi kama binti kutokana na unyanyapaa unaowakumba wanawake wanaohudumu baa, lakini alikaza kamba kuhakikisha yeye na mama yake wanaishi maisha ya kawaida.

 

Anasema kuwa, tukio mmoja ambalo hatalisahau katika kazi ya kuwa mhudumu ni pale aliposhambuliwa na mteja.

“Tukio hilo lilifanyika kwa haraka sana, huyo mteja alikuwa ameagiza kinywaji cha baridi, lakini baadaye akadai alikuwa ameagiza kinywaji cha moto.

 

Kwa kuwa tayari nilikuwa nimefungua kile kinywaji, nilijaribu kumshawishi akubali kinywaji hicho la sivyo ingenilazimu nilipe na sikuwa na pesa.

 

Mara ghafla yule mteja alinizaba kofi ambalo siwezi kusahau,” anasema msanii huyo anayekiwasha na wimbo mpya wa Samahani akiwa na Lava Lava.

 

Katika kipindi hicho, Lulu Diva anasema aliona umuhimu wa kusomea taaluma ya hoteli na akaenda kusomea masuala hayo ili awe na nafasi nzuri zaidi za kazi kuliko aliyokuwa nayo.

Vilevile Lulu Diva anasema hakufa moyo katika kufanikisha ndoto yake ya kuwa mwanamuziki, muigizaji na mfanyabiashara.

 

Jina la Lulu Diva kisanii lilianza kusikika yapata miaka mitano iliyopita akipambania nafasi yake kama mwanamuziki na muigizaji.

 

“Haikuwa rahisi kuwa msanii mkubwa, kwanza kabisa kuna dhana nyingi ambazo zinahusishwa na wasanii wa kike, hasa jinsi tunavyofika kwenye majukwaa makubwa ya usanii, ila mimi naamini kuwa ni jasho langu na ari ya kuendeleza talanta yangu imenifikisha nilipo,” anasema Lulu Diva.

 

Tukio ambalo limekuwa pigo kubwa katika maisha yake, lilianza miaka tisa iliyopita wakati mama yake mzazi alipoaanza kuumwa ugonjwa ambao ulimuathiri kiakili.

 

Tangu wakati huo hadi leo, Lulu Diva anasema maskini mama yake mzazi hajazungumza wala kutembea mwenyewe.

Kilio kikuu cha msani huyu ni kuwa wakati anaanza kupata kipato cha kumuwezesha yeye na mama yake kuishi maisha ya stara kuliko maisha ya taabu walikotoka, ndiyo wakati mama yake alianza kuumwa ugonjwa ambao umekuwa ukiwasumbua kwa muda mrefu.

 

“Mama hajazungumza kwa miaka tisa, sijui anafikiria nini? Sijui ananiwazia yapi na hata sielewi yuko katika dunia ipi? Ni jambo linalonikosesha usingizi. Najiuliza na usanii wangu huu mama hajaweza kunishabikia kwani haelewi kinachofanyika, inauma sana kumuona mama akiwa katika hali hii,” anasema.

 

Kwa miaka tisa hii, Lulu Diva hajaweza kuzungumza na mama yake na hata akimzungumzisha kutokana na maradhi yake, hana uwezo wa kujibu na hajui kama anatambua au hatambui akizungumzishwa.

 

Lulu Diva anasema anajivunia mwaka 2018 kupitia kipato chake cha muziki aliweza kumpeleka mama yake hospitalini alikofanyiwa upasuaji sehemu ya kiuno, lakini baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, mama yake alipata ajali na akavunjika mguu tena.

 

Ugonjwa wa mama yake umekuwa ni mtihani mkubwa kwake kwani mwezi Aprili mwaka huu aliamua kumuandikia wimbo maalum wenye historia yake na mama yake mzazi.

 

Wimbo huyo unaoitwa Mama ni maalum kwa ajili ya mama yake. Kwenye wimbo huo unaoibua hisia ya huruma anatoa ujumbe wa maombi yake kwamba siku moja mama yake atazungumza na kutembea tena.

 

Kwenye wimbo huo, Lulu Diva anasema; “Hii ni kutoka moyoni, nakupenda mama na ndiyo sababu kutwa napambana, kinachonitesa moyoni unaumwa sana, ila naamini ipo siku utapona, maana huwezi kula mwenyewe, wala kutembea mwenyewe, pengine ni siri yangu mwenyewe.”

Kwenye video ya wimbo huo, anaonekana mama yake akiwa kitandani.

MAKALA NA SIFAEL PAUL | GPL

Leave A Reply