The House of Favourite Newspapers

Mastaa Hawa… Kwa Tiffah Watapata Tabu Sana!

Princess Tiffah

KUWA mtu maarufu ni jambo moja, ‘ku-maintain’ huo umaarufu huwa ni jambo lingine tofauti.

Unaweza kuwa maarufu kwa maana ya kujulikana na watu lakini ndani ya muda mfupi, ukarudi katika kiwango cha katikati hata kupotea kabisa. Mara nyingi wanaojua ‘kumaintain’ umaarufu siku zote huwa wanajua kuzitumia fursa za umaarufu na umaarufu huo unageuka kuwa dili.

Mtoto wa mkali wa Bongo Fleva, Tiffah amedhihirisha kwamba amewekewa misingi mizuri ya umaarufu na kujua kuuishi. Wazazi wake kwa maana ya Diamond na mzazi mwenzake, Zarina Hassan ‘Zari The Boss Lady’, walimwekea misingi mizuri ya umaarufu tangu anazaliwa hadi sasa.

Hiyo ndiyo sababu binti huyu amezidi kuwa maarufu siku hadi siku. Kudhihirisha hilo, ingia kwenye ukurasa wake wa Instagram, utaungana na mimi juu ya hiki ninachokizungumza.

Tiffah ana wafuasi wengi zaidi kuliko hata mastaa wengi wenye umri mkubwa kuliko yeye. Si tu umri kwa maana ya miaka, wana umri mrefu tangu waanze kujiunga na mitandao lakini Tiffah yeye amejiunga mwaka 2015, mara tu baada ya kuzaliwa.

Akiwa na umri wa takriban miaka minne, Tiffah amewafunika mastaa ambao yawezekana walijiunga mtandaoni miaka sita au zaidi kabla ya kuzaliwa. Kwenye ukurasa wake, amepata ubalozi na matangazo ya makampuni mbalimbali kama Pugu Mall, Msasani City Mall, Babyshop, NMB Junior Account na VodacomKid.

Hayo yote kwake ni fedha! Akaunti yake ya Instagram ina wafuasi milioni mbili kasoro (1.8M), ana kila sifa ya ukurasa wake kutumiwa na wanaohitaji kutangaza bidhaa zao.

Atakayetangaza kwake, ana uhakika wa kuwafikia angalau wafuasi milioni moja na zaidi kwa wakati mmoja ambao wanaweza kushawishika kununua bidhaa husika.

Hana kazi yoyote Tiffah kama ilivyo kwa mastaa wengine wanaotumia kazi zao za sanaa yao kujiongezea wafuasi, Tiffah yeye anaposti tu picha akiwa nyumbani, sebuleni au jikoni lakini zinapendwa kweli.

Mastaa ambao wameingia miaka mingi kwenye mtandao lakini kumfikia Tiffah watapata tabu sana ni pamoja na Jenifa Kyaka ‘Odama’ mwenye wafuasi milioni 1.1, Sanch (630,000), Monalisa (milioni 1.6), Irene Uwoya (milioni 1.5) na Mayasa Mrisho ‘Maya’ (89,000).

Wengine ni Gigy Money mwenye wafuasi 713,000, Amber Lulu (999,000), Esha Buheti (684,000), Salma Jabu ‘Nisha’ (Milioni 1.3) na Flora Mvungi mwenye wafausi 125,000.

Katika hao, ukimuondoa Uwoya, Monalisa na Nisha wanaojitahidi kumfukuzia angalau kwa ukaribu Tiffah, waliobaki wote hawana sifa ya kupata matangazo ya maana kwa sababu hawajafikia hata wafausi milioni moja.

Kuna kitu cha kujifunza kwa mastaa wetu. Ni vyema kujipima, kujitathimini na kuchukua hatua maana ili ujijue nguvu yako ya ushawishi katika kizazi cha sasa, lazima uwe na wafuasi wengi.

Mbali na kukusaidia kutangaza kazi zako za sanaa lakini ukurasa wako unaweza kuwa platform ya matangazo na ukaingiza fedha vilevile.

Makala: Erick Evarist

Comments are closed.