The House of Favourite Newspapers

MASTAA HAWA… MISTARI NDO’ MAISHA YAO!

Bob Marley.

SUALA la wanamuziki kuimba mambo ambayo yanatokea kwenye maisha yao huwa ni la nadra sana kutokea. Wanamuziki wengi huwa wanaimba vitendo ambavyo wanavilaani, vimekwisha tokea au vinavyoendelea kutokea.

 

Lakini wapo waliothubutu kuimba mambo ambayo baadaye yametokea na kuandika historia.

Kwa mfano marehemu Robert Nesta ‘Bob Marley’. Ni mwanamuziki mkali wa Rege, ambaye aliwahi kutamba na ngoma nyingi duniani zilizompa heshima.

AY.

 

Ukiachana na historia ndefu, inasemwa kwamba Bob aliwahi kutabiri kwamba atakufa akiwa na miaka 36, jambo ambalo baadhi ya rafiki zake walimuona kama nabii.

 

Lakini hata baada ya kifo chake mistari aliyoimba kwenye wimbo wa Redemption Song; kwamba; “How long shall kill our prophet, while we stand aside and look.” akiwa anamaanisha kwamba, kwa kipindi gani watawaua manabii wetu, huku tukiwa tumesimama pembeni tukitazama. Hii ilionesha kwamba alikuwa anafahamu kwamba siku moja atakufa kwa kuuawa.

 

Kuawa kwa maana kuwa ripoti ilionesha alikufa kwa ugonjwa wa kansa akiwa na umri wa miaka 36 lakini baadaye kuna taarifa zilienea kwamba Bob Marley aliuawa na ofisa wa FBI ambaye alimuua kwa mionzi.

Joh Makin.

 

Mbali na Bob Marley, bila shaka wafuatiliaji wa muziki watakuwa wanamkumbuka vizuri mkali wa HipHop, Christopher Walles ‘B.I.G’. Kabla ya kifo chake mwaka 1997, B.I.G aliwahi kutoa album mbili Redy To Die na Life After Death. Katika album hizo kuna nyimbo ambazo alikuwa anagusa juu ya kifo chake.

 

Kwa mfano wimbo uitwao Suicidal Thoughts, kuna mistari aliimba; “I saw the God and I feel death is calling me.” Akiwa anamaanisha kwamba nimemuona Mungu na ninahisi kifo kinaniita. Kwenye wimbo mwingine uitwao My Downfall, B.I.G kuna mistari aliimba; “I was high when they hit me, took a few cats with me, Shit, I need the company!”

 

Miaka michache baadaye B.I.G aliuawa kwa kupigwa risasi huko Los Angels. Hapo ni kwa upande wa mbele na Kibongobongo hawa nao wamewahi kuimba mambo ambayo yamewatokea wenyewe na mengine kutokea katika nchi!

 

Sugu.

SUGU

Joseph Mbilinyi ni Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye kwa sasa anasota katika gereza la Ruanda huko Mbeya baada ya kupatikana na hatia katika kesi iliyokuwa ikimkabili ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

 

Kabla ya hapo Sugu amekuwa akiingia kwenye mikono ya polisi mara kadhaa jambo ambalo aliliimba wakati anafanya muziki na kutikisa kila kona Afrika Mashariki.

 

Ukiusikiliza wimbo uitwao Mikononi mwa Polisi ambao kwa mujibu wake alikuwa akiu-dedicate kwa marehemu Michael Sikubya, mwanafunzi wa Iyunga, Mbeya aliyeuawa mikononi mwa polisi, Sugu ameimba;

“Nipo mikononi mwa polisi, maisha yangu bado ni mikosi,

Nipo ndani nimechoka, polisi wamenipiga damu zinanitoka!” Na kweli aliingia mikononi mwa polisi na sasa anasota jela.

R.O.M.A.

 

R.O.M.A

Tukio la kutekwa la R.O.M.A pamoja na mwanamuziki mwenzake Moni Central Zone na prodyuza Bin Laden, lilitikisa nchi nzima kuanzia kwenye mitandao ya kijamii, mitaani na hata bungeni.

Lakini pamoja na hayo yote ni kama R.O.M.A, kabla aliona tukio hilo kama litakuja kutokea siku moja kwenye maisha yake. Ukisikiliza baadhi ya mistari kwenye ngoma iitwayo Mr President, aliyoitoa mwaka 2010, R.O.M.A aliimba; “Harakati ndiyo jadi siogopi hata wanichape mijeredi, hadi Yudi alikuwa shahidi kwa vinanda na vinubi!”

 

Ukiitafakari mistari hiyo na ‘nature’ ya tukio, utaona kwamba ni kweli R.O.M.A alichezea mijeledi na bado hajaacha harakati za kuimba ukweli. Sikiliza wimbo aliotoa baada ya Kutekwa wa Zimbwabwe utakubaliana na hili. Lakini hata aliposema;”Hadi Yudi alikuwa shahidi kwa vinanda na vinubi.”

Mwana FA.

 

Yudi alikuwa prodyuza wa R.O.M.A, kwenye ngoma hiyo ya Mr President na aliimba kwamba alishuhudia tukio la kutekwa kwake. Lakini wakati anatekwa tukio hilo lilishuhudiwa na Bin Laden, ambaye ni prodyuza wake pia. Kwa hiyo ni vitu vinavyoendana. Mbali na wimbo huo, ukisikiliza Wimbo wa Viva R.O.M.A Viva (2015), “Na wanaokufa masikini ni wanangu wa Briakhuru, Mungu aliwapa madini leo mnambinafsisha mkaburu?” Mwaka 2017, tumesikia mambo ya makinikia ambayo yanatokana na mgodi huo.

 

Ukisikiliza pia wimbo huo kuna sehemu kaimba; “Pesa sherehe za muungano hamzingatii itifaki, wanafunzi mnawachoma jua na shule hawana madawati, mnalipa mishahara hewa na hamlipi mafao walimu, mlimpiga Warioba alipowaletea rasimu.”

Ukiangalia ishu ya mishahara hewa ni suala ambalo limetikisa miaka miwili baada ya R.O.M.A, kuimba wimbo wake huo, lakini pia ishu ya madawati mashuleni imekuwa ni kampeni ya viongozi wengi katika miaka ya hivi karibuni.

PROFESSOR JAY.

 

PROFESSOR JAY

Kwa sasa mkali huyu wa michano, Joseph Haule ni mwanasiasa na Mbunge wa Jimbo la Mikumi, ambaye kabla alikuwa mwanamuziki mwenye jina kubwa Bongo.

Kabla ya ubunge Profesa, aliwahi kuimba wimbo uitwao Ndiyo Mzee ambao ni kama alitabiri kuwa siku moja atakuwa mwanasiasa. Ukisikiliza wimbo huo, mwanzoni kabisa kuna sehemu ameimba;

“Naitwa Joseph Haule mwana Mslopaganzi, nadhani nimeletwa niokoe hiki kizazi. Mimi ni mwanasiasa niliyebarikiwa na Mungu, nimeletwa kwenu waungana niwapunguzie machungu.”

Na kweli kwa sasa Profesa ni mwanasiasa na kwa Mikumi anawapunguzia machungu kama mbunge.

MAKALA: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.