The House of Favourite Newspapers

Mastaa Jifunzeni Hili Kifo cha Masogange!

Agness Gerald ‘Masogange’,

KWENU mastaa mbalimbali wa Bongo. Kwa ujumla wenu nawasalimu, uwe muigizaji, mchekeshaji, mwanamuziki au muuza sura kwenye video za wasanii kama alivyokuwa marehemu Agness Gerald ‘Masogange’, wote mpokee salamu yangu kwa moyo mkunjufu kabisa.

 

Nimewakumbuka leo kwa ujumla wenu na ninataka kuzungumza nanyi mambo makubwa matatu hususan katika kipindi hikihiki cha maombolezo ya kifo cha mwenzetu Masogange.

Ndugu zangu, nimeona niwaandikie barua hii katika kipindi hiki maana najua sisi wanadamu tulivyo. Tunasahau haraka sana. Hili limetokea na kuna mengine yaliwahi kutokea huko nyuma lakini baada ya muda tunasahau na kuendelea na maisha yetu. Ndugu zangu, imekuwa ni kawaida yetu kumkumbuka Mungu katika vipindi hivi vya misiba. Unapoona mwenzako amefariki, hapohapo utakuta mtu ameanza kwenda kanisani au msikitini lakini baada ya muda, anaacha kwenda.

 

Huo ni unafiki. Tusimfanyie Mungu unafiki, mnapaswa kuishi katika misingi ya hofu ya Mungu kila siku na si tu pale mnapoona misiba. Kimsingi najua wapo baadhi ya mastaa huwa wanasali siku zote lakini wengi wenu huwa hamumkumbuki Mungu. Mnafikiri kwamba maisha yenu yatakuwa sanaa tu hadi mbinguni, badilikeni. Anzeni kutengeneza uhusiano wenu na Mungu hapahapa duniani.

 

Jambo la pili ninalotaka kuwaambia ni kuhusu mabifu. Mastaa wengi hampendani. Mna chuki kweli, ni wanafiki sana. Utakuta fulani na fulani hawaongei, fulani anaungana na fulani kwa ajili ya kumshambulia fulani mitandaoni na kumdhalilisha, haipendezi. Kumbukeni haya maisha tunapita tu. Tusiwe watu wa kuchukiana.

 

Unapoona umemkosea mwenzako, muombe radhi na yule aliyeombwa radhi awe tayari kusamehe. Siyo mtu unaapa eti nikifa fulani asinizike, huo ni upungufu wa upeo. Maisha yetu ni mafupi, ni vyema kupendana, kuheshimiana na kuishi kama ndugu. Mwenzako akiwa na shida msaidie, imetokea misiba kama hivi, shirikianeni.

Siyo eti inatokea misiba halafu wewe huendi wala hutoi mchango wowote. Ukipata tatizo wewe unategemea watakusaidia? Sitawataja ambao hamkuhudhuria msiba wa Masogange kwa makusudi lakini najua mnajijua na Mungu anawaona. Kitendo cha nyinyi kutokwenda hakimaanishi kwamba Masogange hatazikwa lakini mngeenda, mngeonesha umoja wenu na mshikamano.

 

Jambo la mwisho ni kuhusu heshima yenu. Kila mmoja anapaswa kujitafakari kuhusu heshima na jina lake katika jamii. Jiulize ukifa leo, utazungumzwaje? Watu watasema ‘mtu wa watu amefariki’ au watakupuuza kutokana na jina lako baya katika jamii? Haijalishi

 

una jina baya kiasi gani lakini kama bado unapumua, unayo nafasi ya kubadilisha jinsi watu watakavyokuzungumzia baada ya kifo chako. Anza sasa kumrudia Mungu. Acha unafiki, acha majungu, jitahidi sana kutenda mema kadiri Mungu alivyokujalia.

 

Usiishi kana kwamba uhai ni mali yako. Kama ni muislamu, tenga muda wa ibada. Kama ni mkristo, Jumapili au Jumamosi, nenda kanisani. Mshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai. Muombe akupe ulinzi katika siku zijazo. Akujalie hekima, busara na ufuate mafundisho yake. Mkizingatia hayo, kwa ujumla wenu mtaishi vizuri na vipaji vyenu Mungu atavibariki. Asanteni na nawapenda wote.

Mimi ni ndugu yenu;

Comments are closed.