The House of Favourite Newspapers

Mastaa wa Mchiriku na Taarab… Kukinukisha Pasaka Dar Live

0

khadija_kopa1Khadija Kopa

MASTAA kibao wa Muziki wa Mchiriku na Taarab wakiongozwa na Msaga Sumu na Khadija Kopa wanatarajiwa kukinukisha Machi 27 (Sikukuu ya Pasaka) ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.

Akizungumza na mwandishi wetu, Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alisema kuwa mashabiki wengi wa Muziki wa Mchiriku na Taarab walikuwa wakiomba kukutanishwa jukwaa moja mastaa hao na Dar Live kwa mara ya kwanza itawashusha mastaa hao.

msagasumu akiimba wimbo wa shemeji unanitega (2)Msaga Sumu

“Mchiriku ama Singeli kama wengi wanavyoutambua umekuwa ukiliteka soko la muziki kwa sasa. Mashabiki wengi hasa vijana wamekuwa na shauku kubwa kuushuhudia muziki huo ukipigwa sambamba na Taarab ambapo ombi hilo tumelisikia na Pasaka hii hatoki mtu Dar Live,” alisema Mbizo.
Burudani kwa watoto

Mbizo alisema kuwa siku hiyo ambayo itakuwa ni Jumapili, pazia la burudani litafunguliwa mapema kuanzia saa mbili za asubuhi ambapo kutakuwa na burudani kwa watoto huku Dar Live ikiwaandalia michezo yote.

“Tumewaandalia michezo mingi ikiwemo kuteleza, bembea, kuogelea, mazingaombwe na pia kutakuwa na kikundi kipya cha sarakasi kitakachotoa burudani safi kwa watoto hadi mida ya saa kumi na mbili kisha itaanza shoo kwa wakubwa.”
Mchiriku

Kuhusiana na Muziki wa Mchiriku, Mbizo alisema mbali na Msaga Sumu mashabiki wa muziki huo wategemee kuwaona jukwaani wakali kibao wanaobamba kila mitaa ambao ni Dogo Mfaume, Siza Mazongele, Jagwa, Sholo Mwamba pamoja na Man Fongo.

“Utakuwa ni usiku wa toa kitu weka kitu. Naweza sema ni shoo ya kibabe kutoka kwa wakali hao. Kama wewe ni shabiki wa Singeli huu si wakati wa kukosa.”

Taarab
Mbizo alisema kuwa Muziki wa Mchiriku pacha wake ni Taarab kwani kiasili unatokana na Taarab hivyo ili kunogesha jukwaa na kila shabiki wa muziki akate kiu yake, Dar Live itawashusha wakali wa Taarab wakiongozwa na Malkia wa Mipasho, Khadija Kopa.

“Bendi ya Ogopa Kopa itakuwepo kutoa burudani mwanzo mwisho huku ikifunikana na East Africa Melody wakali wa mujini.”

Mtonyo
Siku hiyo ambayo wengi hutoboa mifuko na kuvunja vibubu, Dar Live itapokea mtonyo kwa watoto shilingi 2,000 tu huku shoo ya Mchiriku na Taarab ikiwa kwa mtonyo wa shilingi 6,000 tu na geti litajifungua lenyewe.

Leave A Reply