The House of Favourite Newspapers

Mastaa Wagombea Ubunge Matumbo joto

0

WAKATI zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu, imeelezwa kuwa mastaa waliojitosa kuwania ubunge katika uchaguzi huo, sasa presha inawapanda na kushuka. RISASI linachambua.

 

Hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba Uchaguzi wa mwaka huu umewaleta ulingoni wasanii ambao wanawania nafasi hiyo kwa mara ya kwanza huku wale wakongwe wakikumbana na ushindani mkali unaoweza kuweka rehani nafasi ya kurudi mjengoni.

 

Katika uchaguzi mkuu huu, wabunge ambao ni manguli wa fani ya sanaa na majimbo yao kwenye mabano ni Joseph Haule ‘Profesa Jay’ (Mikumi – Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini – Chadema), wamedaiwa kuwa kivutio cha kipekee kwa mastaa wenzao ambao nao katika uchaguzi huu, wamenuia kutobaki nyuma.

 

MATUMBO JOTO

Hata hivyo, licha ya unguli huo, hali sasa imekuwa tofauti baada wasanii hao kukumbana na ushindani mkali majimboni mwao kutoka chama tawala.

 

SUGU

Joseph Mbilinyi maarufu Sugu au Mr. 2, ni mwanamuziki mkongwe na muasisi wa muziki wa Hip Hop nchini. Sugu ametumikia wananchi wa Jimbo la Mbeya Mjini (Chadema), tangu mwaka 2010.

Mkongwe huyo anapambana na aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri, Dk. Tulia Ackson (CCM) ambaye alikuwa mbunge wa kuteuliwa na rais.

Ushindani kwa Sugu umeleta msisimko wa kipekee kutokana na nguvu ya ushawishi aliyonayo mwana mama huyo.

 

PROFESA JAY

Profesa Jay ni nguli wa muziki wa Hip Hop, amekuwa mbunge wa Jimbo la Mikumi, Morogoro kupitia Chadema kwa kipindi kimoja kuanzia 2015-2020.

 

Mkongwe huyu naye anapambana na Dennis Lazaro Londo anayegombea jimbo hilo kupitia CCM. Hata hivyo mazingira ya siasa katika uchaguzi wa mwaka huu, hayatokuwa rahisi kama mwaka 2015 ambapo mkongwe huyo alipata mtelelezo kutokana na upepo wa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

 

Hali sasa imekuwa tofauti kwani Mwenyekiti wa CCM, Dk. John Magufuli ameonesha wazi kutumia kila aina ya mbinu kuhakikisha majimbo hayo yaliyokuwa upinzani yanarejea chini ya himaya ya CCM.

 

WAKAZI

Wakazi ambaye jina lake kamili ni Webiro Wasira, ndiye mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga, kupitia chama cha ACT Wazalendo. Hata hivyo, ugumu kwa msanii huyo wa hiphop unatokana na ukweli kwamba ndio mara yake ya kwanza kuwania nafasi hiyo.

 

Lakini pili, jimbo hilo la Ukonga ni sawa na kusema halina tena mwenyewe baada ya aliyekuwa mbunge wake kupitia Chadema, Mwita Waitara kutimkia CCM katika nngwe ya mwisho lakini licha ya kurejeshwa kwenye jimbo hilo kwa kupitia CCM, aliamua kwenda kuwania jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara.

Kwa sasa mgombea wa CCM Ukonga ni, Jerry Silaa ambaye anatoa changamoto kubwa kwa msanii huyo.

 

KINGWENDU

Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’, ni Msanii wa Vichekesho Bongo, ambaye katika uchaguzi huu amekuwa kimya katika kampeni zake licha ya kutangaza kuwania jimbo la Ilala kupitia CUF.

Awali katika uchaguzi wa mwaka 2015, aliwania jimbo la Kisarawe na kuangushwa vibaya na Seleman Jaffo (CCM).

Hata hivyo, ugumu wake katika jimbo la Ilala unatokana na ukongwe na uzoefu alionao mshindani wake kutoka CCM, yaani Mussa Hassan Zungu.

 

MWANA FA

Hamis Mwinjuma ‘Mwana Fa’, ni mwanamuziki nguli wa Hip Hop, ambaye pia anawania jimbo la Muheza mkoani Tanga.

Katika uchaguzi huu jimbo hilo lina na ushindani wa kipekee hasa ikizingatiwa vinara wanaochuana wote ni vijana.

Mwana Fa anagombea kwa mara ya kwanza kupitia CCM huku mshindani wake mkubwa akiwa ni Yosepha Komba kutoka Chadema.

Mwanadada huyo ambaye ni machachari katika kuzungumza, kujenga hoja, anampa wakati mgumu msanii huyo hasa ikizingatiwa Yosepha tayari anao uzoefu kupitia ubunge wa viti maalumu nafasi aliyoitumikia kuanzia mwaka 2015-2020.

JHIKOMAN

Msanii huyo wa Muziki wa Reggae Jhikolabwino Siza Manyika maarufu kwa jina la Jhikoman anawania jimbo la Nyasa kupitia chama cha ACT Wazalendo.

Hata hivyo, msanii huyo anakumbana na kigingi kizito kutoka kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo lililopo mkoani Ruvuma, Mhandisi Stella Manyanya.

Kwa kuwa msanii huyo anawania jimbo hilo kwa mara ya kwanza, mikiki ya kisiasa inatarajiwa kuwa mwiba kwake hasa ikizingatiwa mwanamama huyo kutoka CCM, tayari amejijengea mizizi katika jimbo hilo.

BABA LEVO

Msanii mwingine ambaye katika uchaguzi huu, presha inapanda na kushuka ni mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva na aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mwanga Kaskazini (ACT Wazalendo), Clayton Revocatus Chipando ‘Baba Levo’.

Baba Levo anawania kata hiyo kwa mara ya pili, lakini safari hii anakumbana na CCM iliyojiandaa kimapambano tofauti na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambao CCM iligawanyika baada ya Lowassa kutimkia Chadema.

Leave A Reply