The House of Favourite Newspapers

Mastaa Yanga wavunja Ukimya, Tambwe Amtaja Kakolanya

Kikosi cha timu ya Yanga.

BAADA ya Yanga kupokea vichapo mfululizo, mastaa wa timu hiyo wamevunja ukimya na kuwaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kutamba kuwa bado lengo lao ni kuhakikisha wanatwaa makombe mawili msimu huu.

 

Kauli hiyo, wameitoa ikiwa ni siku chache tangu watoke kufungwa mchezo wa ligi na Stand United kwa bao 1-0 na ule wa robo fainali ya SportPesa Cup dhidi ya Kariobangi ya nchini Kenya kwa mabao 3-2.

Yanga inajitupa tena kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Alhamisi ijayo katika mchezo wa FA watakapovaana na Biashara FC ya Mara. Mpaka sasa kwenye ligi, Yanga imecheza mechi 20 imefanikiwa kushinda mechi 17, ikitoka sare mbili huku ikipoteza mchezo mmoja hali inayompa matumaini mshambuliaji huyo mwenye mabao sita msimu huu kuweza kutwaa ubingwa.

 

Wakizungumza na Championi Jumamosi, nyota Juma Abdul, Mrisho Ngassa na Amissi Tambwe walisema wao kama wachezaji wamekuwa wakijadiliana mambo kadhaa ya kuhakikisha timu yao inapata ushindi na kuchukua ubingwa wa ligi kuu kama walivyopanga.

 

Tambwe alisema kupoteza mchezo mmoja kwenye ligi siyo sababu ya wao kupoteza ubingwa wa ligi zaidi watajipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika michezo ijayo.

“Kiukweli malengo yetu ni kutwaa ubingwa, hakuna mchezaji ambaye hatambui hilo na ndiyo sababu ya kila mechi kwetu huwa tunacheza kama fainali kwa kuwa tunahitaji matokeo, maana bado kuna mechi nyingi na wapinzani wetu wamekuwa wakifukuzia kutokana na ushindani ulivyo.

 

“Nikwambie tu sisi tunaangalia mechi zetu tunashinda vipi kwa kuwa tunataka ubingwa wa msimu huu na jambo ambalo linawezekana kwa nafasi kubwa iwapo tutaendelea kufanya vyema kwenye mechi zetu, hakuna jambo lingine.”

 

Kwa upande wake nahodha msaidizi, Juma Abdul alisema: “Wanayanga waondoe hofu ya ubingwa wa ligi katika msimu huu, kwani kama wachezaji malengo yetu tuliyojiwekea ni ubingwa pekee na siyo kitu kingine.

 

“Hivyo, wasikatishwe tamaa na matokeo ya mchezo wetu uliopita na Stand, ninaamini kocha ameona upungufu wetu uliosababisha tupoteze, hivyo tunajipanga kwa ajili ya michezo ijayo.”

 

Kwa upande wake Ngassa alisema: “Sisi kama wachezaji malengo yetu tuliyojiwekea katika msimu huu ni kuona Yanga inauchukua ubingwa na siyo kitu kingine na hilo linawezekana kwetu. “Tuliona upungufu uliojitokeza katika mchezo uliopita na Stand baada ya kukaa na kocha na kupitia video ya mechi hiyo, hivyo tumepanga kufanyia marekebisho ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika michezo ijayo ya ligi, hivyo mashabiki wawe watulivu, wasubiri furaha.”

TAMBWE AMTAJA KAKOLANYA

Aidha mbali ya malengo yao, Tambwe alizungumzia suala la kipa namba moja wa timu hiyo Beno Kakolanya kusimamishwa huku mashabiki wakionekana kumkataa kipa Klaus Kindoki kutokana na kuwa na uwezo mdogo.

 

“Kuhusu suala la mashabiki wanataka Kakolanya kurudi kwenye timu, kiukweli hilo siyo jukumu langu kabisa ni suala la mwalimu mwenyewe ndiyo anajua nini cha kufanya hata kama mashabiki wanasema hivyo.

 

“Lakini kama mchezaji akirejea tutaendelea kushirikiana naye ili kufikia malengo ya msimu huu kwa kuwa alikuwepo kabla ya kutokuwepo maana hata leo mimi nikiambiwa nicheze nitacheza hivyo sioni sababu kuongelea hilo kwa kuwa siyo jukumu langu,” alisema Tambwe.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.