The House of Favourite Newspapers

Mbaroni kwa Kutumia Jina la Mke wa JPM Kutapeli, Kutakatisha Fedha!

WATU wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka manne ikiwemo kutumia jina la Mke wa Rais Dkt John Magufuli, Mama Janeth Magufuli wakijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ikiwemo kutapeli Tsh milioni 4.5.

 

Mkurugenzi wa Leseni wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), John Raphael amesema hayo leo nje ya mahakama hiyo baada ya watuhumiwa ambao ni Saada Uledi, Maftah Shaban, Heshima Ally na Shamba Baila kusomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde.

Wakisomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali, Batilda Mushi washitakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari 2017 na Machi 2019 katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ambapo walikula njama na kuchapisha taarifa kupitia akaunti waliyofungua wakiita jina la Janeth Magufuli kwenye mtandao wa Facebook.

Kosa jingine ni la kuchapisha taarifa za uongo ambapo wanadaiwa katika tarehe hizo ndani ya mkoa wa Dar es Salaam walichapisha taarifa kupitia akaunti ya mtandao wa Facebook ukiwa na jina la Janeth Magufuli ambaye ni mke wa Rais wa Tanzania wakionyesha kuwa wanamiliki taasisi inayotoa mikopo wakiwataka watu wenye uhitaji na wa kupatiwa mikopo, wanatakiwa kutoa kiasi flani cha pesa ili wapatiwe mkopo huo huku wakijua kwamba ni uongo.

Katika kosa jingine ni la utakatishaji fedha, wanadaiwa kati ya Machi 2 na 8, 2019 ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine walijipatia kiasi cha Tsh milioni 4.5 wakati wakijua ni zao la fedha haramu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, hivyo wamerudishwa rumande na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na imeahirishwa hadi Mei 2, mwaka huu.

Akizungumza baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili watuhumiwa hao, Raphael amesema kuwa ni kosa la jinai kufungua akaunti mbalimbali za mitandao na kutumia majina ya viongozi ama watu mashuhuri na kuyatumia kujipatia fedha zisizo halali.

Aidha, katika tukio hilo pia TCRA wamewafikisha mahakamani watuhumiwa wengine katika Mahakama hiyo ya Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kuendesha televisheni ya matandaoni kupitia Chaneli ya YouTube bila kuwa na leseni ya uendeshaji shughuli hiyo kutoka TCRA jambo ambalo ni kinyume na sheria na kanuni za makosa ya mtandao za mwaka 2018.

 

Akiwasisitiza wananchi, Raphael amewataka kuzingatia sheria ya TCRA kuendesha mitandao ya kijamii ikiwemo kuendesha televisheni za YouTube zilizosajiliwa na matumizi yaliyosahihi na kuepuka kusambaza maudhui potofu katika jamii, badala yake kuzingatia weredi na kanuni zilizowekwa.

Comments are closed.