Mbelgiji awaondoa hofu Simba, aahidi kipigo AS Vita

AKITUA kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jana, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems ametamba kuwa kama wamewafunga Al Ahly na JS Saoura hapa nyumbani, basi AS Vita Club nao watakufa tu.

 

Simba jana ilirejea jijini Dar es Salaam ikitokea Algeria ilipokwenda kucheza na JS Saoura ya nchini humo katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Simba walifungwa mabao 2-0.

 

Jumamosi hii, Simba inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuvaana na AS Vita katika mchezo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa. Akizungumza na Championi Jumatano, Aussems alisema kuwa tayari alishaanza maandalizi ya mchezo huo tangu akiwa Algeria na kikubwa anahitaji ushindi wowote ili kufanikisha malengo yao ya kwenda hatua ya robo fainali.

 

Aliongeza kuwa, anawafahamu vizuri AS Vita ambao alicheza nao katika mchezo wa awali uliochezwa Kinshasa nchini DR Congo, hivyo hana hofu baada ya kuyafanyia marekebisho baadhi ya makosa. “Mchezo wetu na Saoura ulikuwa mgumu kwa upande wetu kutokana ukubwa wa safari yenyewe ambao ulisababisha wachezaji kuchoka.

 

“Tayari nimewaambia wachezaji wangu kusahau matokeo ya mechi na Saoura na badala yake kuelekeza nguvu katika mchezo na Vita.

“Tunaamini mechi haitakuwa nyepesi kwetu, lakini kwa maandalizi niliyoyafanya na sapoti ya mashabiki ninaamini hatutapoteza mchezo huu,” alisema Aussems na kuongeza.

“Leo (jana) baada ya timu kurejea moja kwa moja tunaelekea kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huu.”

 

Kwa upande wa nahodha wa timu hiyo, John Bocco alisema katika mchezo dhidi ya JS Saoura, walipoteza kutokana na bahati haikuwa kwao, lakini nguvu na akili sasa wanazielekeza mechi na Vita kuhakikisha wanashinda, kikubwa wanaomba sapoti ya mashabiki wao

Toa comment