The House of Favourite Newspapers

Mbelgiji wa Simba Afunga Hesabu Sauzi, Anogewa na Mkongo

 

Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems

WAKIWA wamefikisha siku 12 kambini nchini Afrika Kusini, Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems ametamba kuwa muda ambao wameutumia kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao unatosha kabisa kwao kuutetea Ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa Afrika.

 

Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kumaliza kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa na Platinum Stars ya Afrika Kusini na kumalizika kwa Simba kushinda mabao 4-1 ukiwa ni mchezo wa pili baada ya awali kuwachapa Orbet TVET ya nchini humo kwa mabao 4-0.

 

 

Simba leo Jumamosi itaingia Uwanja wa Royal Bafokeng huko mjini Rustenburg ambako imeweka kambi, kucheza na wapinzani wa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Township Rollers FC ya Bostwana. Mechi ya kwanza ya Yanga na Township inapigwa kati ya Agosti 9 na 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Simba tangu imetua Sauzi imekuwa ikifanya mazoezi ya nguvu ili kuhakikisha wanatetea ubingwa msimu ujao pia kuifikia na kuivunja rekodi yao ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Baadhi ya wachezaji wapya waliosajiliwa Simba ni Ibrahim Ajibu, Gadiel Michael, Beno Kakolanya, Francis Kahata raia wa Kenya, Wabrazil Fraga Gerson na Wilker Henrique Da Silva pamoja na Mkongo, Deo Kanda ambao wote kocha anaonekana kuwakubali. Wilker ambaye ni mshambuliaji, ndiye Mbrazil pekee ambaye mpaka sasa anaonekana kuwika huku akifunga bao moja kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya TVET ya nchini humo.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu ambaye yupo kambini nchini Afrika Kusini alisema kuwa, kocha huyo amefurahishwa na kuridhishwa na viwango vya wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo.

 

Rweyemamu alisema, siku hizo walizozitumia mazoezini zimetosha, licha ya kuwa bado ana muda wa kukiandaa kikosi chake, ana matumaini makubwa ya timu hiyo kufanya vema. Aliongeza kuwa, hivi sasa anamalizia vitu vichache vya kuwaongezea wachezaji wake vya kimbinu na kiufundi katika kufunga mabao na kuiimarisha safu ya ulinzi.

“Tulipofika hapa kambini Sauzi, kocha alianza na program ya mazoezi ya kuiandaa miili ya wachezaji kwa kuwafanyisha mazoezi ya fitinesi uwanjani na gym pekee ambayo alitumia siku tano. “Baada ya kumaliza program hiyo, mwanzoni mwa wiki iliyopita alihamia kwenye program ya mazoezi ya mbinu za kiufundi za kushambulia kwa washambuliaji, pia kuiboresha safu ya ulinzi.

 

“Na sasa yupo katika hatua za mwishoni za kukamilisha kukisuka kikosi chake kwa kuangalia sehemu zenye upungufu na kikubwa ni baada ya kuridhishwa na viwango vya wachezaji wake wakiwemo wa zamani na wapya baada ya kuwaona kwenye michezo mitatu ya kirafiki waliyocheza,” alisema Rweyemamu.

 

Naye Aussems alizungumza kuhusiana na hilo ambapo alisema: “Nimeridhishwa na ninachokiona lakini huu ni mwanzo wa maandalizi bado tuna muda. “Natengeneza kikosi bora kwa ajili ya msimu ujao na nimefanikiwa kwa kiasi fulani mpaka sasa kuwaandaa vijana na nimeona wote wapo vizuri na wanajuhudi kubwa uwanjani.”

ONA MAGUFULI ALIVYOSAFIRI KWA TRENI LEO, HELCOPTER IKIMSINDIKIZA!

Comments are closed.