The House of Favourite Newspapers

Zahera: Yondani Hawezi Kugoma Yanga

Mkongomani Mwinyi Zahera.

KOCHA mkuu wa Yanga, Mkongomani Mwinyi Zahera amemtetea beki wake mkongwe, Kelvin Yondani kuwa kamwe hawezi kugoma. Kocha huyo amefunguka juu ya suala hilo kutokana na kitendo cha beki huyo mkongwe kutojiunga kwenye kambi ya timu hiyo ambayo ipo mkoani Morogoro.

 

Yondani, Juma Abdul na Andrew Vicent ndiyo wachezaji pekee wa Yanga ambao hawakuripoti katika kambi ya timu hiyo ambapo awali ilidaiwa kwamba waligomea wakidai fedha zao.

 

Zahera ameliambia Spoti Xtra, kuwa wengi hawajui kwamba Yondani hakugoma kujiunga na timu hiyo badala yake alipewa mapumziko maalum baada ya kumalizika kwa Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) ambapo siku ambayo alitakiwa kutua Morogoro ndipo akaitwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo inacheza leo Jumapili na Kenya.

 

“Mimi nashangazwa na hili ambalo linaendelea, kusema kwamba Yondani amegomea kambi siyo kweli kwa sababu alikuwa na mapumziko maalum baada ya kutoka Afcon.

 

“Siku ambayo alitakiwa kujiunga na wenzake, ndiyo ambayo Stars ilianza mazoezi yake ndiyo maana akaenda huko, lakini siyo kwamba aligomea kujiunga kwenye timu kama inavyosemwa,” alisema Zahera ambaye ameutema uraia wa DR Congo.

Comments are closed.