The House of Favourite Newspapers

Mbelgiji Wa Simba Avujisha Siri Mabao Ya Kagere

 

KWA mara ya kwanza Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, amefungukia siri na mbinu za mabao anayofunga mshambuliaji wake tegemeo, Mnyarwanda, Meddie Kagere.

 

Mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita aliumaliza akiwa mfungaji bora akifunga mabao 23, ameweka rekodi ya kipekee ya kucheza michezo mitano na kila mmoja ametupia wavuni.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Aussems alisema kuwa mshambuliaji huyo siri yake kubwa ya kufunga ni kufuata maelekezo yake ya kumtaka muda wote atembee ndani ya 18 na 6 kwenye goli la wapinzani.

 

Aussems alisema lengo la kumtaka acheze umbali huo ni kwa ajili ya kusubiria makosa ya mabeki na makipa kabla ya kuyatumia kufunga mabao.

 

Aliongeza kuwa hilo lipo wazi hadi hivi sasa hakuna bao alilolifunga la umbali wa mita 20, yote ni ndani ya 6 na 18 kwa njia ya kichwa au kumchambua kipa, siyo shuti.

 

“Kagere siyo mzuri katika kukaa mpira na kupiga chenga, hilo nililiona mapema tu na ndiyo sababu ya kumtaka yeye kusubiria mipira akiwa ndani ya 6 na 18 kwa ajili ya kufunga.

 

“Hivyo, baada ya kugundua siyo mzuri katika kupiga chenga huku akiwa anakokota mpira nikambadilishia majukumu kwa kumpa kazi ya kutembea eneo la 6 na 18 akisubiria upungufu wa makipa na mabeki wa timu pinzani.

 

“Nimemtaka Kagere muda wote kutokauka maeneo hayo ya hatari akisubiria mipira kutoka kwa wachezaji wenzake, ninaendelea kumpa mbinu zaidi za kuhakikisha anaendelea kufunga, ipo programu maalum nimemuandalia,” alisema Aussems.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Comments are closed.