The House of Favourite Newspapers

Mbelgiji Yanga Ambakisha Lamine Moro

0

IMEBAINIKA kwamba Mbelgiji Luc Eymael ndiye ambaye amehusika kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kikosi hicho kinampiga pini beki wake kisiki, Lamine Moro, raia wa Ghana.

 

Iko hivi; Moro ameongeza mkataba mpya wa miaka miwili ambayo inamfanya kubakia na Yanga hadi mwaka 2023 baada ya mkataba wake wa awali kuwa unafika ukingoni mwaka 2021.

 

Sasa Eymael ndiye ambaye amewaambia mabosi wa timu hiyo kwamba ni muhimu kwa beki huyo kubakia kikosini hapo, baada ya yeye mwenyewe kuomba kuongezewa mkataba mrefu wa kubakia klabuni hapo.

Lamine alitua Yanga msimu huu akitokea Buildcon ya Zambia na alifanya kazi ya kumdhibiti vilivyo straika wa Simba, Meddie Kagere kwenye mechi ya Kariakoo Dabi iliyopigwa Machi 8, na Yanga kushinda bao 1-0.

 

Habari ambazo Championi Jumatatu, limezipata ni kuwa Eymael ndiye ambaye amehusika kumbakisha beki huyo baada ya kuwaambia mabosi wa timu hiyo kuwa wamuongezee mkataba kwa kuwa awali mwenyewe aliomba mkataba mpya.

 

“Mwanzo ilikuwa Lamine ndiye aliomba aongezewe mkataba licha ya kwamba bado alikuwa na mkataba hadi mwaka 2021.

 

“Baada ya hilo ndipo akaulizwa kocha Eymael ambapo kwa upande wake aliwaambia mabosi wampe mkataba huo mpya kwa sababu ni mmoja wa wachezaji ambao wapo kwenye hesabu zake kwa msimu ujao, ndiyo maana umeona Lamine amesaini mkataba mpya,” kilisema chanzo hicho.

 

Championi Jumatatu lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Yanga, Hassan Bumbuli ambapo alisema: “Hilo suala ndiyo lipo hivyo, Lamine alitaka mkataba na kocha ndiye amemuidhinisha kupewa mkataba mpya wa kuendelea kubakia hapa.

 

“Lakini nje ya Lamine, hakuna mchezaji ambaye amepewa mkataba, tunaendelea na mazungumzo na kila kitu kikiwa sawa basi tutasema.”

STORI NA SAID ALLY, CHAMPIONI JUMATATU

Leave A Reply