The House of Favourite Newspapers

MBIVU, MBICHI PENZI LA MARIOO, MIMI MARS

0

MARIOO jina lake halisi ni Omary Ally Mwanga. Huyu jamaa anatajwa kuwa ndiye mfalme ajaye wa muziki wa Bongo Fleva.  Marioo ambaye ameachia ngoma mpya ya Aya na inafanya vizuri, amefunguka mbivu na mbichi juu ya tetesi za kutoka kimapenzi na mrembo anayefanya Bongo Fleva, Marianne Mdee ‘Mimi Mars’ aliyefanya naye ngoma ya Una.

Ili kujua kinagaubaga juu ya kinachoendelea kati ya wawili hao, Gazeti la IJUMAA linamleta hapa Marioo ambaye amefunguka mengi juu ya ishu hiyo na muziki wake kwa jumla.

IJUMAA: Ni msanii gani alikushawishi au kukuvutia hadi ukaacha kazi yako ya fundi gereji na kuingia kwenye muziki?

Mario: Ni wengi sana. Nilikuwa ninatamani kuwa kama wao, lakini kati ya hao wengi, kuna mmoja ambaye ni Diamond Platnumz (Nasibu Abdul).

Kiukweli Chibu (Diamond) ni mtu ambaye alinifanya nipende sana muziki. Amekuwa akiwavutia vijana wengi sana. Diamond anajua kucheza na akili za mashabiki. Pia ni mtu ambaye anatamani watu wote wafanikiwe. Natamani sana kuwa kama yeye. Pia kuna wasanii wengine wawili ambao ni King Kiba (Ali Saleh Kiba) na Rich Mavoko (Richard Martin). Hawa jamaa niliwapenda na ninawapenda na kutamani kuwa kama wao, lakini zaidizaidi ni Diamond tu aisee.

IJUMAA: Kwa mwaka 2019, mashabiki na baadhi ya wasanii wenzako walikusifu mno kwa kile ambacho ulikifanya, wanasema ulifanya mambo makubwa kwenye gemu ndani ya muda mfupi, kwa mwaka 2020 watarajie nini?

Mario: (anacheka) nashukuru sana kwa comments (maoni) yao, nimezipokea vizuri. Kikubwa ni kuzidi kujituma kwani mwaka juzi nilivyoanza muziki na Ngoma ya Dar Pagumu haikuwa kazi rahisi. Ni kweli mwaka jana nilifanya vizuri. Kwa hiyo niseme tu kwamba nitazidi kuchana mawimbi mwaka huu na ninaahidi kufanya mambo mengi makubwa kiasi cha kushangaza dunia.

IJUMAA: Ni muda sasa kumekuwa na tetesi kwenye mitandao ya kijamii kwamba unatoka kimapenzi na Mimi Mars tangu ulipofanya naye Ngoma ya Una, je, ukweli ni upi kuhusiana na ishu hiyo?

Marioo: Hakuna ukweli wowote kuhusiana na hilo. Mimi na Mimi Mars ni marafiki wa kawaida tu, tumezoeana, lakini hatuna uhusiano wa aina hiyo, hayo ni mambo ya mitandao tu.

IJUMAA: Ni wimbo gani uliokufanya ukajulikana?

Marioo: Ngoma zote kwa kweli zilinifanya nikajulikana kwa sababu kila ngoma yangu ilikuwa na maana yake na watu walikuwa wanapenda sana kusikiliza, ninamshukuru Mungu kwa hilo.

IJUMAA: Ngoma yako ya Inatosha iliteka mno hisia za mashabiki wako, kila mtu alikuwa anajirekodi, anaimba. Je, ni stori ya kweli au?

Marioo: Hapana… ni wimbo tu niliamua kuimba wala hakuna kitu cha kweli hapo. Mimi nilikaaa, nikatunga, basi nikaimba ila hata mimi ninashangaa kuona ni wimbo ambao umegusa wengi sana. Pia ni moja ya nyimbo zangu ambazo zimekuwa na comments (maoni) nyingi sana kwenye Mtandao wa YouTube, lakini hata ukiangalia nusu ya dunia hivi sasa wanateseka na mapenzi.

IJUMAA: Watu wanatamani kumjua Marioo ni mtu wa aina gani?

Marioo: Ni mtu anayependa sana kujishughulisha. Pia ana uchu wa kupata maendeleo. Ila kiukweli mtu huwezi kujijua wewe ni wa aina gani, bali watu wanaokuona ndiyo wanajua. Cha msingi waendelee tu kunifuatilia, nadhani watanifahamu vizuri.

IJUMAA: Vipi kuhusu usimamizi, unajisimamia mwenyewe au unasimamiwa na uongozi wako?

Marioo: Mimi ninaji-manage (ninajisimamia) mwenyewe kila kitu. Hapa nilipo bado sijapata management.

IJUMAA: Nini mipango yako ya baadaye au unajiona wapi baada ya mwaka huu?

Marioo: Malengo yangu ni kuupeleka muziki wa Bongo Fleva mbali huko duniani. Kama ilivyo kwa wasanii wengi, nami natamani kufanya kolabo na wasanii wakubwa duniani, hilo najua litafanikiwa kwani plans (mipango) zipo nyingi, zikitiki tu, mashabiki watanisikia.

IJUMAA: Unawaambia nini mashabiki wako?

Marioo: Ninawapenda sana, ninawaomba waendelee kunisapoti. Tupo kwenye competition (ushindani) kubwa ya muziki. Mimi kama msaniii mpya ninawaahidi kufika mbali hivyo wasiniache na mimi sitawaangusha.

Makala: Khadija Bakari 

Leave A Reply