The House of Favourite Newspapers

Mbivu,mbichi Yamoto Band Hizi Hapa!

USIKU wa Septemba 21, 2014 ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar kulikuwa na tukio moja kubwa katika Muziki wa Bongo Fleva ambapo vijana wanne, Aslay, Enock Bella, Beka Flavour pamoja na Maromboso walitengeneza historia ya kuanzisha Yamoto Band.

 

Yamoto Band kipindi hicho ilikuwa ikitambulisha wimbo wao wa kwanza ulioitwa Yamoto. Nilipata bahati ya kuwa mmoja wa wahudhuriaji na nikiri siku hiyo niliwaangalia kwa jicho la tatu kuwa vijana watakuja kuwa moto wa kuotea mbali kama alivyosema siku hiyo Mzee Yusuf ambaye alialikwa kuwasindikiza.

 

Mwaka mmoja baadaye, Yamoto Band ilikuwa miongoni mwa bendi za vijana zinazotikisa wakiwa na ngoma kibao kama vile Nitajuta, Niseme, Nisambazie Raha, Nitakupelepweta na nyingine kibao.

Yamoto ilikuwa yamoto kweli, walipata mashavu ya kutosha ndani na nje ya nchi na miongoni mwa nchi walizofanya shoo ni Norway, Sweden, Uswisi, Denmark pamoja na Ujerumani.

 

Oktoba, mwaka jana taarifa zilianza kusambaa kuwa Yamoto Band imekufa, Mkurugenzi wa Mkubwa na Wanawe aliyekuwa akiwasimamia, Said Fella alitoa ufafanuzi kuwa kuendesha bendi imekuwa kazi kubwa hivyo umefika wakati kila mmoja kufanya kazi peke yake na wanapohitajika kwa pamoja watajikusanya.

Ni ukweli kuwa, tangu waachie ngoma ya pamoja ya Mama na Suu, mwaka 2015/16 hawajawahi kuwa pamoja tena.

 

NGOMA ZAO:

Aslay kwa sasa anafanya poa, ameendelea kufanya muziki kivyake, alianza kuachia vibao mfululizo na kwa mwaka jana pekee alifanikiwa kutoa ngoma zaidi ya kumi zikiwemo Natamba, Mahabuba, Likizo, Hauna, Pusha, Angekuona, Baby, Nyakunyaku, Koko, Marioo na nyinginezo. Mwaka huu pia upo poa kwake kwani anaendelea kubamba na Ngoma ya Nibebe.

 

Beka Flavour naye ameonesha kukubalika tangu ajitenge na wenzake, Ngoma ya Libebe ndiyo iliyomtoa na kwa sasa anaendelea kutikisa na ngoma kibao kama vile Sikinai, Kibenteni, Sarafina, Tuwasare pamoja na Umenimaliza.

Maromboso kwa sasa amebadili jina na kujiita Mbosso, hadi sasa ana ngoma kadhaa ambazo anatoa mfululizo kama ilivyokuwa kwa Aslay na Beka Flavour. Ngoma zake zote amezitoa mwaka huu ambazo ni Shida, Alele, Nimekuzoea, Watakubali na Picha Yake.

 

Enock Bella a.k.a Mabesi naye hayupo nyuma sana, anashikilia ngoma mbili mkononi ambazo ni Sauda ya mwaka jana mwishoni na Nitazoea ya mwaka huu.

 

MAISHA YAO:

Japokuwa amekuwa hapendi kulizungumzia hili lakini Aslay anadaiwa kuwepo chini ya kituo kimoja cha redio na ndiyo wanaomsimamia kuanzia audio, video hadi shoo zake. Beka Flavour anasimamiwa na mdau wa muziki anayefahamika kwa jina moja la Siraji wakati Mbosso akisimamiwa na Diamond Platnumz chini ya lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WCB), Enock Bella yeye hadi sasa hajapata wa kumsimamia japokuwa anatafuta msimamizi wa kazi zake.

 

NYUMBA ZAO ZILE VIPI?

Wakiwa ndani ya Yamoto Band, kutokana na mchango wao waliouonesha katika kazi zao, walijengewa nyumba za kuishi eneo moja pande za Mbande-Kisewe.

Hadi sasa hawajakabishwa na zipo chini ya Fella, mbili zimekamilika kila kitu na mbili zilizobaki zipo katika hatua ya mwisho kumalizika.

Kwa mujibu wa Beka Flavour, aliomba wapatiwe nyumba hizo ili wamalizie wenyewe.

 

WADAU WANASEMAJE?

Wadau wengi wa Muziki wa Bongo Fleva, wamezungumzia juu ya kuvunjika kwa kundi hili ambapo wapo wanaopenda waendelee kila mmoja kivyake na wapo wanaopenda Yamoto Band irudi.

Jacqueline Emmanuel wa Mwenge jijini Dar anasema kuwa yeye ni mpenzi mkubwa wa Yamoto Band na kuwepo mmojammoja kumepoteza ladha.

 

“Kuna ‘chemistry’ ambayo mwanamuziki akikutana na mwenzake basi hutokea kitu cha kitofauti sana. Ukimchukua Aslay, sauti yake ukaichanganya na Beka Flavour halafu unampata Mbosso mwisho unaweka besi la Enock Bella lazima ngoma iwe kali na ndiyo maana Yamoto Band ilikuwa ya kitofauti. Napendelea warudi bendi kama bendi,” anasema Jacqueline.

Josee wa Samaki-Samaki, Masaki anasema kuwa kila mmoja aendelee kuwa kivyake.

 

“Uwezo siku zote huwa kwa mmoja mmoja. Walipokuwa kundi ilikuwa vigumu kutambua uwezo wa kila mmoja. Leo hii Aslay kumbe alikuwa na vitu adimu tunamsikia, Beka Flavour naye kumbe alikuwa anaweza kusimama peke yake na kuwa na mashabiki wake.”

Daniel ‘kinyozi’ wa Bamaga jijini Dar anasema walipokuwa kundi wapo waliokuwa wakifichwa.

“Waendelee kubaki hivihivi, leo hii ambao wana uwezo mdogo tumewaona na wenye uwezo tumewajua.

Makala: Andrew Carlos.

Comments are closed.