The House of Favourite Newspapers

MBOWE, MATIKO WAWATAKIA CHADEMA SIKUKUU NJEMA, WARUDISHWA LUPANGO

KESI Na. 112/2018 ya uchochezi inayowakabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Mbunge wa Tarime mjini, Ester Matiko na viongozi wengine saba wa chama hicho imeahirishwa leo Desemba 21, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi January 3, 2019.

 

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, amesema mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na kudai kuwa hawana taarifa yoyote kuhusu kinachoendelea mahakama ya juu hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

 

Wakili Faraja Mangula alidai kuwa Wakili wa washitakiwa hao Peter Kibatala na Sheck Mfinanga wamepata dharura hivyo wanaomba mahakama ipange kesi hiyo kusikilizwa Januari 4, mwakani lakini akijibu hoja hiyo, Wakili Simon amedai wanaiachia mahakama ipange tarehe itakayoona inafaa.

 

Hakimu Mashauri amesema January 4, mwakani atakuwa na kazi nyingine hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi January 3, mwaka huo. Baada ya kuelezwa hayo, Mbowe na Matiko waliwakia wafuasi wao heri ya sikukuu wakiamini kuwa hawawezi kutoka gerezani kwa kipindi hiki.

 

Washitakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu.

Comments are closed.