The House of Favourite Newspapers

Mchezo Umeisha, Ngoma Anarudi Yanga

YANGA inasita kuwapa mikataba washambuliaji wawili wa kigeni walio katika rada zake, lakini kwa hali ilivyo kuna uwezekano straika Donald Ngoma akabaki Jangwani licha ya misimamo ya kocha George Lwandamina.

Lwandamina inadaiwa kwamba ameuambia uongozi kwamba hapendi utovu wa nidhamu wa mchezaji huyo ambaye aliondoka na kurudi kwao bila taarifa yoyote.

 

Baadhi ya viongozi wanaamini suala la Ngoma linakuzwa na kuonekana kubwa lakini wao wamepanga kulimaliza kwa amani kwa pande zote mbili.

Kocha tayari amemzuia Ngoma kufanya mazoezi na amepigwa akijipiga picha na kutupia kwenye mitandao ya kijamii kuonyesha huko aliko anafanya mazoezi ya gym.

 

Yanga awali ilifikiria kumpiga chini na kununua straika mwingine kutoka nje huku ikiangalia pia hali ya majeraha ya Amissi Tambwe kabla dirisha dogo halijafungwa.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika alisema suala la Ngoma siyo kubwa na haliwezi kufikia hatua ya kumtimua mshambuliaji huyo.

 

Nyika alisema suala la Ngoma ni dogo ambalo lipo kwenye hatua za mwisho baada ya kikao na Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa na kutoa maelezo yake ambayo yamefikia pazuri na wakati wowote atajiunga na timu.

 

“Ishu ya Ngoma na klabu siyo kubwa kama wengi wanavyofikiria na uzuri ni kwamba mchezaji mwenyewe alikutana na katibu na kufanya naye kikao na kikubwa alikuwa akisikilizwa utetezi wake baada ya kuondoka nchini bila ya ruhusa.

 

“Na wakati matatizo hayo yanatokea, mimi sikuwepo nchini, hivyo nilishindwa kulitolea ufafanuzi na maamuzi kutokana na kukosa taarifa za upande wa pili wa mchezaji.

“Hii ishu haiwezi kufikia kubaya kama watu wanavyofikiria na hivi karibuni litaisha na mchezaji atarudi kwenye timu, najua mengi yamezungumzwa juu ya Ngoma, lakini yataisha,” alisema Nyika.

 

Aliongeza kuwa, anataka kuona suala hilo linamalizika haraka na lisifikie katika hatua iliyofikia ya kufikishana kwenye Kamati ya Nidhamu ya timu hiyo inayonolewa na George Lwandamina raia wa Zambia.

Ngoma wiki iliyopita alirejea nchini akitokea kwao Zimbabwe akiwa na ripoti ya daktari wake aliyekuwa anamtibia na kuiwasilisha kwa Mkwasa.

Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Comments are closed.