The House of Favourite Newspapers

Meli Aina ya Frontier Ace Yatua Bandari ya Dar es Salaam Ikiwa na Magari 40,41

0
                  Meli aina ya Frontier Ace imetoka moja kwa moja Japan hadi Bandari ya Dar es Salaam

MELI ya mizigo aina ya Frontier Ace iliyobeba magari 4,041 imewasili katika Bandari ya Dar es Salaam leo April 8 2022 na ikiweka rekodi ya kuwa Meli ya kwanza kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa na mzigo mkubwa Zaidi wa magari tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania.

 

Meli ya Frontier Ace ina ukubwa wa GRT 52,276 na urefu wa mita 189.45 imewasili moja kwa moja kutoka nchini Japan.

 

Mwanzo rekodi ilikuwa inashikiliwa na Meli aina ya Tranquailace (IMO: 9561253) inayomilikiwa na Kampuni ya Mitsui ambayo ilitia nanga katika bandari ya Dar es Salaam Agosti 10, 2021 ikiwa na jumla ya magari 3,743. Ambapo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Eric Hamissi aliisifia na kuelezea kuwa imeweka rekodi na historia ya kuwa Meli iliyotia nanga ikiwa na mzigo mkubwa Zaidi.

 

Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameitaka TPA kufanya kazi usiku na mchana na kuongeza juhudi kuhakikisha mzigo huo unapakuliwa mapema licha ya kwamba mamlaka inakabiriwa na uhaba wa vifaa.

 

Pia ametoa maagizo juu ya kuongeza uaminifu na umakini mkubwa katika mizigo ya wateja lakini pia akiwaasa viongozi wa Mamlaka ya bandari hiyo kwamba ufanisi wao wa kazi ndiyo utaongeza uaminifu kwa mataifa mengine kuendelea na kuanza kutumia Bandari ya Dar es Salaam.

 

“Sio sawa mtu leo ameletewa gari lake anakuta halina kioo, najua tumekuwa tukisifika kwa uaminifu basi hili tuliendeleze.” amenukuliwa Profesa Mbarawa.

                                  Meli hii imetua nanga leo katika Bandari ya Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Eric Hamissi amesema kati ya magari 4,041ambayo yamebebwa na meli hiyo, 2,936 yatasafirishwa kwenda katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Msumbiji, Burundi, Sudani, Malawi, Zambia, Uganda na Zimbabwe huku mengine 1,105 yakibaki hapahapa nchini.

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Balozi Ernest Mangu amesema menejimenti inawasiliana na mamlaka mbalimbali kuhakikisha inatekeleza maagizo kutoka kwa Rais ya ukaguzi wa magari kufanyika nje ya nchi.

 

Leave A Reply