The House of Favourite Newspapers

Meya Dar Ataka Kiswahili Kifundishiwe Sekondari, Vyuo

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, akizungumza jambo katika siku ya mashindano ya mashairi.
Afisa Rasilimali Watu kutoka kampuni ya Mabati ya ALAF ambao ndiyo wadhamini wa mashindano hayo,  Angela Tukai,  akizungumza na washiriki wa mashindano. 
Washiriki wa mashindano ya mashairi wakitoa heshma kwa mstahiki Meya wa jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita wakati akiingia ukumbini kwa ajili ya kufungua mashindano hayo.
Jaji wa mashindano akizungumza jambo.

MSTAHIKI Meya wa jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, ameishauri serikali kuanza kutumia lugha ya Kiswahili katika kufundisha masomo ya shule za msingi, sekondari na vyuo ili kuwawezesha wanafunzi kupata uelewa.

 

 

Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua mashindano  ya mashairi ya Meya wa Jiji lake yaliyodhaminiwa na kampuni ya mabati ya Alaf.

 

 

Amesema ni vyema kama nchi kuthamini lugha ambayo ndiyo inayotuunganisha Watanzania wote na si kuiga lugha za nchi nyingine.

 

“Ukienda Uganda wanazungumza lugha yao na Wakenya pia hutumia lugha zao lakini sisi Watanzania tunapenda kuiga lugha za wenzetu na kuacha kupenda vyetu,” alisema Mwita.

 

 

Alisema wanafunzi wamekuwa wakichelewa kupokea na kuelewa maarifa yanayotolewa kwa lugha ya Kiingereza.

 

 

“Inawawia vigumu wanafunzi wanapoanza masomo ya sekondari kuanza kujifunza lugha mpya wakati huohuo wakipokea maarifa,” alisema Mwita.

 

 

Alisema lugha ya Kiswahili ina uwezo wa kukidhi mahitaji ya kufundishia na kuondoa changamoto iliyopo sasa ya kukariri.

“Lazima nchi iheshimu lugha ya Kiswahili na kuitumia kama njia ya mawasiliano lengo ikiwa ni kuhakikisha inasambaa na kuingia katika nchi za kusini mwa Afrika,” alisema Mwita.

 

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili katika Chuo Kikuuu cha Dar es Salaam,  Dk Elnester Mosha,  alimpongeza Mwita kwa kuanzisha mashindano hayo kwa kuwa yanasaidia kukuza Kiswahili nchini.

 

 

“Nimpongeze Mstahiki Mwita kwa kutambua nafasi ya washairi kwa kuwa katika kukuza lugha,  wao ndiyo wamekuwa wakisaidia kupatikana kwa misamiati na istilahi mbalimbali,” alisema.

Akizungumzia suala la matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia, alisema haiwezekani kupata mabadiliko kwa kutumia maarifa ya kukariri.

 

 

Alisema huwezi kufanya ugunduzi kwa kutumia maarifa ya kukariri ambapo hata tafiti zimeweka bayana kuwa ukimfundisha mwanafunzi kwa lugha anayoielewa vizuri anapata maarifa.

 

Mashindano hayo yameanza leo ambapo jumla ya washairi 51 kutoka halmashauri tano za jijini hapa.

Katika mashindano hayo ambayo yamedhaminiwa na kampuni ya mabati ya ALAF, yatafikia tamati kesho na hivyo washindi kupatiwa zawadi na rais mstaafu wa awamu ya pili,  Ali Hassan Mwinyi.

Na Christina Mwagala, Ofisi ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Comments are closed.