The House of Favourite Newspapers

Mfalme Mswati 111; Anaongoza Kwa Kuwa Na Wake Wengi Afrika

MFALME Mswati 111 (50) wa Swaziland mwaka jana amemuoa mke wa 14, hivyo kuongoza kwa Bara la Afrika kwa kuwa na wake wengi ukilinganisha na wakuu wengine wa nchi barani humu.

 

Msichana huyo ajulikanaye kwa jina la Siphelele Mashwama ambaye ni mtoto wa mshauri wa Baraza la Mawaziri nchini Swaziland, Jabulile Mashwama, atakuwa amefikisha idadi ya wanawake 14 wa Mfalme tangia aingie kwenye utawala mwaka 1986. Kwa mujibu wa gazeti la HYPERLINK “http://www.maravipost. com/swazi-king-mswati-marriescabinet-minsters-daughter/” Maravi Post taarifa za kuoa kwa mfalme huyo zilithibitishwa na msemaji wa familia hiyo ya kifalme, Hlangabeza Mdluli na kusema kuwa Mfalme Mswati alioa na akaondoka na mrembo huyo kwenda nchini Marekani kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa.

 

Msichana huyo alipatikana kwenye sherehe za msimu wa ngoma za asili zijulikanazo kama ‘Umhlanga Annual Reed Dance’ ambapo mamia ya wasichana wenye bikra hujitokeza wakiwa vifua wazi na kuvaa ‘kihasarahasara’ kujaribu bahati yao ya kuolewa na Mfalme. Mfalme Mswati III alipewa ufalme wa nchi hiyo mwaka 1986 akiwa na umri wa miaka 18 baada ya baba yake mzazi Mfalme Sobhuza II, kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 82.

 

Mfalme ambaye kwao humuita Ngweyama wakiwa na maana simba, huchomoza hadharani kila mwaka kwenye sherehe hiyo akiwa katika mavasi ya kiasili. Swaziland ni moja ya nchi chache duniani ambazo zimebaki kuwa na utawala wa kifalme barani Afrika. Nyingine ni Morocco.

 

Nchi hii ndogo kwa mujibu wa Unicef, ina maambukizi makubwa ya ugonjwa wa Ukimwi kwani watu 210,000 wana maambukizi wakati nchi yenyewe ina watu milioni 1.2 na wengi wao ni wakulima.

 

Mfalme Mswati kwa sasa ana watoto 13 ambapo binti yake wa kwanza Princess Sikhanyiso ana miaka 24 na wengine ni Sibahle Dlamini, Makhosothando Dlamini, Majaha Dlamini, Tiyandza Dlamini, Sakhizwe Dlamini, Saziwangaye Dlamini, Bandzile Dlamini, Lindaninkosi Dlamini, Mcwasho Dlamini, Temtsimba Dlamini na Temaswati Dlamini.

 

Huko nyuma Waziri wa Haki wa Swaziland, Ndumiso Mamba, aliwahi kunaswa akiwa kitandani na mke wa Mfalme wa nchi hiyo, Makhosetive Dlamini. Mamba, alinaswa kwenye kitanda cha mke wa 13 wa mfalme huyo, Nothando Dube na tangu wakati huo, walinzi wa Mfalme Mswati, wamepewa madaraka makubwa ya kuwalinda wake hao.

 

Kwa upande mwingine, inaelezwa kuwa mtindo wa maisha ya Mfalme Mswati na wakeze, umesababisha mpaka sasa akimbiwe na wanawake watatu. Mke wa sita wa mfalme huyo, Angela “LaGija” Dlamini, ndiye anatajwa kuwa mwanamke wa hivi karibuni zaidi kuondoka katika himaya ya mfalme huyo.

Mke wa 12 wa mfalme, Inkhosikati LaDube, alitimuliwa Desemba mwaka juzi kwa kile kilichobainishwa kwamba aligombana na bodigadi wake. Taasisi ya Swaziland Solidarity Network ilieleza kwamba Dlamini, alikimbia makazi ya mfalme baada ya kuwa kwenye mateso kwa miaka kadhaa.

 

Dlamini, aliaga anakwenda kuwasalimia wazazi wake kwenye Mji wa Hhohho, lakini aliporuhusiwa alitimka jumla. Mfalme Mswati pamoja na tabia ya kupenda kuoa mabikra, vilevile anatuhumiwa kujilimbikizia utajiri wa kutisha, hivi karibuni Jarida la Forbes lilimtaja kwamba anamiliki utajiri wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 200 (shilingi bilioni 300).

Comments are closed.