The House of Favourite Newspapers

Mfaransa Ashusha Straika Mbadala Wa Bocco, Okwi

Emmanuel Okwi.

WAKATI Ligi Kuu Bara ikielekea ukingoni Kocha Mkuu wa Simba Mfaransa, Pierre Lechantre amegusia usajili kwa kuwaambia mabosi wake kuwa anahitaji mshambuliaji mwingine tishio wa kimataifa atakayekuwa mbadala wa Mganda, Emmanuel Okwi na John Bocco.

 

Kauli hiyo ameitoa kocha huyo akiwa amefikisha miezi mitatu tangu akabidhiwe majukumu ya kukinoa kikosi hicho kilichokuwa kinafundishwa na na Mcameroon, Joseph Omog.

 

Kwa maana hiyo, kama mahitaji hayo ya kocha yakifanywa ya kusajili mshambuliaji mwingine, basi Mrundi, Laudi Mavugo ataonyeshewa mlango wa kutokea kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kutokana na mkataba wake kumalizika. Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, kocha huyo tayari ametoa mapendekezo hayo na yeye mwenyewe atasimamia mchakato huo wa kumpata mshambuliaji huyo.

John Bocco.

Mtoa taarifa huyo alisema, kocha amekuwa na presha kubwa pale washambuliaji wake Okwi na Bocco wanapoumia na kuwakosa katika mechi zake, hivyo katika kuhakikisha anapunguza presha yake ameomba kuongeza mshambuliaji mwingine mwenye uzoefu wa michuano ya kimataifa na kitaifa.

 

“Mara kadhaa kocha amekuwa akipata presha pale anapomkosa mshambuliaji wake mmoja wapo kati ya Okwi na Boco kutokana na majeraha ambayo yamekuwa yakiwapata katika mechi kadhaa za ligi na michuano ya ligi.

 

“Hivyo, kocha hataki kuona hali hiyo ikimtokea katika msimu ujao wa ligi, hivyo tayari ameanza mikakati ya kukisuka kikosi chake wakati ligi ikielekea ukingoni.

 

“Kocha amesifu uwezo wa Okwi na Bocco ambao wamekuwa wakionyesha, hivyo anafurahia kufanyakazi na wachezaji hao ambao ndiyo wanaibeba timu katika ufungaji, hivyo ameomba mshambuliaji mwingine wa aina hiyo,”alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya timu hiyo ambaye yupo katika kamati ya usajili, Said Tully kuzungumzia hilo alisema kuwa “Hivi sasa kocha na viongozi akili na nguvu zetu tumezielekeza katika ubingwa wa ligi. “Na kama ameongea kocha, basi yatakuwa ni mapendekezo pekee lakini mchakato wa usajili bado hivyo tusubirie kwanza hadi dirisha la usajili litakapofunguliwa,” alisema Tully.

Comments are closed.