The House of Favourite Newspapers

Mganga Mkuu: Tuhakikishe Tunazuia Vifo vya Wajawazito

0

 

MGANGA Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi, amesema kuwa Serikali haitovumilia tena vifo vya akina mama wajawazito vinavyosababishwa na uzembe wa watumishi kazini.

 

Ametoa kauli hiyo leo Desemba 4, 202,  alipokuwa akifunga kikao-kazi cha timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kilichofanyika wilayani Misungwi kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.

 

“Vifo vya akina mama wajawazito havivumiliki tena kwa sasa hivi kwenye hii dunia ambapo tumeingia uchumi wa kati, ni lazima tutafute mbinu mpya na nzuri tuweze kuziendeleza na kuhakikisha kwamba ambaye amekuja kuleta maisha asifariki,” amesema.

 

Amesema siyo vifo vya akina mama wajawazito tu ndivyo vizuiwe bali hata vya watoto wachanga wanaozaliwa pia vidhibitiwe kwa wataalam wa afya kuhakikisha watoto hao wanazaliwa salama pia.

 

Amesisitiza serikali imewekeza rasilimali nyingi kwenye sekta ya afya hivyo ni vyema matunda ya uwekezaji huo yakaenda kuonekana kupitia uboreshwaji wa huduma bora za afya ikiwemo kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.

 

Alishangazwa na vifo vingi vya akina mama wajawazito kutokea katika vituo vya kutolea huduma za afya na si kwenye jamii, na amewataka watumishi hao kujitafakari kuwa ni sehemu gani kuna changamoto ili zifanyiwe kazi na kudhibiti vifo hivyo.

 

“Kabla ya mwezi wa kwanza haujaisha kila mkoa uwe umeshakaa, ukishirikisha viongozi wote wa mkoa, wilaya na halmashauri, vituo vya afya mpaka zahanati, wawe na wawakilishi ili mjadili mbinu ambazo zinaweza kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kwa kiasi kikubwa zaidi,” amesisitiza.

 

Akitoa agizo hilo kwa timu za uongozi wa afya kwa mikoa yote alisema: “Tuondoke hapa tulipo kwa sababu wananchi wanatamani twende tupige hatua moja mbele ili tukaboreshe huduma zetu, kwa mikakati mliyoweka;  tukiitekeleza naamini tunaweza tukatoka kwenye tatizo hili.”

Leave A Reply