MGAO MALI ZA MENGI SHERIA 2 KUMBEBA K-LYNN ZATAJWA!

BAADA ya mfanyabiashara bilionea, Dk Reginald Abraham Mengi kufariki dunia na kuzikwa, masikio ya wengi yamehamia kwenye mgao wa mali zake na hasa urithi wa mjane wake Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K-Lynn’, utakavyokuwa. 

 

Habari zilizopekuliwa na Risasi Mchanganyiko zimeonesha kuwepo kwa madai kuwa mbali na mali nyingine, jumba la kifahari aliloacha bilionea Mengi lililoko mkoani Kilimanjaro litamilikiwa na K- Lynn.

 

Wanaoeneza taarifa hizo hasa kupitia mitandao ya kijamii wanasema, marehemu Mengi alijenga jumba hilo kwa ajili yake na mkewe (K-Lynn), ingawa wanaotoa madai hayo hawaambatinishi na nyaraka za kuonesha kuwa mjane huyo ana haki kisheria. Kwa kawaida mtu anapofariki dunia, wategemezi wake wakiwemo watoto hufungua mirathi na kwamba mgawanyo wa mali huzingatia sheria ya urithi, mirathi na wosia.

 

SHERIA 2 KUMBEBA K-LYNN

Katika sheria hiyo, urithi ambao msingi wake ulianza mwaka 1865, Serikali ya Jamhuri ya Muungano inatambua aina tatu za sheria ambazo hutumika katika kugawa mali za marehemu. Sheria hizo ni; Sheria ya Serikali ya mwaka 1865, Sheria ya Mila ya mwaka 1963 na Sheria ya Dini ya Kiislam ya mwaka 1967.

Hata hivyo, kutokana na imani ya kidini aliyokuwa nayo marehemu Mengi ya Kikristo; ni wazi kuwa warithi wa Mengi hawawezi kutumia Sheria ya Kiislam. Kutotumika kwa sheria hiyo moja kutaifanya familia ya Mengi kutumia moja kati ya sheria mbili zilizobaki kugawa mali za marehemu.

 

Kwa mujibu wa sheria hizo mbili zilizosalia baada ya ile ya Kiislam kukosa sifa yaani ya Sheria ya Serikali na ile ya Kimila inambeba pakubwa K-Lynn kuweza kupata haki ya kumiliki sehemu ya mali za marehemu mumewe.

 

SHERIA YA SERIKALI

Sheria ya Serikali ni Sheria ya Urithi ya India ya mwaka 1865 ambayo ilianza kutumika nchini India mwaka huo na baadaye kuletwa Tanzania (wakati huo Tanganyika) na Serikali ya Wakoloni wa Kiingereza.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mgawanyo wa mali kwa kutumia sheria hii huwa hivi: Kama marehemu ameacha mjane na watoto, mjane atapata 1/3 na watoto 2/3 ya mali yote ya marehemu. Lakini kama marehemu hakuacha watoto, basi mjane ana haki ya kupata ½ na ½ nyingine inayobaki hugawanywa sawasawa kati ya wazazi, kaka na dada za marehemu.

 

ANGALIZO LA SHERIA HII

Hata hivyo, mbali na muongozo uliowekwa na sheria hii; vipengele tajwa vitazingatiwa endepo marehemu hakuacha wosia na kama ameacha mali zitalazimika kugawanywa kwa kufuata wosia wa marehemu.

WOSIA NI NINI?

Wosia ni kauli inayotolewa na mtu wakati wa uhai wake kwa hiari yake kuonesha nia yake jinsi gani angependa mali yake igawanywe baada ya kufa kwake.

AINA ZA WOSIA

Kuna aina mbili za wosia ambazo ni; wa maandishi na wa maneno na kwamba kila mmoja umewekewa sifa ili uweze kutambulika kisheria. Sifa za wosia wa maadishi ni; lazima uandikwe kwa kalamu ya wino na siyo kalamu ya risasi inayoweza kufutwafutwa.

 

Aidha, sifa nyingine ni kwamba anayeandika Wosia huu lazima awe na akili timamu; utaje tarehe ulipoandikwa, utaje pia muusia anausia kwa hiyari yake. Aidha, ushuhudiwe na mashahidi wanaojua kusoma na kuandika angalau wawili (mmoja wa ukoo na mwingine mtu baki), kama muusia anajua kusoma na kuandika.

 

Endapo muusia hajui kusoma na kuandika mashahidi wasiopungua wanne (wawili wa ukoo na wawili watu baki), watahusika na kwamba lazima wosia uwekwe sahihi ya kalamu au dole gumba la kulia na wahusika wote. Hata hivyo, wanaotarajia kurithi hawaruhusiwi kushuhudia wosia huo ambapo aina hii ya wosia inatajwa kuweza kuufuta ule wa maneno, lakini wa maneno hauwezi kuufuta wa maadishi. Wosia wa mdomo lazima; ushuhudiwe na mashahidi wanne (wawili wa ukoo na wawili watu baki).

 

Muusia awe na akili timamu; kama mashahidi watakufa kabla ya muusia kufa, basi Wosia hautakubalika na urithi utagawanywa kadiri ya mpango wa urithi usio wa wosia. Hata hivyo, aina hizi mbili za wosia zinaweza kubatilishwa ikiwa itathibitika kwamba, muusia amepungukiwa akili kwa sababu ya wazimu, ugonjwa, ulevi au hasira ya ghafla na wanaoruhusiwa kupinga wosia ni warithi pekee.

SHERIA YA MILA

Sheria nyingine inayompa K-Lynn au Jack Mengi nafasi ya kurithi mali za marehemu mumewe ni Sheria ya Mila ambao imeweka madaraja matatu ya warithi mali. Madaraja hayo yamewekwa katika sehemu tatu, ambapo daraja la kwanza na la pili limewazungumzia zaidi watoto wa kiume ambao wanatajwa kumiliki kiasi kikubwa cha mali kuliko watoto wa kike. Aidha daraja la tatu limeweka haki ya watoto wa kike huku nafasi ya mjane ambaye kwa marehemu Mengi ni K-Lynn amewekewa kipengele chake kinachoanisha jinsi mjane atakavyoweza kurithi mali za mumewe.

 

Katika kifungu hicho, mjane haruhusiwi mwenyewe kurithi isipokuwa kama ana watoto atategemea urithi wa wanaye. Aidha, sheri hii imelegeza masharti kwa mjane ambaye hana watoto kwamba atalazimika kuishi kwenye nyumba ya marehemu mumewe huku akipatiwa asilimia 20 ya mali za urithi.

 

Inaelezwa, katika Sheria ya Urithi wa Kimila mjane ambaye atapewa mali endapo ataolewa atalazima kupokonywa urithi wake na ugawanywe kwa ndugu wengine. Hii ina maana kwamba, K-Lynn ambaye ni mama wa watoto pacha wa kiume aliozaa na Mengi atanufaika na urithi wao ambao utajumuisha sehemu ya makazi.

 

K-LYNN MIKONONI MWA MSIMAMIZI WA MIRATHI

Kwa mujibu wa Sheria ya Urithi, mirathi na wosia mambo yote yaliyotajwa yatafanyika endapo taratibu za mwanzo za kifamilia zinasimamiwa bila kuwepo kwa migogoro. Sheria inaelekeza kuwa, mara baada ya mtu kufariki dunia warithi wanalazimika kufungua shauri la mirathi mahakamani ambapo msimamizi wa mirathi aliyeaminiwa na ukoo atakuwa na jukumu kubwa la kusimamia mgao wa mali.

 

Kwa msingi huo, kazi ya K-Lynn kupata mgao wa mali za mumewe itakuwa nyepesi kama ndugu wenye sifa za kurithi mali za Mengi na msimamizi wao ambaye si lazima awe miogoni mwa ndugu watamtambua bila pingamizi mjane huyo na kumuingiza kwenye orodha ya majina ya warithi watakaopelekwa mahakamani.

 

TUJIKUMBUSHE

Bilionea Mengi alifariki dunia Mei 2, mwaka huu huko Dubai katika nchi za Falme za Kiarabu ambapo ameacha utajiri unaokadiriwa kufikia shilingi trilioni 1.2. Aidha, mfanyabiashara huyo ameacha mjane ambaye ni K-Lynn, watoto watatu wa kiume, wawili kati yao ni wa K-Lynn na mtoto wa kike mmoja.


Loading...

Toa comment