The House of Favourite Newspapers

MGUNDUZI WA TANZANITE, MZEE NGOMA AZIKWA SAME

MGUNDUZI wa madini ya Tanzanite na Madini ya Jasi Marehemu Jumanne Ngoma ambaye alifariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam Januari 30, 2019, amezikwa leo Jumamosi, Februari 2, 2019 katika Kijiji cha Makanya wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Waziri wa Madini Mhe. Dotto Biteko (Watatu kutoka kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Senyamule na Rais wa wachimbaji wadogo wa madini John Bina, wakiwa katika mazishi ya mzee Jumanne Ngoma, Kijijini kwake Makanya, Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro .

Waziri wa Madini, Dotto Biteko ameongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi hayo, na wakati akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, amesema kwamba marehemu Ngoma ameacha ujumbe kwa vizazi vya sasa na vijavyo kwa kuwa Mwaafrika wa kwanza kugundua Madini ya Tanzanite.

Aidha, Waziri Biteko ameitaka familia na wachimbaji wa Madini ya Tanzanite kuweka kumbukumbu ya uwepo wa mzee Ngoma kwa vizazi vijavyo kama mgunduzi wa Madini ya Tanzanite pamoja na kuweka msisitizo kwa serikali kumtambua kama mwanzilishi wa madini ya hayo.

Kwa upande wake Shekhe wa Msikiti wa Makanya Hamisi Abubakari amesema wanadamu wameumbwa kwa ajili ya kufa na sio kuishi milele ambapo amesema ni jukumu la kila mtu kujiandaa na maisha mapya baada ya kifo.

Akisoma wasifu wa marehemu mzee Jumanne Ngoma mtoto wake wa kike Asha Jumanne amesema mzee ngoma akiwa mdogo aliondoka Makanya na kwenda Mererani kutafuta maisha akijishughulisha na ufugaji na baadaye kwenda kozi ya miezi mitatu ya Madini ndipo alipoanza harakati za ugunduzi wa Madini ya Tanzanite na Madini ya Jasi.

 

Marehemu Jumanne Ngoma amefariki akiwa na umri wa miaka 80 baada ya kuugua ugonjwa wa kiharusi mwaka 2018 na kupatiwa matibabu ndani na nje ya nchi, ameacha watoto nane na wajukuu.

 

Mwaka jana, Mzee Ngoma alipatiwa msaada wa Tsh. Milioni 100 na Rais Dkt. John Magufuli kwa ajili ya kumsaidia katika matibabu yake ya ugonjwa wa kupooza uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.

Septemba 23, 1967, Bw. Ngoma alipewa barua na maabara ya Dodoma iliyosema madini hayo ni Zoisite. Hiyo ndio inajulikana hadi sasa kuwa ni tarehe rasmi ya ugunduzi wa Tanzanite duniani.

 

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema!

Comments are closed.