The House of Favourite Newspapers

Michirizi Ya Damu – 02

0

Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuifunga mipaka yote ya nchi hiyo, uwanja wa ndege kukawekwa ulinzi wa uhakika, sehemu ya kivuko kwa kupitia katika mfereji wa Suez napo kukawekwa ulinzi mkubwa, kila kona, mpaka bandarini kote huko ilikuwa ni kulindwa kwa nguvu zote na kulipokuwa na askari wachache, wakaongezwa wengine kuhakikisha huyo mwanamke anayejulikana kwa jina la Maria Ogabugu hapiti kuondoka nje ya nchi hiyo. Iwe isiwe ilikuwa ni lazima kumatwa na kufikishwa katika mikono ya sheria.

****

Zilisikika kelele za mwanamke kutoka ndani ya chumba kimoja kilichokuwa katika Hoteli ya Melkizedek iliyokuwa ndani ya Jiji la Marseille nchini Ufaransa. Watu wote waliosikia sauti hiyo walishtuka, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, kwa jinsi sauti hiyo ilivyosikika, haikuonekana kuwa ya amani hata kidogo, ilionyesha kabisa kwamba kulikuwa na kitu kikubwa kilitokea.

Wateja wengine waliokuwa katika vyumba vingine wakatoka, walitaka kujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea. Walipotokea ukumbini, macho yao yakatua kwa msichana aliyekuwa mhudumu ndani ya hoteli hiyo akiwa amekaa pembeni kabisa akilia huku akitetemeka kwa hofu kubwa.

Hakukuwa na aliyejua kitu kilichomfanya msichana huyo mrembo kuwa katika hali hiyo. Wakamsogelea kwa lengo la kumuuliza lakini hakujibu kitu, alichokifanya ni kuwaonyeshea chumba kilichokuwa mbele yake ambapo baada ya watu kuufungua mlango wa chumba hicho, macho yao yakatua katika maiti moja iliyokuwa sakafuni.

Kila mmoja alishtuka, hawakujua ni kitu gani kilichokuwa kimetokea. Harakaharaka simu ikapigwa kwenda kwa polisi na kwa meneja wa hoteli hiyo ambapo baada ya meneja kufika, akamuuliza msichana huyo ni kitu gani kilitokea lakini akawaambia hakuwa akijua, alimpelekea mteja kahawa lakini akakutana na maiti hiyo.

Baada ya dakika chache polisi wakafika mahali hapo. Kitu cha kwanza kilikuwa ni kuzungumza na msichana huyo ambaye maelezo yake alisema kwamba alikuwa na utaratibu wa kumpelekea kahawa mteja huyo kila inapofika jioni lakini kitu cha ajabu kabisa, jioni ya siku hiyo akakuta maiti ya mwanaume huyo ndani ya chumba hicho.

Kitu cha kwanza walichokitaka ni kumfahamu mtu ambaye alikuwa ndani ya chumba hicho na mwanaume huyo ambaye hawakujua alikuwa nani kwani alichomwa visu kadhaa shingoni mwake, damu nyingi zilimtoka, nyingine zikauziba uso wake na pale alipoanguka, aliburuzwa na hivyo kufanya michirizi ya damu kuonekana sakafuni.

Walipokwenda mapokezini na kuangalia wateja walioingia, wakaliona jina la mwanaume huyo, aliitwa Belleck Peter, bilionea mkubwa aliyekuwa akimiliki kiwanda cha karatasi na viwanda kadhaa vya kutengeneza mbao vilivyokuwa nchini Marekani.

Kila mtu alishangaa, hawakuamini kama mtu aliyeuawa ndani ya chumba kile alikuwa Belleck. Alijulikana dunia nzima kutoka na utajiri wake mkubwa wa dola za Kimarekani bilioni 7 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 14, aliheshimika na watu wengi walimuita kwa jina la Golden Angel ‘Malaika wa Dhahabu’ kwa jinsi alivyokuwa akiwasaidia watu wengi, hasa vituo vya watoto yatima na masikini waliokuwa wakilala mitaani.

“Is this Belleck I know?” (huyu ni Belleck ninayemfahamu?) aliuliza polisi mmoja huku akionekana kushangaa.

“Yeah! What has happened?” (ndiyo! Hivi ni kitu gani kimetokea?) aliuliza polisi mwingine.

Hakukuwa na aliyejua, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuwatafuta wasichana wote waliokuwa wamelala naye kwani kwa taarifa walizozikuta hotelini hapo ni kwamba tangu Belleck afike katika hoteli hiyo, kazi yake kubwa ilikuwa ni kubadilisha wanawake tu.

Msichana wa kwanza alikuwa Natasha, alichukuliwa kutoka katika mawindo yake ya usiku, wa pili alikuwa Stella na wa tatu alikuwa Neyonce. Wote hao walikuwa wakijiuza mitaani na mtu ambaye walifanya naye biashara yenye malipo makubwa alikuwa mwanaume huyo.

Kila mtu kwa wakati wake wakaingizwa ndani ya chumba cha mahojiano na kuanza kuulizwa kuhusu msichana huyo. Hakukuwa na aliyejua, kitu pekee walichokuwa wakikifahamu ni kwamba walinunuliwa na mwanaume huyo, wakafanya naye mapenzi na kisha kuondoka zao baada ya malipo kufanyika.

“Alors rien n’est arrivé ,” (kwa hiyo hakuna kilichotokea?) aliuliza polisi kwa kutumia Lugha ya Kifaransa.

“Rien ne se passe que le sexe,” (hakuna kilichotokea zaidi ya ngono)

Walihitaji kufahamu ukweli. Taarifa zilisema kwamba mwanaume huyo alikaa hotelini kwa siku nne, na siku zote hizo alikuwa akilala na mwanamke hotelini lakini mpaka muda huo walikuwa wamefanikiwa kuzungumza na wanawake watatu tu, kulikuwa na mmoja alibaki, alikuwa nani? Walihitaji kumfahamu msichana huyo.

Wakaelekea mpaka hotelini na kuwauliza wahudumu. Wengi walikumbuka kwamba siku ya nne mwanaume huyo aliingia na msichana aliyekuwa amevalia nikabu na suruali ya jinsi, alikuwa na shepu bab’ kubwa na nyuma alionekana kujazia hasa, aliingia na bilionea huyo ndani ya chumba kile lakini hawakumuona alipokuwa ametoka, walihisi kwamba huyo ndiye alifanya mauaji.

“Ana muonekano gani?” aliuliza polisi.

“Ni mrefu, kwa muonekano wa macho yake, anaonekana ni mzuri sana, halafu anatembea kwa madaha kama twiga mbali na hayo, mwanamke huyo ana bomba moja kubwa sana kwa nyuma,” alijibu mhudumu mmoja wa kiume.

“Bomba ndiyo nini?”
“Kalio! Kajazia sana.”

“Na alipotoka hamkumuona?”
“Ndiyo! Ila alikuwa naye hotelini!”

Mpaka hapo polisi wakapata uhakika kwamba mtu aliyemuua biliona huyo alikuwa mwanamke ambaye wakati akiingia ndani na bilionea huyo alijitambulisha kwa jina la Victoria. Walitaka kumfahamu msichana huyo, baada ya kuondoka, alielekea mahali gani, na kama hakupitia pale mapokezi, alipitia wapi?

“Na hakuna mtu anayeweza kupitia mlango wa nyuma?” aliuliza polisi.

“Hakuna! Mlango wa nyuma ni kwa ajili ya wafanyakazi tu, tena inabidi uingize namba za siri ambazo zinajulikana kwa wafanyakazi tu,” alijibu msichana mmoja.

Waliwahoji wafanyakazi kadhaa ndani ya hoteli hiyo, kila mmoja alimwambia alichokuwa akikifahamu kuhusu kifo cha bilionea huyo. Wengine wakahisi kwamba alijiua, kwamba aliingia ndani ya chumba kile na kujimaliza mwenyewe kwa kuwa tu alikuwa na mawazo mengi kuhusu mkewe aliyefariki miezi mitatu iliyopita.

Hilo halikuingia akilini mwa polisi, walijua kabisa kulikuwa na mtu aliyemuua bilionea huyo na walihisi kabisa mwanamke huyo wa mwisho aliyeingia naye ndiye aliyefanya mauaji hayo.

Kwa sababu ilikuwa ni hoteli kubwa na yenye kamera ndogo za CCTV, walichokifanya ni kuhitaji picha zilizorekodiwa, wakapelekwa huko kulipokuwa na video na kisha kuangalia kile kilichokuwa kimetokea.

Ni kweli walimuona mwanamke huyo akiingia na bilionea huyo hotelini, sura yake haikuonekana vizuri kwani alivalia vazi la wanawake wa Kiislamu, nikabu ambalo lilificha sura nzima na ni macho tu ndiyo yaliyokuwa yakionekana.

Wakaingia ndani ya chumba hicho ambapo baada ya saa nne, akatoka na kuondoka, hakupitia mlango wa mbele, akapitia mlango wa nyuma na kilichowashangaza sana polisi ni kwa namna gani mwanamke huyo kupita kwenye mlango huo na wakati hakuwa na namba za siri za kufungua mlango huo?

“Aliufungua vipi huo mlango?” aliuliza polisi huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Hata sisi hatujui!”

“Ni lazima kutakuwa na mtu alimpa namba ya siri!”

Wakati wakijadiliana hilo ndani ya chumba hicho kilichokuwa na kompyuta, mara simu ya mkuu wa polisi ikaita ambapo harakaharaka akaipokea na kusikiliza, aliisikia sauti ya mwanaume kwenye simu ambayo ilimwambia kwamba walikutana na kitu cha ajabu baada ya kuitoa maiti ya bilionea Belleck ndani ya chumba kile.

“What is that?” (Kitu gani?) aliuliza.

“We have found a piece of paper written C’est fait on it,” (tumekuta kipande cha karatasi kikiwa kimeandikwa Imekamilika juu yake) alisema jamaa huyo.

“Is it surprising you?” (hicho ndicho kinachokushangaza?)
“It’s the same person who killed Cotton Keith in Giza, Egypt,” (ni mtu yuleyule aliyefanya mauaji ya bilionea Cotton Keith kule Giza nchini Misri) alisikika mwanaume huyo.

“What?” (unasemaje?)
“That it is sir.” (ndiyo hivyo mkuu!)

ITAENDELEA KESHO

Leave A Reply