The House of Favourite Newspapers

Misosi Afungukia Kilichompoteza

Joseph Rushahu a.k.a Bwana Misosi

WAKATI mwanamuziki Joseph Rushahu a.k.a Bwana Misosi anafanya kolabo na wanamuziki kutoka Kenya, Redson na Chameleone wa Uganda iitwayo Heshima, hakukuwepo lindi la wanamuziki kupiga kolabo nje ya mipaka ya Bongo kama ilivyo sasa.

Bwana Misosi aliyetoka na Ngoma ya Nitoke Vipi aliyomshirikisha Hardmard, kwa namna moja au nyingine ni miongoni mwa wanamuziki wa kwanza kabisa kufungua duru hilo la wanamuziki kutoka nje na kufanya kazi na wanamuziki wengine ambao walikuwa wanafanya vizuri.

Heshima yake hiyo katika historia ya muziki Bongo ni muhimu kukumbukwa na baada yake walifuata wengine akiwemo Ambwene Yesaya ‘A.Y’.Mbali na hilo, Bwana Misosi alitamba na ngoma nyingi zikiwemo Mabinti wa Kitanga, Pilato na Game, Mungu Yupo Busy Zaidi Yako na Safari ni Ndefu.

Hata hivyo baada ya kutamba, kupiga shoo kibao na kufanya kolabo mbalimbali kwenye gemu la Bongo Fleva, amepotea na kwa sasa hasikiki kama ilivyokuwa awali. Nini tatizo, anafanya nini kwa sasa? Ungana naye hapa katika mahojiano aliyofanya na Risasi Mchanganyiko:

Risasi: Kaka vipi mbona kimya sana?

Misosi: Ni kweli kabisa, lakini mwaka huu ni lazima narudi upya.

Risasi: Lakini mara nyingi umekuwa ukisema unarudi lakini hufiki nini tatizo ‘bro’?

Misosi: Hakuna tatizo. Ni vile tu pia tunaangalia maisha ‘side B’. Unajua umri pia unakwenda, majukumu yanaongezeka kwa hiyo lazima uangalie ‘future’ zaidi, ndiyo sababu unakuta tunakaa kimya. Sasa mashabiki wakiona upo kimya wengine wanafikiri pengine mtu kafulia na mambo mengine, wakati tupo tu na maisha yanaendelea vizuri lakini ni kwa vile tunafanya vitu vingine.

Risasi: Kwani nje ya muziki unajishughulisha na nini zaidi?

Misosi: Nilikuwa nimeajiriwa. Lakini kwa sasa ninafanya kazi zangu na ninasimamia kampuni yangu mwenyewe ya masuala ya umeme. Kwa hiyo maisha yanakwenda.

Risasi: Bila shaka unafuatilia nini kinaendelea kwenye muziki nchini, unazungumziaje wakongwe kuzidi kupotea?

Misosi: Ndiyo kama nilivyosema awali. Siwezi kuwa na komenti zaidi na kuwazungumzia wengine. Lakini kikubwa ni kwamba umri huwezi kushindana nao. Leo huwezi kunilinganisha mtu kama mimi na mwanamuziki labda Harmonize. Yule ni mdogo wangu kama wa mwisho. Sasa ukitaka nishindane naye kwa sasa haiwezekani kwa maana yeye ni mwepesi na mimi nikiwakilisha wakongwe, nina mambo mengi.

Kwa hiyo ni lazima kuna wakati nitakuwa kimya ninafanya mambo mengine. Ndivyo wakongwe wanavyopotea. Lakini ninashukuru wapo wengine wanafanya vizuri. Kwa mfano Profesa Jay, hivi karibuni ameachia ngoma nzuri ya Pagamisa, anatuwakilisha vyema.

Ukirudi kwa sasa, mwanamuziki gani ambaye unafikiri anaweza kufiti kupiga kolabo na wewe kwenye gemu la Bongo Fleva?

Misosi: Wapo wengi wanaofanya vizuri. Kumtaja mmojammoja naona sitawakumbuka wengine, lakini yeyote anayefanya vizuri ninaweza kufanya naye kazi. Kwa mfano hao kina AliKiba, Diamond na wengineo, naweza kufanya nao kazi.

Risasi: Ulitoa albamu mbili, Nitoke Vipi ya 2004, baadaye ukatoa Kazi Yangu, una mpango wa kufanya albamu nyingine?

Misosi: Mipango ipo. Unajua mbali na kukaa kimya lakini muziki ni kitu ambacho kinakuwa kwenye damu, kwa hiyo kuacha hivihivi si rahisi. Kwa hiyo mipango ya kufanya makubwa zaidi ipo na muda ukifika tutafanya.

Risasi: Una kipi hasa cha kuwaachia mashabiki wako kwa leo?

Misosi: Wasichoke kunisubiri. Nimesema narudi, kweli narudi. Si muda mrefu nitaachia kazi mpya, tena kazi safi ambayo itanirudisha nilipokuwa.

Risasi: Asante sana.

Misosi: Asante pia.

AKALA: BONIPHACE NGUMIJE

Comments are closed.