The House of Favourite Newspapers

Mitazamo Tofauti Rais Samia Kukutana na Lissu Ughaibuni

0

MUDA mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu viongozi mbalimbali wamepongeza hatua hiyo.

Rais Samia na Lissu walikutana jana Jumatano Februari 16, 2022 mjini Brussels nchini Ubelgiji na kuteta masuala mbalimbali yenye maslahi ya ustawi wa Tanzania.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Zuhura Yunus wawili hao walikutana baada ya ombi la Lissu la kukutana na Rais, ombi ambalo mkuu huyo wa nchi aliliridhia.

Muda mfupi baada ya Ikulu kutoa taarifa za viongozi hao kukutana, Lissu ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu 2020 kupitia tiketi ya CHADEMA alitaja mambo matano aliyosema wameyazungumzia na Rais Samia likiwamo kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

 

Hata hivyo, baada ya taarifa za Rais Samia na Lissu kukutana kusambaa kupitia mitandao ya kijami ikiwamo ya Mwananchi, watu mbalimbali walielezea mapokeo yao kuhusu viongozi hao kukutana.

Baadhi ya waliozungumzia suala hilo ni pamoja na viongozi wa Serikali wakiwamo mawaziri.

 

Kupitia akaunti zao za mitandao ya kijamii wakiweka picha zikimuonyesha Rais Samia akiwa amesimama pamoja Lissu huku wakiambatanisha na maneno ‘captions’ wamesema;

“NI MAMA YETU (Taifa letu, Umoja Wetu)” ameandika Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba katika ukurasa wake wa Twitter akiwa ameambatanisha picha tatu za Rais Samia akiwa na Lissu.

 

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kupitia mtandao wa Instagram akiwa ameweka picha ya Rais Samia amesimama na Lissu wakiwa wameshikana mkono, amesema “My President, My Pride. This is Tanzania (Rais wangu, Fahari Yangu, Hii ni Tanzania)”

Andiko la Waziri Ummy liliungwa mkono na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu ambaye aliweka maoni ‘comment’ kwenye posti hiyo akisema “Excelling Diplomacy (Diplomasia bora)”

 

Mwingine aliyezungumzia hilo ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro (DC), Wakili Albert Msando ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram amesema “Tuna Rais bora sana. Hatumlinganishi na yeyote. Sio lazima. Kila mmoja ana kipawa chake. Mh. Mama Samia Suluhu Hassan tutamuelewa tukitaka kuelewa. #Legacy” ameandika Msando.

 

Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuwa hatua ya Rais Samia kukubali kukubali kukutana na Lissu ni ya kupongezwa “Hatimaye hekima imetawala na mlango wa mazungumzo umefunguka. Sisi @ACTwazalendo tokea awali tunasisitiza kwamba mazungumzo ndiyo njia sahihi ya kupata ufumbuzi wa tofauti zetu za kisiasa na kuleta Mabadiliko. Hatua ya Rais kukubali kuonana na Bwana Lissu ni ya kupongeza sana” ameandika Zitto.

 

Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini ambaye ni mwanachama wa CHADEMA, Godbless Lema kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema “Nimefurahi Rais SSH kukutana na Makamu Mkti wetu Tundu Lissu. Kukutana kwao kuna jenga matumaini ktk siku za usoni. Ninajua watakuwa wamejadili kwa kina hali ya nchi yetu na changamoto zake kwa sasa na njia nzuri ya kuzivuka.”

Ameandika Mbunge huyo wa zamani wa Arusha Mjini kupitia ukurasa wake wa Twitter

Leave A Reply