The House of Favourite Newspapers

MKE AMFANYIA MBAYA MUMEWE – VIDEO

SHINYANGA: Kijana aliyefahamika kwa jina la Andrew Albert (26), mkazi wa Kata ya Mhungula, wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga amedai kufanyiwa mbaya na mkewe kwa kumtelekezea mtoto wa kike wa umri wa miaka miwili.

 

Akizungumzia kutendwa huko akiwa katika ofisi za Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (SHIHABI), Andrew alidai kuwa, mkewe ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora alimkimbia kwa madai ya kukosa uhuru wa kufanya mambo yake hivyo akatoweka na mtoto tangu mwaka 2016 kisha kuibuka mwaka 2019 na kumbwagia mtoto huyo.

 

Mwanaume huyo alidai kuwa wakati mkewe akimtelekeza mtoto alitamka kuwa yeye hawezi kukaa na mtoto huyo kwa kuwa huko alikokuwa alikuwa akishindwa kufanya mambo yake.

Mwandishi wa habari hizi alipotaka kujua kwa nini alifika katika ofisi za SHIHABI, mwanaume huyo alifafanua kuwa, lengo ni kutoa taarifa rasmi katika shirika hilo kuwa mtoto huyo yupo chini ya malezi ya baba kwa sasa.

 

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu jambo hilo, Mwanasheria wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu (SHIHABI), Wilaya ya Kahama, Pius Mpondi alisema sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 inatambua mtu yeyote aliye chini ya miaka 18 ni mtoto.

 

“Dhana ya kisheria inayokanushika inafafanua kwamba mtoto wa chini ya miaka saba inapotokea kuna mgogoro wa ndoa utakaosababisha wazazi kutengana, mtoto huyo atakuwa chini ya uangalizi wa mama.

“Lakini kwa dhana hiyohiyo inayokanushika, mtoto anaweza akawa chini ya baba ikiwa itathibitika kuwa mama anaishi katika mazingira hatarishi kwa ustawi wa mtoto, mfano mazingira ya uasherati pamoja na ulevi,” alifafanua mwanasheria huyo.

 

Naye Paskazia Albert ambaye ni shangazi wa mtoto huyo alieleza kushangazwa na wifi yake kwa uamuzi mbovu wa kutelekeza mtoto kisa akidai ananyimwa uhuru wa kufanya mambo yake.

“Mimi nimshukuru kwa kumleta mtoto wetu akiwa salama, nitamsaidia kaka yangu kulea wakati akiwa anamtafutia mahitaji mengine, lakini namsikitikia wifi yangu kitendo cha kudai ananyimwa uhuru wa kufanya mambo yake, ni kibaya na hakupaswa kumfanyia kaka yangu,” alisema shangazi huyo wa mtoto.

 

Stori: Paul Kayanda, Amani

INASIKITISHA! Mke Amfanyia Mbaya Mumewe!

Comments are closed.