The House of Favourite Newspapers

Mke, mume wapofuka macho

Na Deogratius Mongela
“Nilizaliwa mkoani Tanga miaka 60 iliyopita nikiwa na ulemavu wa macho (upofu), nikakulia katika mazingira magumu kwani ukiachilia mbali kukosa uwezo wa kuona, wazazi wangu hawakuwa na uwezo wa kunipatia mahitaji yangu muhimu, jambo lililofanya niishi katika mazingira magumu sana utotoni,” anaeleza Amiri Abdul, mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na Gazeti la Uwazi.

Amiri ambaye kwa muda wa miaka miwili mfululizo maisha yake yote yamekuwa ni kitandani tu, akiwa hana hata uwezo wa kuamka, anaendelea kueleza kwamba kwa kudra za Mungu, alikua vizuri hadi akafikia hatua ya utu uzima lakini kutokana na ugumu wa maisha ya kijijini, aliamua kusafiri kuja Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta unafuu wa maisha.

AMUOA KIPOFU MWENZAKE
Kwa masikitiko, Amiri anaeleza kwamba kutokana na umri kwenda, aliamua kutafuta mwenzi wa kuishi naye lakini kwa sababu ya hali yake hiyo, ilimuwia vigumu kupata mchumba wa kumuoa kwani kila mwanamke aliyekuwa akienda kumposa, alikuwa akimkataa kutokana na hali yake hiyo.

“Kwa bahati nzuri nikampata kipofu mwenzangu, Halima Kassim, nikamchumbia na hatimaye tukafunga ndoa mwaka 1977.

Tukayaanza maisha mapya kama mume na mke,” anaeleza Amiri na kuongeza kuwa maisha yao ya ndoa yamekuwa yakigubikwa na changamoto nyingi kwani ukiachilia mbali upofu, hawana kazi yoyote ya kuwaingizia kipato, jambo lililosababisha waishi kwa kuombaomba.

Amiri anaendelea kueleza kwamba, katika maisha yao ya ndoa, wamebahatika kupata watoto wanne wenye afya njema lakini bado tatizo limekuwa ni namna ya kumudu malezi ya watoto hao hasa ukizingatia kwamba wanaishi kwa kutegemea kuombaomba kwa wasamaria wema.

“Huwa nakwenda misikitini kuombaomba, kinachopatikana ndiyo nakula na familia yangu, siku nyingine tukikosa basi tunalala na kumshukuru Mungu,” anasema Amiri.

MUME APATWA NA MATATIZO YA MOYO
“Miaka miwili iliyopita, mwaka 2013 nilianza kuona dalili zisizo za kawaida katika mwili wangu, mwili ukawa unavimba, presha za mara kwa mara zikawa zinaniandama. Wasamaria wema wakanisaidia kunipeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo baada ya kupimwa, nilibainika kuwa na matatizo ya moyo.

“Nikaambiwa ili nipate matibabu natakiwa kupelekwa nchini India kwa matibabu, nikaambiwa nitafute shilingi milioni nane pamoja na nauli ya kwenda na kurudi. Kutokana na hali yangu, nikashindwa kupata kiwango hicho kwani hata kula kwangu na familia yangu ni tatizo,” anasema Amiri na kueleza kwamba kutokana na kukosa fedha hizo, ilibidi arudishwe nyumbani.

“Hali yangu ikazidi kuwa mbaya, ikafika kipindi nikawa siwezi hata kunyanyuka kitandani, nimekuwa ni mtu wa kulala tu hapa kitandani kama unavyoniona, familia yangu nayo inateseka kwa sababu siwezi tena kuinuka kwenda kuomba mitaani au misikitini. Wasamaria wema wakija kuniona ndiyo angalau napata vijisenti vya kula na familia yangu.

“Nawaomba Watanzania wanisaidie kwani nimeshakata tamaa, siwezi kupata hizo fedha za matibabu, nasubiria kufa tu,” anahitimisha Amiri kwa masikitiko.

Kwa upande wake, mke wa Amiri ambaye pia ni mlemavu wa macho Halima (53), amewaomba wasamaria wema kumsaidia mume wake ili aweze kupata matibabu ya ugonjwa huo na kurudi katika hali ya kawaida kwani anapata mateso sana hasa nyakati za usiku.

Kwa yeyote aliyeguswa, anaweza kuwasiliana naye kwa namba hizi za simu: 0686 934 110, 0712 686 905.

Comments are closed.