The House of Favourite Newspapers

Mke, Mume Wazua Timbwili, Wausimamisha Mtaa!

TIMBWILI! Hicho ndicho kimetokea baada ya mwanamke Tausi Juma kuibua sekeseke na mumewe, Ally Hamis Makapila, wote wakazi wa mjini hapa. Tukio hilo lililoshuhudiwa ‘live’ na mwandishi wetu lilijiri Jumapili iliyopita kwenye nyumba waliyopanga wanandoa hao katika Mtaa wa Magurumbasi Kata ya Mbuyuni mkoani hapa.

 

Katika tukio hilo, mume na ndugu zake walitaka kumshushia kichapo Tausi wakimshutumu kuuza baadhi ya vitu ikiwemo cherehani na televisheni, jambo ambalo liliwakera majirani ambao waliingilia kati na kusababisha timbwili lililofunga mtaa.

 

Mwanaume huyo na ndugu zake walifikia uamuzi wa kumnyang’anya mwanamke huyo kila kitu baada ya mwanaume kupata ajali ya baiskeli iliyosababisha augue kwa muda na hadi sasa hajapona.Ilielezwa kwamba, baada ya Ally kupata ajali, alichukuliwa na ndugu zake na kumuacha Tausi akiishi peke yake zaidi ya miezi mitatu huku wakimzuia kwenda kumuuguza mumewe.

Ilisemekana kwamba, zoezi la kumnyang’anya vitu mwanamke huyo lilisimamiwa na mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Salum Shomari, mmiliki wa nyumba hiyo, Omar Kibwana na baadhi ya majirani ambao ni wapangaji wenzao. Baada ya zoezi hilo kukamilika, mwandishi wetu alifanikiwa kuzungumza na wahusika wote ambapo alikuwa na haya kusema juu ya timbwili hilo:

HUYU HAPA MKE

“Mimi ni yatima, nilikuwa ninaishi Dar nikifanya biashara zangu ndogondogo. Mwaka jana, mwezi wa nane alikuja Ally kunichumbia ambapo mwezi uliofuata, yaani wa tisa tulifunga ndoa nyumbani kwa mama yake mdogo, SUA (Morogoro).

 

“Tumekaa kwenye ndoa miezi mitano tu, wakati mume wangu anatoka kazini, akiwa na usafiri wake wa baiskeli, alipata ajali, akaumia sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani.

“Tulimpeleka hospitalini, nikawa ninamuuguza kwa upendo mkubwa na alipopata nafuu, aliruhusiwa, cha ajabu baada ya kuja hapa nyumbani, ndugu zake walikuja kumchukua na kupeleka SUA kwa mama yake mdogo.

 

“Nikasema siyo tatizo, nikawa ninakwenda kumuona huko. Cha ajabu, siku moja nilikwenda na wembe kwa lengo la kumnyoa ndefu na kumkata kucha, lakini walinizuia huku wakinitolea maneno makali.

 

“Mimi sina ndugu wala mtu ninayemjua hapa Morogoro, wala biashara yoyote, sina ndugu wala pesa ya kula. Kuna dada mmoja anaitwa Farham lbraham ambaye ni Mtangazaji na Somo wa Kipindi cha Mcharuko wa Pwani cha Radio Planet FM, siku zote amekuwa akinipa chakula cha mchana na jioni huku akinipa muongozo wa mawazo na kunitaka kuwa mvumilivu wakati huu mgumu.

 

“Nilijiongeza nikaenda kwa Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Abood, nikamuelezea matatizo yangu na kumuomba anitafutie kazi ili nipate pesa za kujikimu.

 

“Kweli alinipeleka kiwanda cha nguo, zamani kilijulikana kama Polister, nikapewa mkataba ambapo kwa sasa ninaendelea na kazi.

 

“Baada ya sintofahamu ya mimi kuzuiwa kumuona mume wangu, ndugu zake walinipigia simu, wakaniambia wanataka kuja nyumbani. Nikawaambia waje ndipo wakaja, wakasema wanataka kuchukua vitu na mimi twende kuishi kijijini.

“Nikawaambia siwezi kwenda kijijini maana kazini itakuwaje? Hao ndugu walikataa na mimi siwezi kuacha kazi. Wakasema basi wanachukua vitu, nikawaruhusu, cha ajabu wanadai TV, cherehani na nguo za mume wangu hakuna, wakadai mimi ni mwizi, wakataka kunipiga ndipo wapangaji wenzangu wakanitetea.”

 

MSIKIE MUME

“Nimepata ajali, siwezi hata kwenda kazini hivyo pesa ya kodi ya nyumba sina, kule kijijini kuna nyumba na mama yangu yuko kule, kodi ya nyumba mkataba unakwisha mwezi huu (wa nne) hivyo nimeamua kuja kumchukua mke wangu na vyombo, twende kijijini, lakini amekataa,” alisema Ally na kuangua kilio huku akiondoka na kumwacha mkewe huyo.

Kwa upande wake, mmiliki wa nyumba, Mzee Kibwana alikuwa na haya kusema juu ya sakata hilo:“Yaani huyu mwanaume anaacha mwanamke bora kabisa kwa zama hizi, mwanamke ana hofu ya Mungu. Kwa kipindi chote alichoishi hapa peke yake hajawahi kuingia na mwanaume wala kurudi usiku.

 

“Kabla hajapata kazi, alikuwa akishinda na njaa, mimi naona huruma, ninampa pesa. Hii ina maana hana mwanaume nje.

 

”Naye mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Salum Shomari alithibitisha kutokea kwa tafrani hiyo kwenye mtaa wake.

Stori: Dunstan Shekidele, Morogoro.

Comments are closed.