The House of Favourite Newspapers

Mkude ampongeza kocha Yanga

KIUNGO mkabaji wa Simba, Jonas Mkude, ameshindwa kujizuia na kujikuta akimpatia tano (kumpongeza) Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera.

Unajua ni kwa nini? Ni kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kumbadilisha mshambuliaji wa timu hiyo, Ibrahim Ajibu na kuwa mmoja wa wachezaji wa kutumainiwa katika kikosi cha timu hiyo msimu huu.

Mpaka sasa, Ajibu anaongoza kwa kutengeneza nafasi za kufunga (asisti) ndani ya Yanga, lakini pia kwa wachezaji wote wa ligi kuu msimu huu ambapo katika mabao 14 ambayo mpaka sasa Yanga imefunga, yeye ametoa asisti nane na kufunga mabao matatu, hivyo hajahusika katika mabao matatu tu.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkude alisema kuwa juhudi za Zahera ndiyo zimemfanya Ajibu leo hii kuwa katika kiwango hicho ambacho kimemwezesha kuwa mchezaji anayeongoza kwa kupiga asistI nyingi kuliko wote ligi kuu.

“Kusema kweli bila ya Zahera, naamini Ajibu asingekuwa tishio hivi sasa katika michuano ya ligi kuu, nasema hivyo kwa sababu sisi wachezaji tunajuana vilivyo na huwa tunazungumza tunapokutana.
“Kila wakati huwa napata taarifa kuhusiana na Zahera jinsi anavyopambana na Ajibu ili kuhakikisha anakuwa fiti, na hiyo ni kwa sababu tayari ameshamjua rafiki yangu huyo jinsi alivyo, kwa hiyo anataka awe bora zaidi, nampongeza sana kwa hilo.

“Lakini pia nimwombe Ajibu aendelee kupambana na kuzingatia ‘madini’ yote anayopata kutoka kwa Zahera kama anataka mafanikio msimu huu,” alisema Mkude ambaye ni mmoja kati ya viungo mahiri wa Simba.

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam

Comments are closed.