The House of Favourite Newspapers

Mkuki Moyoni Mwangu – 47

0

ILIPOISHIA…

CATARINA hajafa! Ulimwengu unachofahamu ni kwamba binti huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha, aliyefanya mchezo huo ni tajiri Jackson Motown, ambaye alimbaka wakiwa ndani ya ndege mpaka kupoteza fahamu na kuaminika kwamba alikufa, Motown akafanya mpango na wakala wa Catarina Mario Pizaro ili Catarina azikwe ndani ya Uwanja wa JF Kennedy maana hapakuwa na namna yoyote ya kuutoa mwili wake hadi nje ya uwanja bila kugundulika.

Vijana waliopewa kazi ya kuuzika mwili wa Catarina ndiyo waliogundua kwamba kumbe hakuwa amekufa, kwa huruma wakaamua kumwondoa uwanjani kwenda kumficha nyumbani kwa mmoja wao ambako walimtafutia matibabu mpaka akapata nafuu ndipo wakaamua kutoa taarifa kwa FBI, muda mfupi baadaye vijana wote hao waliuawa kifo cha aina moja.

Kwa maelezo waliyopewa FBI waliamua kumtafuta Jackson Motown, juhudi zao kumpata nyumbani kwake Miami hazikuzaa matunda, mfanyakazi wa nyumbani kwake ndiye aliyewapatia namba ya mlinzi wa Motown aitwaye Dragon, waliporejea New York waliingiza namba hiyo kwenye mtambo maalum uitwao GPS Tracer ambao hutumika kuonyesha mahali simu ilipo.

Mtambo huo ukaonyesha Dragon akiwa nje ya Mji wa Miami, katika eneo la mashamba liitwalo Opa Locka, wote wakaamini lazima alikuwa amejificha huko akiwa na Jackson Motown kukimbia mkono wa sheria, uamuzi walioufikia ukawa ni kurejea Miami na baadaye kwenda hadi Opa Locka.

Je, watafanikiwa kuwakamata Jackson Motown na Dragon? Je, Kevin yuko wapi? Ameuawa na kuzikwa? SONGA NAYO…
WALICHOKIFANYA maofisa wa FBI ni kumpigia simu Catarina wakimtaarifu juu ya safari yao kurejea Miami, wakamtaka atulie ndani bila kutoka nje kwa sababu hali haikuwa nzuri, lazima kulikuwa na watu wanamtafuta ili wamuue kupoteza ushahidi.
Walimhakikishia kabisa kuwa mtandao wa Jackson Motown haukuwa mdogo, hata wao wenyewe uliwahangaisha kwani alikuwa na wakala kila mahali hata ndani ya FBI ambao wangeweza kumpa taarifa ya kilichokuwa kikiendelea, Catarina akaingiwa na hofu kubwa.
“Nitafanya hivyo, sitatoka kabisa!”
“Hao maofisa tuliowaweka hapo hotelini watakulinda usiku na mchana!”
“Hawawezi kununuliwa?”
“Hawawezi, tunawaamini.”
“Basi niwatakie kazi njema, kumbukeni pia kumtafuta Kevin, nina wasiwasi kabisa walimteka na kumuua, bila shaka hivi tunavyoongea anaoza ardhini, Mungu wangu! Kevin wangu! Naomba tu mawazo yangu yasiwe sahihi!”
“Tutahakikisha anapatikana, acha twende huko Opa Locka kwanza, tukishamtia nguvuni Dragon, bila shaka tutapata mwanga wa kilichopo mbele hasa wapi aliko Motown na hata Kevin!”
“Nitashukuru sana.”
“Basi tutawasiliana, tutakupigia simu mara kwa mara kufahamu kinachoendelea!”
“Ahsanteni!”
Simu ilipokatika Catarina alipiga simu Tanzania kuwajulisha wazazi wake juu ya kilichokuwa kikiendelea akiwataka pia wamwombee, siku hiyo pia aliongea na wazazi wa Kevin na kuwaondolea wasiwasi waliokuwa nao, hakutaka kuwatisha, badala yake aliongea uongo akidai alishawasiliana na Kevin na siku si nyingi mambo yakitulia wangeungana.
“Tunakupenda Catarina, wewe na mtoto wetu mtatuzalia wajukuu wazuri!”
“Ahsante mama!”
***
Ndege ndogo ya FBI aina ya Cessna 172 ilitua Uwanja wa Ndege wa Miami na maofisa wanne wakiongozwa na Derrick Fisherman, mzoefu wa kupambana na wahalifu tegemeo la FBI wakashuka na kuingia ndani ya magari mawili aina ya Ford ya rangi nyeusi, ndani yake yakiwa yana silaha zote muhimu, yaliandaliwa na Jeshi la Polisi Tawi la Miami ambao walishapewa taarifa na kutakiwa kusaidiana na FBI.
Safari kueleka Opa Locka ikaanza na kuchukua muda wa saa sita ndipo wakaingia kwenye eneo hilo la mashamba, mtambo wa GPS Tracer ukiwaongoza kuelekea mahali ilipokuwa namba ya simu ya Dragon, maneno kama “Go straight five kilometers, turn left, drive one hundred kilometers then turn right…” yaliyomaanisha nyoosha moja kwa moja kilometa tano, kata kushoto, kisha endesha kilometa mia moja halafu kata kulia…yalisikika na dereva alifuata maelekezo hatimaye walipofika maeneo ambapo simu ya Dragon ilikuwa, GPS Tracer ikaanza kupiga kelele kuashiria huo ndiyo ulikuwa mwisho wa safari yao.
Mbele yao kulikuwa na nyumba kubwa iliyojengwa kwa mbao, magari ya kifahari yakiwa yameegeshwa kwenye maegesho yake na pia kulikuwa na Helikopta kando kwenye uwanja ulioonekana wa ndege, wote wakashuka wakiwa na silaha zao na kuizunguka nyumba hiyo wakifuata maelekezo ya Derrick Fisherman.
Wawili kati yao waliusogelea mlango na kuusukuma, wakagundua ulikuwa wazi, wote isipokuwa wawili wakavamia ndani, hawakuamini walichokishuhudia, watu wanne walikuwa wamelala sakafuni wakiwa wameunguzwa vibaya nyuso zao na sehemu kubwa ya miili.
“Hands up! Hands up!”(Mikono juu! Mikono juu!) aliamrisha Derrick Fisherman lakini watu hao hawakunyanyua mikono yao kama alivyotaka, walionekana wasio na nguvu miilini mwao.
“You are under arrest!”(Mko chini ya ulinzi!) askari mwingine alitoa sauti hiyo huku wote wakifungwa pingu mikononi.
Haikuwa rahisi kuwatambua kwa jinsi nyuso zao zilivyoharibiwa na walionekana kuwa katika maumivu makali kupindukia, wakawanyanyua na kuwasimamisha kisha kuanza kusukumwa kuelekea nje kwa taabu, huko walijaribu kuwatambua lakini haikuwezekana.
“We are FBI officers, can we know your names? What is your name?” (Sisi ni Maofisa wa FBI, tunaweza kufahamu majina yenu? Wewe ni nani?) aliongea Derrick na kumuuliza aliyekuwa jirani yake.
“My name is Jackson Motown!”(naitwa Jackson Motown!)
“And you?”(Na wewe?)
“They call me Dragon!”(Wananiita Dragon!)
“Tell us your really name!”(Tuambie jina lako halisi!)
“Malcom Timberlake!”
“You?”(Wewe?)
“Patrick Antony!”
“The last one?”(Wa mwisho?)
“Henrico Peninye!”
Hapakuwa na mtu mwenye jina la Kevin na maofisa wa FBI hawakuelewa ni kitu gani hasa kiliwakuta mpaka wakawa kwenye hali hiyo, wakafikia uamuzi wa kuwapakia kwenye gari tayari kuelekea Miami ambako wangepanda ndege na kuruka hadi New York, vichwani mwao walikuwa wakijiuliza ni wapi alikokuwa Kevin.

Je, nini kitaendelea? Nini kiliwapata? Kevin yuko wapi? Ameuawa na kuzikwa? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika Gazeti la Championi Jumatatu.

Leave A Reply