MKURUGENZI wa kampuni ya VKP Investment For Youth, David Manot, mwanasheria wa kampuni hiyo, Ernest Ngonyani na wenzao wanne wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 31 ya kujipatia zaidi ya sh. milioni 300 kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja la kula njama.
Washtakiwa wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni, mfanyabiashara, Yona Kiita, Mkurugenzi wa Masoko, Jane Isack; Ofisa Masoko, Modikai Kilala na Meneja Uendeshaji, Juliana Kasambala.
Akiwasomea mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando, wakili wa serikali, Ester Martin, alisema kati ya Januari 2016 na Desemba 2018 katika jengo la Mwalimu House lililopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu washtakiwa wote hao wanadaiwa kati ya Novemba 21, 2017 na Aprili mahali hapo, kwa nia ya kutenda kosa walijipatia fedha kupitia kampuni hiyo ya VKP Investment For Youth kutoka kwa Anna Kavishe kwa kujifanya kuwa wangemuuzia kiwanja huku wakijua kuwa siyo kweli.
Washtakiwa hao wanadaiwa kupata kiasi tofauti-tofauti cha pesa kutoka kwa Joel Olinda, Mlolu Chelehani, Shukuru Olomi, Emmanuel Mlambity, Agnes Joseph, Christopher Mraha, Prowin Mtei, Mustapha Ngahyoma, Chausiku Kinyehe, Issa Illy, Samson Ngahyoma, Asha Mtangaza, Prisca Mrope Dotto Pangimoto, Nice Mohammed, Elizabeth Makombe, Elirehema Mangore na baadhi ya wengine.
Watuhumiwa kwa pamoja wamekana kutenda makosa hayo na wamerudishwa rumande hadi Januari 11 mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutolewa maamuzi juu ya dhamana ya washtakiwa.
Comments are closed.