The House of Favourite Newspapers

Makonda Amwonya Mjenzi Mradi wa Wilaya ya Kigamboni -Video

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa pili kulia) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, kwenye ukaguzi wa ujenzi wa majengo ya wilaya mpya ya Kigamboni leo.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa hospitali na jengo la wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam na kumtaka mkandarasi kumalizia ujenzi huo hadi mwezi wa sita mwaka huu ili wananchi waweze kunufaika na huduma za wilaya hiyo kwa urahisi.

Jengo la Manispaa ya Kigamboni likiwa linaendelea kujengwa.

Akizungumza na Global Publishers, Makonda alisema kuwa hakuna ulazima wa manispaa ya Kigamboni kulipia majengo wanayoyatumia kwa sasa  kwa kuwa pesa zilishatolewa na serikali ili kukamilisha mradi huo.

Makonda na ujumbe wake wakiendelea kukagua miradi mbalimbali.

“Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanapata huduma na ametoa pesa kwa ajili ya mradi huu lakini  mkandarasi anasuasua kuukamilisha na aliomba muda ambao alipewa hadi mwezi wa kwanza mwaka huu lakini hadi sasa bado hajakamilisha,” alisema Makonda akisisitiza kwamba amempa makandarasi huyo hadi mwezi wa sita kukamilisha kazi hiyo kwa vile wananchi wanapata huduma kutoka mbali.

Ukaguzi ukiendelea katika jengo la hospitali (haliko pichani).

Alisistiza kwamba kama mkandarasi hajamaliza mradi huo kwa muda aliopewa itambidi alipie kodi na gharama za jengo linalotumika sasa  na kunyang’anywa tenda ambapo atapewa mtu mwingine.

 

Taswira nyingine ya ujenzi wa jengo la Manispaa.

Naye mratibu wa miradi ya Wakala wa Majengo (TBA) Mkoa wa Dar, Wilson Tesha,  alisema kuwa atahakikisha siku ambayo wamepewa na Mkuu wa Mkoa kumalizia mradi huo inatekelezwa.

“Tutahakikisha mwezi wa sita tunakamilisha majengo haya kwa kuwa sehemu iliyobakia ni ndogo na tupo kwenye hatua ya mwisho ya kumalizia kwa hiyo changamoto hiyo tamalizika,” alimalizia.

Makonda akizungumza jambo kuhusu upatikanaji wa matofali.

Stori: Neema Adrian

Comments are closed.