The House of Favourite Newspapers

MLINGA AHOJI ‘BIBI’ KUVAA WIGI KWENYE NEMBO YA TAIFA

MBUNGE wa Ulanga, mkoani Morogoro (CCM), Goodluck Mlinga ameiomba Serikali ipige marufuku matumizi ya Nembo ya Taifa yenye picha ya mwanamke na mwanamume ‘Bibi na Bwana’ akidai kwamba mwanamke huyo amevaa wigi, hivyo haiakisi maisha ya halisi na desturi za Mtanzania.

 

Mlinga amesema hayo leo Bungeni Mjini Dodoma, baada ya kuomba mwongozo wa Spika kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge na kudai katika nembo hiyo kuna bwana anaonekana akiwa amevaa lubega ambaye anaakisi maisha ya halisi ya Mtanzania.

 

“Bibi aliyevaa wigi haendani na uhalisia wa Mtanzania, haakisi maisha halisi ya Mtanzania, haijulikani kama ni Mwarabu au Mzungu, ninaiomba Serikali isitishe matumizi ya nembo hiyo, izuie isitumike hadi pale itakapofanyiwa marekebisho?” alisema Mlinga.

 

Akijibu mwongozo huo Mwenyekiti, Andrew Chenge alihoji endapo tukio hilo limetokea leo hadi Mbunge huyo akafikia hatua ya kuhoji. “Narudi kwenye kanuni je, suala hili limetokea leo na kama halijatokea leo halipo kwenye kanuni. Wabunge mnatakiwa kuheshimu sheria inayosimamia nembo,” alisema Chenge.

Comments are closed.