The House of Favourite Newspapers

MMILIKI WA CHELSEA ACHUKUA URAIA WA ISRAEL

Roman Abramovich

BILLIONEA wa Urusi, Roman Abramovich, anayemiliki klabu ya soka ya Chelsea ya Uingereza, ambaye amejikuta hana visa ya kuingilia nchini humo, juzi (Jumatatu) alichukua uraia wa Israel ambako amenunua mali kadhaa, habari kutoka Israel zimesema.

Abramovich, mmoja wa matajiri wakubwa zaidi nchini Uingereza tangu alipoinunua klabu hiyo iliyoko kwenye Ligi Kuu ya Uingereza mwaka 2003, visa yake ilimalizika mwezi uliopita na kwa kawaida, itachukua muda mrefu kupata nyingine.  Serikali ya Uingereza bado haijasema lolote kuhusu suala hilo.

Tovuti ya Ynet inayomilikiwa na gazeti kubwa zaidi nchini Israel la  Yedioth Aharonoth, imesema   Abramovich ambaye ni Myahudi, alitua jijini Tel Aviv jana na kupewa hati kuthibitisha ni raia wa Israel.

Msemaji wa wizara ya utoaji uraia ya Israel alikataa kusema lolote juu ya jambo hilo akisema ni la kibinafsi, lakini msemaji wa idara ya masuala ya utawala inayoshughulikia uhamiaji, alithibitisha Abramovich alikuwa nchini humo.

Israel hutoa uraia kwa Myahudi yeyote anayetaka kuhamia humo na pasipoti inaweza kutolewa mara moja.  Raia wa Israel anaweza kuingia Uingereza bila visa ikiwa atakaa huko kwa muda mfupi, japokuwa nahitajika kuwa na visa ili afanye kazi nchini humo.

Uhusiano kati ya Urusi na Uingereza umelegalega baada ya kulishwa sumu kwa jasusi wa zamani wa Urusi, Sergei Skripal aliyeko Uingereza mwezi Machi, jambo ambalo Uingereza imeilaumu serikali ya Urusi.

Abramovich kila mara amekuwa akiitembelea Israel ambako amenunua mali ambayo ilikuwa ni hoteli jijini Tel Aviv kwenye pwani ya bahari ya Mediterranea.

 

Comments are closed.