The House of Favourite Newspapers

Mo Dewji Amgeukia Gadiel Michael

Gadiel Michael.

SIMBA wameshaanza kukisuka kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao na sasa wanachofanya ni kuwapa mikataba ya awali nyota wote ambao wanawataka.

 

Tetesi kuwa tayari wameshawapa mikataba Ibrahim Ajibu wa Yanga na straika matata Jacques Tuyisenge wa Gor Mahia zimeshasambaa, sasa kuna nyingine mpya.

 

Imedaiwa kuwa Simba wapo kwenye mikakati mizito ya kuhakikisha wanamnasa beki wa kushoto wa Yanga, Gadiel Michael.

 

Usajili huo wa beki huyo ambaye pia huanza katika timu ya taifa, Taifa Stars unatarajiwa kufanyika kutokana na pendekezo la Kocha wa Simba, Patrick Aussems raia wa Ubelgiji.

 

Simba wanamtaka beki huyo ili kuongeza nguvu upande wa kushoto wa timu hiyo ambao sasa unachezwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Asante Kwasi ambaye huenda akapigwa panga katika usajili wa msimu ujao. Chanzo kutoka Simba kimelieleza Championi Ijumaa, kuwa hadi sasa kuna mazungumzo na mwakilishi wa beki huyo kwa ajili ya msimu ujao.

 

“Huu usajili wa Gadiel ni pendekezo maalum la kocha ambaye yeye mwenyewe ndiye ametaka aletewe beki huyo baada ya kuridhishwa naye. “Kinachofanyika sasa ni kuzungumza naye taratibu ikisubiriwa amalize mkataba wake kisha ndiyo atapewa mkataba.

 

Siyo yeye tu kuna watu wengine ambao watachukuliwa katika usajili huo ujao,” kilisema chanzo hicho. Mbali na Gadiel mchezaji mwingine wa Yanga ambaye anawaniwa na

 

Simba ni kipa Beno Kakolanya ambaye hana uhusiano mzuri na kocha wa sasa wa Yanga, Mwinyi Zahera ambaye hivi karibuni aliweka wazi kuwa hatakuwa na muda wa kumbembeleza mchezaji yeyote ambaye atataka kuondoka klabuni hapo kwa kuwa ana mpango wa kushusha vifaa vya maana kwa ajili ya msimu ujao.

 

Mratibu wa Klabu ya Simba, Abbas Ally alipoulizwa juu ya suala hilo, alisema: “Sifahamu chochote lakini kama suala hilo lipo litajulikana, huu siyo muda wake.” Ikumbukwe kuwa mkataba wa miaka miwili wa Gadiel aliyesajiliwa akitokea Azam FC unaelekea ukingoni na utamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Sweetbert Lukonge na Said ally, Dar

Comments are closed.