The House of Favourite Newspapers

Mo Dewji Asimulia Mateso ya Kutekwa

 

BAADA ya kupita mwaka mmoja tangu mfanyabiashara bilionea Afrika na muwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ kutekwa, kwa mara kwanza amesimulia mateso ya siku tisa aliyoyapata wakati wa sakata hilo.

 

Mo alikumbana na kadhia hiyo Oktoba, mwaka jana alipotekwa na watu wasiojulikana nje ya Hoteli ya Collessum kwa muda wa siku tisa mfululizo kabla ya kuachiwa kwake.

 

Bosi huyo amesimulia tukio hilo kupitia mahojiano yake na Kituo cha BBC kwa kusema: “Nilipoegesha gari langu pale hotelini sehemu ambayo huwa nimetengewa na walinzi wa pale karibu na mlango wa kuingia gym.

“Zilitumika sekunde 60 tu, watu wanne wakiwa wamezipa nyuso zao walinichukua baada ya kupiga risasi hewani.

“Awali nilijua wanataka gari langu lakini baadaye wakanichukua na kuniingiza kwenye gari safari ikaanza, nilifungwa macho, wakanivua nguo zote wakijua labda nina kifaa maalum cha kufuatiliwa.

 

“Walinifikisha kwenye chumba kilichokuwa na godoro moja, humo ndimo nilimokuwa naishi. Hawakuwa wakitumia lugha za Tanzania.

“Walinipa chakula lakini nilikuwa nashindwa kula, kwa sababu ya hofu, usiku walinifunga mikono kwa nyuma, asubuhi walinifunga kwa mbele.

 

“Nilitumia muda mwingi kumuomba Mungu, nilijua maisha yangu yataishia pale, kila nilipofikiria familia yangu nilikuwa nalia.

“Siku waliyonirudisha walinibeba, kufika eneo waliloniacha wakanisukuma wao wakaondoka, nilivyofungua kitambaa usoni ndipo nikagundua nipo maeneo ya Gymkhana.

 

“Nikaanza kukimbia kulekea Southern Sun nikapita njia ya European Union. Nilipofika wale watu wa hoteli hiyo wakanipokea vizuri kisha wao ndiyo wakatoa taarifa kwa baba yangu.

 

“Baba na mdogo wangu walipofika hawakumiani, walisujudu kumshukuru Mungu, ndipo nikaondoka nao nikafika nyumbani kuungana na familia,” alisema Mo.

STORI NA Ibrahim Mussa, Dar es Salaam

Comments are closed.