The House of Favourite Newspapers

Mo Dewji: Bado Nipo Simba, Amtaja Waziri Mwakyembe

SIKU chache baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe kuzitaka klabu kuwa na wawekezaji zaidi ya mmoja, Mwekezaji wa klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ amesema ataendelea kuwepo ndani ya klabu hiyo kwani mabadiliko hayo wanayafahamu tangu mwaka juzi, 2017.

 

Dk Mwakyembe alisema kwamba klabu ambazo zinabadilisha mifumo kutoka wanachama kwenda mfumo wa hisa ni lazima wawekezaji watakaomiliki hisa asilimia 49 waanzie watatu na sio mmoja kama ilivyo Simba.

 

Kauli hiyo ilizua sintofahamu kwa wadau wa soka nchini kwani tayari Simba ilianza mchakato huo na unaelekea kukamilika ambapo leo Jumamosi Mo Dewji amewatoa shaka Wanasimba juu ya uwepo wake ndani ya Simba.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Mo Dewji ameandika hivi; “Nimesikitishwa na mijadala mitandaoni ya kumshutumu Waziri Mwakyembe kwamba ameanzisha utaratibu mpya wa mwekezaji kuwa na 49% na wanachama 51% ya hisa. Ndugu zangu, si kweli. utaratibu huu upo tangu 2017 kisheria na sisi Simba tulikubali.

 

“Waziri Mwakyembe alituruhusu Simba tuendelee na mwekezaji mmoja. Ndugu Wanasimba mimi nipo na niko na nyinyi, siendi popote. Na sasa tumeishazungumza na serikali na mazungumzo ni mazuri. Nawasihi Wanasimba wote twendeni tukaishangilie timu ya Taifa na tukutane Simba Day tarehe 6. Tulianza vizuri na serikali na tutamaliza vizuri na Serikali,”

Mo Dewji ni mwekezaji pekee aliyeshinda tenda ya uwekezaji baada ya kutojitokeza mwekezaji mwingine huku akiweka Sh 20 bilioni. Mo Dewji pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba baada ya kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu.

Comments are closed.