The House of Favourite Newspapers

Mondi Ajirudi Kwa Kiba, Harmo

AMEONESHA uungwana! Hiyo ndiyo kauli ambayo imezungumzwa zaidi wikiendi iliyopita mara baada ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kufanya tukio lililoashiria kwamba, moyoni mwake hana kinyongo cha aina yoyote na mastaa ambao mashabiki wanaamini ana bifu nao, Gazeti la Ijumaa Wikienda linakupa habari kamili.

 

NI WIKIENDI ILIYOPITA

Diamond au Mondi alifanya tukio hilo la kiungwana wikiendi iliyopita ambapo alitamka kwamba hana kinyongo kabisa na wasanii; Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ na Richard Martin ‘Rich Mavoko’ ambao watu wengi wanaamini picha haziivi. Mondi alifunguka hayo ‘live’ kupitia ukurasa wake wa Instagram, baada ya kuripoti matangazo hayo akiwa moja kwa moja kwenye Studio za Wasafi TV zilizopo Mbezi-Beach jijini Dar.

MAMBO YALIKUWA HIVI…

Kupitia kipengele cha Insta Live kilichopo ndani ya Mtandao wa Kijamii wa Instagram, Mondi alitangaza kuwa anapokea maombi mbalimbali ya nyimbo ambazo watu wanataka zichezwe moja kwa moja kupitia Wasafi TV.

 

MAOMBI KAMA YOTE

Watu kutoka ndani na nje ya nchi walianza kuomba nyimbo zao wanazopenda zionekane live kwenye Wasafi TV, lakini cha kushangaza, maombi yaliyotawala wakati huo, yalikuwa ni ya wale mahasimu wa Mondi ambayo wengi waliamini isingekuwa rahisi kuyasoma wala kucheza nyimbo zao.

 

AONESHA UUNGWANA

Tofauti na matarajio ya wengi kwamba ni kwa muda mrefu nyimbo za Harmonize au Harmo, Mavoko na Kiba zilikuwa hazijawahi kupigwa kwenye runinga hiyo, mkali huyo anayetamba na Wimbo wa Yope alioufanya na Innoss’B wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alisema kwamba atawachezea nyimbo hizo.

 

FULU MBWEMBWE

Kwanza, alianza kusoma yale maombi moja kwa moja kwa kuwataja wale waliokuwa wanaomba zile nyimbo huku akisoma kwa bashasha zote majina ya mahasimu wake hao ambao inaaminika ilikuwa ni vigumu hata kutaja tu majina yao hewani.

“Hii ni televisheni yenu, nitazicheza hizo nyimbo zote mlizoomba, naona hapa kuna mtu anaomba Wimbo wa Uno wa Harmonize Harmo Nenga, lakini namuona mwingine hapa anaomba Wimbo wa Kiba, namuona mwingine pia ameomba wimbo wa Kokoro wa Rich Mavoko,” alisema Mondi.

AJITETEA KIDOGO KWA HARMO…

Licha ya Mondi kujinasibu kwamba televisheni hiyo ni ya watu wote, aliwaomba radhi mashabiki wake kwamba hataweza kucheza wimbo mpya wa Harmonize unaotikisa kwa sasa wa Uno kutokana na kutokuwa na video na badala yake alisema atacheza wimbo mwingine wa jamaa huyo wa Shulala.

Pamoja na wimbo huo, Mondi alicheza nyimbo za mahasimu wote akiwemo Kiba na Mavoko na Hamisa Mobeto ambaye iliaminika kuwa haziivi baada ya kufikishana mahakamani kwa ishu za mtoto aliyezaa naye, Dyllan.

MAONI YA WANANZENGO SASA

Wadau mbalimbali walikomenti kwenye ukurasa wa Instagram huku wengine wakizungumza moja kwa moja na Gazeti la Ijumaa Wikienda wakionesha ni jinsi gani mkali huyo amejirudi kwa mahasimu wake hao.

“Mh! Jamani huyu si alikuwa hachezi hizi nyimbo za Harmonize? Imekuwaje leo? Nafikiri ameamua tu kujirudi ili kujisafisha asionekane mbaya mbele ya jamii kwa sababu kwa muda mrefu tulikuwa tukipiga kelele humu Insta,” aliandika shabiki aliyejiita Keleno.

WADAU WANENA…

Gazeti la Ijumaa Wikienda lilizungumza na wadau mbalimbali ndani ya Jiji la Dar kuhusu mtazamo wao na mambo yalikuwa kama hivi; “Ameamua kushuka ili kupata huruma ya mashabiki maana tayari watu wengi wameshamuona hana maana kwa sasa,” alisema John Njao wa Kinondoni.

“Ni mwendelezo wa kutafuta huruma, unajua watu walishajenga chuki dhidi yake maana ana kituo cha televisheni, lakini alikuwa na utabaka sana katika kucheza nyimbo zake hivyo hata watu walianza kuichukia televisheni yake,” alisema Mahimbo Kileo, mkazi wa Tandika.

Maoni mengi ambayo yalikusanywa na gazeti hili kupitia kwenye ‘peji’ za mitandao ya kijamii mbalimbali za gazeti hili, yalisema Mondi amefanya hivyo baada ya Harmonize kufanya mahojiano na Clouds FM na kuongea maneno ya kiungwana yaliyoonesha kukerwa na suala la vyombo vya habari kubagua wasanii.

NUKUU YA HARMO

Kwenye mahojiano hayo, Harmo alinukuliwa akisema; “Moja kati ya mambo makubwa yanayowalostisha wasanii ni mabifu, hususan vyombo vya habari kubagua kazi za wasanii, kucheza za huyu na kutocheza za huyu. Natamani sana vyombo vyote vya habari visapoti kila msanii wa Bongo ili muziki wetu uweze kufika mbali.”

TUJIKUMBUSHE

Rekodi inaonesha, mara kadhaa Mondi amekuwa akijishusha kwa Kiba, lakini hata hivyo kwa upande wa mwenzake huyo imekuwa ni vigumu mno kuonesha hadharani kwamba yupo tayari wakae kwenye mstari wa kushirikiana kama wasanii wa Bongo.

Kwa upande wa Harmo, kabla ya kuruka live hiyo juzi, nyimbo za Harmo zilikuwa hazipigwi kwenye Kituo cha Wasafi hususan baada ya kijana huyo kuachana na Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) na kuanzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide.

Comments are closed.