The House of Favourite Newspapers

Mondi Amelianzisha, Wengine Vipi?

0

 

KATIKA kipindi cha zaidi ya miaka kumi, nimemuona megastaa wa muziki wetu wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ akisaidia jamii ya wenye uhitaji.

Nimemuona Diamond au Mondi akiwashika mkono watu wenye taabu mbalimbali.

 

Nimemuona Mondi akicheka na wanaocheka na kulia na wanaolia! Hapa ndipo mastaa wengi Bongo hii wanapofeli. Wanafeli eneo nyeti la kurudisha kwa jamii ambayo ndiyo walaji wakuu wa bidhaa yao ya muziki.

 

Nimemuona Mondi akipeleka misaada ya vyakula na kula na watoto yatima kwenye vituo vyao wakati wa siku yake ya kuzaliwa (Oktoba 2, kila mwaka).

Nimemuona Mondi akijenga misikiti kwenye mikoa mbalimbali nchini.

 

Nimemuona Mondi akitengeneza mastaa kupitia lebo yake ya muziki ya Wasafi Classic Baby (WCB). Kuanzia kwa Harmonize, Rich Mavoko, Rayvanny, Mbosso, Darleen, Lava Lava na sasa Zuchu. Kupitia yeye na wasanii wake, ametengeneza ajira nyingi na kulipa kodi kwa Serikali kuliko msanii mwingine yeyote Bongo na nadiriki kusema Afrika Mashariki!

 

Nimemuona Mondi akigawa Bima za Afya kwa watu 2,000 pale Tandale.

Nimemuona Mondi akitoa mitaji ya biashara ndogondogo kwa akina mama 200 na bodaboda 20 pale Tandale.

Nimemuona Mondi akijenga visima vya maji na kusomesha watoto ambao wazazi hawana uwezo kabla ya elimu bure ya Rais Dk John Pombe Magufuli.

Nimemuona Mondi akimsaidia mama mmoja mlemavu wa miguu kwa kumnunulia Bajaj ambayo sasa inamuingizia kipato cha kuendeshea maisha na familia yake na kuacha kuombaomba barabarani.

Hayo yote ni cha mtoto, katikati ya janga linaloitafuna dunia la Corona, namuona Mondi akiwalipia kodi za nyumba familia 500.

 

Namuona sasa Mondi akitoa ghorofa la hoteli yake ya kifahari aliyonunua hivi karibuni pale Mikocheni B kwa ajili ya wagonjwa wa Corona!

Nimemuona Mondi akifanya mengi na kumbuka haikuwa lazima kwa yeye kufanya hivyo.

 

Lakini kwa sapoti ambayo amekuwa akipewa na Watanzania, Mondi anawiwa na kuona ni jukumu lake kurudisha kwa jamii yake.

 

Namuona Mondi amelianzisha, najiuliza wako wapi mastaa wengine Bongo wanaojua kutafuta kiki, halafu hawajui kurudisha kwa jamii? Wako wapi akina nanii wanaopenda kutafuta kiki kwa mambo yasiyokuwa na kichwa wala miguu? Kwanini sasa wasitafutie kiki kwenye kusaidia jamii wakati huu wa Corona?

 

Tunawahitaji mastaa wengine wengi kama Mondi na Madee ambaye naye nimemuona akigawa barakoa na sanitaiza pale Manzese.

Wako wapi mastaa ambao wako tayari kutoa nyumba zao kwa Serikali ili zitumike kama karantini au hospitali katika kipindi hiki cha Corona?

 

Wako wapi mastaa ambao wanarudisha fadhila kwa Watanzania ambao hupakua ngoma zao kwa malipo mitandaoni.

Tunahitaji mastaa wengine wanaoweza kusema watalipia gharama za matibabu ya wagonjwa wa Corona pale Amana au kwingine kokote kwenye kituo cha wagonjwa wa Corona.

 

Hatuhitaji mastaa ambao wanawahitaji Watanzania pale wanapokuwa wamekwama wao ndipo wanaomba kuchangiwa pesa za matibabu. Ni somo kubwa ambalo Mondi ametoa kwa mastaa wengine Bongo.

Hii inaitwa kurudisha fadhila kwa jamii yako. Wote tunafahamu historia ya maisha ya Mondi. Mara kadhaa amekuwa akisimulia namna alivyohaso kufika hapo alipo.

 

Mondi ni kijana wa kimaskini ambaye sote tunajua amekulia kwenye shida pale Kitongoji cha Tandale.

Kwa kurudisha kwake kwenye jamii, baraka za Watanzania zimekuwa msaada mkubwa kwake. Kitendo cha kutangaza kuzilipia kodi za miezi mitatu familia 500 za Watanzania, ni kuonesha uungwana wake kwa watu ambao wamekua wakimsapoti kwenye muziki na biashara zake nyingine.

 

Hii siyo tu atapata heshima duniani, bali hata kibali mbinguni. Mondi ametoa funzo kwa mastaa wengine nchini siyo tu wa muziki hata kwenye soka na michezo mingine. Kuna kila sababu na wao kujitafakari na kuona umuhimu wa kurudisha shukrani kwa mashabiki na watu wote ambao wamekuwa wakiwasapoti.

 

Kuna kundi kubwa la watu wenye majina makubwa ambao hawajawahi kukumbuka hata jamii ya mtaani kwao, achilia mbali Watanzania kwa ujumla.

Hawajui bila Watanzania hawa ambao wamewasapoti kwenye muziki, filamu na soka lao wangekuwa si chochote si lolote.

 

Wapo matajiri wakubwa Bongo hii ambao wanapaswa kuiga alichokifanya tajiri Rostam Aziz aliyechangia shilingi bilioni moja, lakini wamekaa kimya na pesa zao. Hawajatoa barakoa wala sanitaiza.

Wapo wabunge ambao wameingia bungeni kwa kura za walalahoi wa Kitanzania, lakini hawajatoa chochote kwa wapiga kura wao hadi sasa.

 

Waone wanamuziki wakubwa, Jay Z na Rihanna pale Marekani, pamoja na kwamba taifa hilo ni tajiri duniani, lakini wametoa Dola za Kimarekani milioni moja (zaidi ya shilingi bilioni 2.3 za Kibongo) kwa ajili ya kusaidia janga la Corona. Hii ni kwa sababu wanajua nini maana ya kurudisha fadhila kwa jamii.

 

Hicho ndicho alichokifanya Mondi, anapaswa kupewa heshima yake na popote ulipo, kwa niaba ya OVER ZE WEEKEND… piga kelele kwa Mondi akeee!

MAKALA: SIFAEL PAUL

Leave A Reply