The House of Favourite Newspapers

Moto umewaka, polisi kuwatumia wasanii kuwataja wauza madawa

0

sacp mihayoMkuu wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa, ACP Mihayo Msikhella.

Richard Bukos na Issa Mnally, UWAZI

DAR ES SALAAM: Kufuatia kauli ya mwanamuziki wa kizazi kipya nchini, David Genzi ‘Young D’ kuwa anawajua wauza madawa ya kulevya ‘unga’ wote na akipata ushirikiano kutoka Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini atawataja wote, tayari mkuu wa kikosi hicho, ACP Mihayo Msikhella ametangaza kumtafuta msanii huyo, Uwazi linakupa zaidi.

young-dee1Young D

Mbali na Young D, pia Kamanda Msikhella amewaita ofisini kwake wasanii wote ambao vyombo vya habari viliwahi kuwaandika juu ya madai ya kutumia unga.

Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka ndani ya kikosi hicho, Kamanda Msikhella amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, wasanii hao wanawajua vizuri wauza unga kwani wengi wao walianza kutumwa kusafirisha (punda) madawa hayo kabla ya kuanza kutumia na kuwaathiri.

KUHUSU YOUNG D

Hivi karibuni, Young D alijitokeza kwenye vyombo mbalimbali vya habari na kukiri kwamba alikuwa mtumiaji wa unga, jambo ambalo kwa sasa analijutia.

Mwanamuziki huyo alikwenda mbele zaidi kwa kusema yupo tayari kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kitengo hicho ili kuwataja watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu duniani kote.

APATA NAMBA YA YOUNG D

“Huwezi amini, kamanda Msikhella aliposikia tu habari za Young D akaamua kumsaka. Alitafuta namba yake ya simu siku ya Jumapili, akaipata na kumpigia lakini simu yake ilikuwa haipo hewani. Lakini anaendelea kumsaka,” kilisema chanzo hicho.

chid beenz (1)Chid Benz

WATAKIWA KWENDA NA MAMBO MATATU

Chanzo kiliendelea kusema: “Kamanda anawaita kwenda kwake wakiwa na mambo matatu. Kwanza wakawataje kwa majina waliokuwa wakiwauzia unga. Pili, watatakiwa kuelekeza wanakopatikana watu hao na tatu, waahidi mbele yake kwamba, hawatarudia tena kubwia unga.

WASANII WALIOWAHI KUTAJWA KWA UNGA

Mpaka sasa, wasanii mbalimbali wamekuwa wakitajwa kujihusisha na ubwiaji wa unga, wengine wakifikia hatua ya kukiri wenyewe huku wengi wakiendelea kukanusha.

RAYCRehema Chalamila ‘Ray C’

Miongoni mwa wasanii hao ni Rashid Abdallah Makwiro ‘Chid Benz’ (hivi karibuni alikuwa Sober House, Bagamoyo, Pwani), Isaac Makuto ‘Lord Eyez’ (pia anadaiwa kumfundisha Rehema Chalamila ‘Ray C’ kutumia unga) na msanii mwanzilishi wa kundi la zamani la muziki wa Hip Hop nchini la Hard Blaster Crew ‘HBC’, Terry Msiaga ‘Fanani’ ambaye Juni 19, mwaka huu na yeye alipelekwa Sober House kwa ajili ya uangalizi maalum baada ya kuathirika na unga.

Wengine ni Ray C (yupo Sober House baada ya dozi ya Hospitali ya Mwananyamala kushindikana), David Jacob ‘Daz Baba’ (hakuna taarifa zaidi), Aboubakar Katwila ‘Q-Chillah’ (ameacha) na wengine wengi.

QCHILA8Q- Chillah

KAMANDA MSIKHELLA HUYU HAPA

Baada ya kuyasikia hayo, juzi Uwazi lilifanya juhudi za kumtafuta Kamanda Msikhella ili kumuuliza kuhusu kuwepo kwa madai hayo.

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda Msikhella alikiri kumtafuta au kumwita Young D ofisini kwake kwa vile amesikia ameamua kulisaidia jeshi la polisi kupambana na wauza unga.

“Huyo mwanamuziki (Young D) namtafuta, nikimpata nitakaa naye sehemu tulivu ili anieleze hao watu ambao walikuwa wakimuuzia hayo madawa tuwashughulikie haraka sana,” alisema kamanda huyo.

Aliendelea kusema kuwa, kwa sasa ameuwasha moto  wa kupambana na biashara hiyo na hautazimika, akaongeza kuwataka mastaa wote wanaojihusisha na utumiaji wa unga kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kutokomeza biashara hiyo.

“Tutawashughulikia wauzaji wote. Nawataka wanamuziki na wasanii wengine kuiga aliyoyafanya Young D, ameamua kulitumikia taifa lake akiwa salama kabisa huku akikemea utumiaji wa unga, wengine wajitokeze,” alisema kamanda huyo.

Kuhusu mwanamuziki Ray C, Fanani na wengine ambao wapo katika vituo vya kupambana na matumizi  ya madawa hayo, Kamanda Msikhella alisema wakipona anawakaribisha katika kazi ya kupambana na madawa ya kulevya.

KAULI YA WAZIRI

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alilitaka jeshi la polisi kutotumia nguvu kubwa katika mambo yasiyokuwa na manufaa kwa wananchi bali nguvu hizo zitumike kupambana na biashara ya madawa ya kulevya kwa maslahi mapana ya taifa.

Waziri Nchemba aliyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya awali ya jeshi la polisi na uhamiaji katika Chuo cha Polisi mkoani Kilimanjaro ambapo zaidi ya wanafunzi 3,000 walihitimu mafunzo hayo.

VIGOGO WANAOSHIKILIWA

Mpaka sasa, vigogo kadhaa wanaotajwa kuwa vinara wa biashara ya madawa ya kulevya ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, wanashikiliwa katika magereza mbalimbali nchini.

Miongoni mwao, wamo Ali Khatib Haji ‘Shkuba’ na Muharami Abdallah Chonji wanaotuhumiwa kwa biashara ya madawa ya kulevya, yanayotajwa kuteketeza nguvu kazi ya taifa, hususan vijana.

Wakati huohuo, muda mfupi kabla gazeti hili halijaenda mitamboni, taarifa kutoka kwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege, Martine Otieno, zilieleza kwamba raia mmoja wa Nigeria (jina halikupatikana mara moja), anashikiliwa na polisi baada ya kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini hapa, akiwa na madawa ya kulevya aina ya heroin, kilo 5.

Leave A Reply