MPENZI WANGU SARAFINA-07

“Nesi….nesi fungua mlango!” alisikika mwanaume mmoja akipiga kelele, saa ilionyesha ni saa saba usiku.

“Kuna nini jamani?”
“Huyu dada! Analalamika tumbo! Nadhani anataka kujifungua,” alisema jamaa huyo aliyekuwa na wenzake wawili.

Sarafina alikuwa akipiga kelele, alilishika tumbo lake, miezi tisa ilikatika na sasa alisikia uchungu wa kutaka kujifungua. Usiku huo alikuwa kwenye wakati mgumu, alikuwa akilia huku akiomba msaada, wanaume hao waliokuwa wakipita njiani ndiyo waliomfuata na kumsaidia.

Walimpeleka katika Hospitali ya Halmashauri ya Tandale, kwa kuwa alitaka kujifungua, wakamchukulia usafiri na kutakiwa kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mwananyamala. Njiani ilikuwa tabu tupu, msichana huyo alikuwa akipiga kelele za kutaka kujifungua.

“Damu! Jamani damu!” alisema jamaa mmoja, tayari aliona damu zikianza kumtoka Sarafina sehemu za siri.

“Kaka ongeza mwendo! Kama kanyaga moto,” alisema mwanaume mmoja.

“Nakufa! Nakufa! Nisaidieni nakufa!” alisema Sarafina huku akisikia maumivu makali chini ya kitovu.

***

“Nesi…nesi…sogeza machela…” alisema jamaa mmoja kwa sauti kubwa iliyowakurupusha manesi waliokuwa nje.

Hawakutaka kupoteza muda, haraka sana wakachukua moja ya machela zilizokuwa nje na kuwasogezea watu wale kisha kumuweka Sarafina na kuanza kuisukuma kuelekea ndani.

Damu hazikukoma, alionekana kuwa kwenye hatua za mwisho kujifungua. Wakampeleka katika chumba cha kujifunguliwa kilichoandikwa Labour mlangoni na kumlaza kitandani.

Ilikuwa ni lazima wafanye haraka sana kwani kama wangechelewa walihofia kuyapoteza maisha ya mama na mtoto. Ndani ya dakika moja tu, tayari walikuwa wakimtoa mtoto kutoka katika mfuko wa uzazi wa Sarafina.

“Sukuma…sukumaaaa…” alisema daktari aliyekuwa ndani ya chumba hicho.

“Naumiaaaaa…siweziiiiii…” alisema Sarafina huku akipiga kelele.

Hawakutaka kukubali, tayari mtoto alianza kuonekana, kitendo cha kukubaliana naye kwamba hawezi kusukuma kulimaanisha kwamba mtoto angekufa na hata yeye maisha yake yangekuwa hatarini.

Wakaanza kumpiga vibao mapajani na mashavuni kwa kumtaka kusukuma zaidi. Alijitahidi, alisukuma kwa nguvu zote, kichwa cha mtoto kikaanza kutoka, hakukoma, aliendelea kusukuma zaidi na zaidi na baada ya dakika chache, mtoto akatoka na nesi kumkata kitovu.

Sarafina akawa hoi, hakuamini kama alijifungua salama, akataka kujua ni mtoto wa jinsia gani alikuwa amejifungua, alikuwa mtoto wa kike, mzuri. Akapewa na kumuweka kifuani mwake kwa ajili ya kuchukua harufu yake.

Uso wake ukawa na tabasamu pana, alipomaliza kumuweka kifuani kwa dakika moja, manesi wakamchukua na kwenda kumuogesha kisha kumletea. Sarafina hakutakiwa kuondoka, walimtaka kubaki hospitalini hapo kwa siku mbili kwani hali yake haikuwa nzuri kama watu wengine walivyokuwa wakijifungua.

Hospitalini hapo, hakuwa na ndugu, hakujua ni kwa namna angeweza kuishi na mtoto wake baada ya kutoka hospitalini hapo. Aliendelea kuwa mahali hapo huku vyakula vya wagonjwa vilivyokuwa vikiandaliwa na uongozi wa hospitali hiyo ndivyo alivyokuwa akila kila siku.

Kichwa kilimuuma, alikuwa na mawazo tele, aliyafikiria maisha yake, yalikuwa ni ya kuumiza sana na hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kuishi kama ilivyokuwa zamani. Alivyokuwa peke yake tu alikuwa na maisha ya tabu, vipi kama angekuwa akiishi na mtoto wake.

Kwenye kufikiria sana, ndipo akakumbuka kwamba zamani alipokuwa akipita katika mitaa ya kitajiri ya Masaki na Mikocheni kulikuwa na nyumba nyingi za matajiri ambazo hazikuwa zimemaliziwa na ndani kulikuwa na familia za mafundi waliokuwa wakiishi.

Hukoo ndipo alipotaka kwenda kuanza maisha mapya, hakujua kama angepokelewa na familia za mafunid hao au la. Siku aliyoruhusiwa, akamchukua mtoto wake aliyempa jina la Malaika na kuanza kwenda naye huko.

Hakuwa na pesa, hakukuwa na kitu chochote zaidi ya mtoto wake tu. Safari ya kwenda Mikocheni ikaanza mara moja. Ilimchosha, ilikuwa ni safari yenye kuchosha lakini alipambana njiani mpaka kufika huko akiwa hoi.

Alisimama mbele ya jumba moja kubwa na la kifahari, halikuwa limemaliziwa, lilizungushiwa ukuta na alipoangalia kwa ndani, aliona kukiwa kumeanikwa nguo na kugundua kwamba humo ndani kulikuwa na moja ya familia za mafundi waliokuwa wakiishi.

Akaingia huku akiwa na mtoto wake, hakuogopa, aliufuata mlango ambao ulizibwa kwa khanga na kuingia ndani. Macho yake yakatua kwa watu watatu, mwanamke mmoja, mwanaume na mtoto wao.

“Hodi!” alipiga hodi huku tayari akiwa ndani ya nyumba ile.

Watu wale wakaamka na kumwangalia Sarafina. Walishtuka! Hawakumfahamu mwanamke huyo na hawakujua alifuata nini. Wakakaa kitako kwa lengo la kumsikiliza shida zake.

Sarafina hakutaka kuwaficha, alikuwa mahali hapo kwa kuwa alihitaji sana msaada hivyo kuwaambia watu hao kwamba alikuwa masikini hivyo alihitaji msaada. Kwa kumwangalia tu ilionyesha dhahiri alikuwa masikini wa kutupwa, alikonda sana, macho yaliingia ndani, maziwa yake yalilala na hata nguo alizokuwa amezivaa zilionyesha ni kwa jinsi gani alikuwa masikini.

“Huyu ni nani?” mwanamke alimuuliza mumewe kwa sauti ya chini, japokuwa Sarafina aliwahadithia historia ya maisha yake lakini bado walitaka kujua zaidi.

“Sijui! Tumsaidie kweli au?” aliuliza mwanaume huyo, walikuwa wakiteta kwa sauti za kunoing’ona.

“Labda! Haina jinsi, ila tumebakiza miezi sita tu ya kuishi hapa, itakuwaje?” aliuliza mke.

“Haina jinsi! Japokuwa sisi ni masikini, haina jinsi, tumsaidie hata masikini mwenzetu,” alinong’ona mwanaume huyo.

Hawakuwa na kitu chochote kile, walikuwa wakiishi ndani ya nyumba hiyo kwa mwaka wa pili. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao, wakati nyumba za matajiri zilivyokuwa zikijengwa, waliomba hifadhi, walikuwa wakipewa, kwa kifupi maisha yao yalikuwa ya kuhamahama.

Wakaishi na Sarafina nyumbani hapo, hakukuwa na maisha mazuri hata kidogo, sakafu ilikuwa ni ya mchanga, madirisha hayakuwekewa nyavu wala kioo, yaliwekewa khanga kwa ajili ya kuzuia wadudu kuingia humo ndani.

Malaika alikuwa msumbufu, mara kwa mara alikuwa mtoto wa kulia, alisumbua sana lakini Sarafina hakuonekana kukasirika hata mara moja. Huyo alikuwa mtoto wake, aliyemzaa yeye mwenyewe, alimpenda zaidi ya kitu chochote kile.

Siku zikaendelea kukatika. Mtu aliyekuwa akitegemewa nyumbani hapo alikuwa mzee Hamidu, mwanaume aliyekuwa akiishi na mkewe. Yeye ndiye aliyekuwa akitafuta pesa ya matumizi kwa kwenda kwenye kazi zake za ujenzi na kufanya mishemishe yake nyingine.

Miezi iliendelea kukatika huku mtoto Malaika akiendelea kukua pamoja na mtoto wa wasamaria wema hao aliyeitwa Saleh aliyekuwa na miaka mitatu. Maisha hayakuwa rahisi hata mara moja, wakati mwingine walilazimika kulala na njaa hasa pale walipokuwa wakikosa chakula.

Baada ya kutimiza miezi mitano tangu aishi mahali hapo Aisha akaanza kujisikia hali ya tofauti mwilini mwake. Uchovu ukamuanza na muda mwingi alikuwa akisikia maumivu katika maziwa yake.

Alijishangaa, hakuwahi kuwa katika hali hiyo hata siku moja, alikuwa na hofu kwamba inawezekana alikuwa na kifua kikuu lakini kitu kilichompa maswali mengi. Hakutaka kubaki kimya, akamshirikisha Aisha ambaye alimwambia kwamba ni lazima waende hospitali kwani inawezekana maziwa yake yalikuwa yakiisha kwa haraka.

“Naogopa!” alisema Sarafina.

“Unaogopa nini?”
“Basi tu kwani hata huku kwapani nimepata uvimbe!” alisema Sarafina.

Hilo lilimuogopesha zaidi Aisha na hivyo kumlazimisha kwenda hospitalini ili kujua ni kitu gani kilisababisha hali hiyo mwilini mwake. Wakaondoka hapo mpaka katika Hospitali ya Mwananyamala ambapo baada ya kuonana na daktari, Sarafina akaambiwa kwamba alikuwa na saratani ya matiti ambayo kwa Kiingereza iliitwa Breast Cancer).

“What?” (nini?)

“You have breast cancer,” (una saratani ya matiti) alijibu daktari.

Sarafina akanyamaza, akakiinamisha kichwa chake chini, machozi yakaanza kumtoka. Moyo wake ulikuwa na maumivu makali, hakuamini kama aliathirika kwa kupata ugonjwa huo.

Aisha akaanza kumbembeleza anyamaze lakini mwanamke huyo hakunyamaza, aliendelea kulia zaidi. Wakapewa dawa na kurudi nyumbani. Mimba aliyopewa na David ikaharibu kila kitu, ikayaharibu maisha yake kwa ujumla na kujikuta akipata matatizo makubwa zaidi.

Alijuta kuwa na mwanaume huyo, alimwamini kwa asilimia mia moja lakini matokeo yake mwanaume huyo akamuumiza, hakumuonea huruma hata kidogo.

Kitendo cha kuumwa ugonjwa huo, tayari aliliona kaburi mbele yake, hakuona kama angeweza kupona kwani aliwafahamu watu wengi waliowahi kuumwa ugonjwa huo, wengi walikufa na yeye mwenyewe kuwazika.

“Ninakufa,” alisema Sarafina huku akiendelea kulia.

“Hutokufa! Kuumwa si kufa!”
“Ila ninaumwa kansa!”
“Hata kama kuumwa si kufa Sarafina!” alisema Aisha.

Matumaini ya kuendelea kuishi yakafutika, aliuona mwisho wake, alichokuwa akikifikiria kilikuwa ni mtoto wake tu. Hakujua kama angekufa mtoto huo angekuwa mgeni wa nani. Kila alipokuwa akimwangalia Malaika, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu mazito.

“Who will love my baby?” (nani atampenda mtoto wangu?) alijiuliza, kila alipomwangalia Malaika, alikosa nguvu kabisa.

Kuanzia siku hiyo maisha yake hayakuwa kama yalivyokuwa kipindi cha nyuma, yakabadilika na mwezi wa sita ulipoingia, mwenye nyumba akafika na kuwaambia kwamba alitaka kuendeleza ujenzi wa nyumba yake na hivyo walitakiwa kuondoka haraka iwezekanavyo.

“Nyie mnakwenda wapi?” aliuliza Sarafina.

“Hatujajua! Ila tutaishi popote pale! Na wewe?” aliuliza Aisha.

“Sijajua! Ila nitakwenda mtaani, nitaishi hivyohivyo na mtoto wangu!” alisema Sarafina.

Hakutaka kubaki mahali hapo, siku hiyohiyo akaondoka kuelekea mitaani. Hakuwa na pa kwenda, kwa Dar es Salaam hakuwa na ndugu yeyote yule, marafiki zake hawakumtaka tena.

Sarafina hakuwa mrembo tena, alisinyaa, mwili ulikwisha na kwa jinsi alivyoonekana alionekana kama bibi aliyekaribia kufa. Maisha ya mitaani yakaanza, akaanza kuombaomba fedha ya chakula. Mtoto wake alimsumbua, ili anyonye, alitakiwa kula chakula cha kutosha.

Alipokuwa akipita mitaani, watu walimuonea huruma, hawakujua historia ya maisha yake, walimsaidia kwa kuwa alionekana kuwa mwanamke aliyehitaji sana msaada.

Hakuwa na pesa za kununua dawa, kansa aliyokuwa nayo ikaendelea kusambaa, ikatoka katika maziwa na kusambaa katika kifua chake. Akaanza kukohoa, mwili ulipata tabu lakini alivumilia.

Hakuacha kumuomba Mungu, alijua kwamba asingepona lakini alimwambia Mungu kwamba amchukue wakati mtoto wake amefikisha hata miaka saba, kipindi ambacho angekuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote kile.

Akayarudia maisha ya kulala vibarazani, usiku aliumwa na mbu, alipigwa na baridi lakini hakuwa na jinsi. Kila alipokuwa akilala, alihakikisha Malaika anamfunika vizuri kabisa. Si kila mtu aliyependa Sarafina alale kibarazani kwake, wakati mwingine alikuwa akifukuzwa kama mbwa, aliondoka na kwenda kulala katika kibaraza cha nyumba nyingine.

“Nyamaza mwanangu! Nyamaza Malaika!” alisema Sarafina huku akimwangalia mtoto wake aliyekuwa akilia.

Usiku wa siku hiyo ulionekana kuwa tofauti! Malaika alikuwa akilia kupita kawaida, alionekana kuwa na tatizo, ilimuogopesha mno Sarafina na kuhisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha ya mtoto wake.

Mwili wake ulichemka mno, aliogopa, alipomwangalia machoni, mboni nyeusi haikuwa ikionekana, alikuwa akitetemeka mno huku aking’atang’ata ulimi wake kwa fisi zake zisizokuwa na meno.

“Mungu wangu! Malaika! Kuna nini mpenzi?” aliuliza Sarafina.

Aliuona mwisho wa mtoto wake, aliona kabisa kwamba alikuwa akienda kufa. Alikuwa tayari kushuhudia kila kitu maishani mwake lakini si kushuhudia mtoto wake akifariki dunia.

Akainuka pale kibarazani alipokuwa, hakutaka kubaki mahali hapo, akambeba na kuanza kuondoka. Alikuwa Magomeni Mapipa, kuelekea katika Hospitali ya Mwananyamala ilikuwa mbali sana lakini hakuwa na jinsi, hakuwa na nauli, ilikuwa ni saa nane usiku, kama hakuwa na nauli, alitakiwa kukimbia kuelekea hospitalini huko.

Hali ya Malaika iliendelea kubadilika, kila alipopiga hatua ndivyo hali yake ilivyozidi kuwa mbaya. Sarafina alilia, kilio chake hakikubadilisha kitu! Malaika aliendelea kuwa vilevile.

“Please my baby! Don’t go! Please don’t leave me,” (tafadhali mtoto wangu! Usiondoke! Usiniache!) alisema Sarafina huku akilia.

Alikuwa akikimbia, alifika Magomeni Morocco huku hali ya mtoto wake ikiwa mbaya kabisa. Aliendelea kugongagonga fizi zake huku akionekana kuwa kwenye hatua za mwisho kabisa za kuishi. Angefanya nini kama mtoto wake, Malaika angekufa? Angelia vipi? Angemlaumu Mungu kiasi gani?

“Mungu! Nina kansa! Najua nitakufa! Ila naomba uniachie mtoto wangu! Mungu! Nisikie kilio changu, naomba uniachie mtoto wangu! Mungu! Niue mimi, nipo tayari kufa hata sasa hivi, niue Mungu, niue Mungu, nipo tayari kufa hata sasa hivi ila naomba uniachie mtoto wangu! Ni mdogo mno, sijajua ataishi vipi baada ya mimi kufa, ila nipo tayari kufa kwa ajili ya mtoto wangu! Niue Mungu hata sasa hivi ila umuache Malaika aishi!” alisema Sarafina huku akilia.

Hakujua kama mwilini mwake alikuwa na nguo ya ndani tu. Khanga aliyokuwa nayo mwilini ilidondoka, hakujua, alikuwa akikimbia. Mwananyamala kulikuwa mbali, hakusimama, hakujua kama alikuwa na nguo ya ndani, kitu alichokuwa akikifikiria ni kumuokoa mtoto wake tu ambaye mwili wake ulipata joto kali mno na kila alipomwangalia, alikuwa na uhakika kwamba usiku huo ndiyo ulikuwa wa mwisho kumuona mtoto wake akiwa hai.

“Niue Mungu!” alisema huku akikimbia kama mtu aliyechanganyikiwa. Kwa jinsi alivyokuwa, kila mtu aliyemuona alifikiri kwamba mwanamke huyo alikuwa chizi, wengi wakaanza kumpiga picha na kuchukua video, yeye hakutaka kujali, alikuwa akikimbia kuelekea katika Hospitali ya Mwananyamala huku tayari ikiwa imefika saa nane kasoro usiku.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho hapahapa.

Toa comment