MREMBO AFA KIFO TATA

INASIKITISHA sana! Mrembo mmoja ‘mtoto wa mjini’ aliyejulikana kwa jina la Rehema Kidae almaarufu Rose, mkazi wa Mwananyamala – Kwa Kopa, jijini Dar amekufa kifo chenye utata mkubwa.

 

Mapema wiki hii, Rose alikutwa amefariki dunia ndani ya chumba alichokuwa akiishi huku akiwa amekaa kwenye kiti na pembeni yake kuna ndoo yenye mabonge ya damu. Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, mwili wa Rose uligundulika baada ya siku mbili hivyo kukutwa ukiwa umeanza kuharibika.

 

Akizungumza na Risasi Jumamosi juu ya mkasa huo, rafiki wa karibu wa Rose alisema alimfahamu Rose miaka kumi iliyopita kwani walikuwa wakiishi sehemu moja na alitoka kwao mkoani Iringa mwaka 2001 kwa ajili ya kufanya kazi za ndani jijini Dar.

 

Alisema tangu kipindi hicho, Rose hakuwahi kurudi tena nyumbani kwao au hata kujua ndugu zake; lakini alikuwa na dada yake wa hiyari aliyekuwa akiishi naye nyumba moja aitwaye Maria. Maria kwa kushirikiana na majirani na marafiki ndiyo waliohusika katika kufanya maziko ya Rose.

“Hatukuwahi kumuona ndugu yake hata mmoja. Tunamfahamu Maria tu ambaye alikuwa mpangaji mwenzake na ndiye alikuwa karibu naye kwa sababu alitoka kwao huko Mufindi muda mrefu.

 

“Inasemekana hata ndugu zake walijua alishakufa, lakini hapa (Dar) alikuwa na mwanaume wake aitwaye Alex.

“Huko nyuma Rose na Alex kila mmoja alikuwa akiishi kivyake, lakini baadaye Rose alipata tatizo la kodi, akahamia kwa Alex,” alisema rafiki huyo wa Rose.

 

Alisema siku ya tukio alipata kuwa rafiki yake huyo amefariki dunia na alikutwa ndani akiwa amekaa zaidi ya siku mbili. “Ilisemekana mpenzi wake huyo alisafiri na kufunga mlango kwa nje bila mtu kujua kama kuna mtu ndani wala mama yake mzazi ambaye pia anaishi hapo.

 

“Unajua Rose alikutwa amekufa ndani, tena akiwa amekaa kwenye kiti, lakini pia pembeni yake kulikuwa na ndoo yenye damu ya mabongemabonge, lakini pia mwili wake ulionekana umekaa zaidi ya siku mbili kwa sababu ulishaanza kutoa harufu. “Cha kwanza kilichofanyika ni kuita Polisi ambao waliuchukua mwili na kuupeleka Hospitali ya Mwananyamala na baadaye Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi na kuuhifadhi mochwari.

“Kingine walichokifanya Polisi ni kumkamata mama wa Alex, lakini baadaye Alex alijitokeza hivyo mama yake akaachiwa na yeye akatiwa mbaroni kwani tukio hilo liligubikwa na utata mzito juu ya kilichomuua Rose na mazingira mwili wake ulivyokutwa,” alisema rafiki huyo.

 

Rafiki huyo aliendelea kusema kuwa mwili wa Rose ulikaa Muhimbili wakati ndugu wakitafutwa hivyo baada ya kuona kimya marafiki na majirani walichukua jukumu la kuubeba msiba huo kwa kuandaa kila kitu.

 

Hata hivyo, alisema siku moja kabla ya mazishi ndipo walipojitokeza ndugu na kuomba majirani na marafiki waendelee na taratibu za mazishi wao watakuja kuona kaburi. “Watu walihangaika sana kutafuta ndugu kila kona, ikabidi tu majirani na marafiki wajitoe kwa hali mali kwa ajili kumsitiri na ndivyo ilivyokuwa,” alisema.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Musa Tahib alithibitisha kupokea taarifa ya kifo hicho na bado uchunguzi unaendelea. Mwili wa Rose aliyekuwa maarufu mitaa ya Mwananyamala ulipumzishwa kwenye Makaburi ya Mwananyamala jijini Dar huku utata ukiendelea kutawala juu ya kifo chake.

STORI: Imelda Mtema,  Risasi Jumamosi


Loading...

Toa comment