The House of Favourite Newspapers

Mrithi Wa Lwandamina Akumbuke Hili

 

Wachezaji wa timu ya Yanga.

WIKI hii wapenzi na mashabiki wa Yanga walipigwa na but­waa baada ya aliyekuwa kocha wa timu yao, Mzambia, George Lwandamina kutimka ndani ya kikosi hicho kipindi ambacho alikuwa anahitajika zaidi kutoka­na na majukumu yaliyopo mbele yao.

 

Ndani ya Yanga, Lwandamina al­ipokea kijiti kutoka kwa Mholanzi, Hans van Der Pluijm ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Singida United kinachoshiriki Ligi Kuu Bara.

 

Kocha huyo msimu uliopita ali­fanikiwa kuipa Yanga ubingwa uki­wa ni msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi hicho, ingawa msimu huu kidogo mpaka ligi ilipofika mambo yameonekana kuyumba ingawa ligi bado haijamalizika.

Lwandamina alipambana na ku­weza kuibeba Yanga tangu alipoan­za kuinoa msimu uliopita ambapo alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na timu yake ikafanikiwa kushiriki michuano ya kimataifa ambayo mpaka sasa inashiriki na Jumatano ijayo timu hiyo itacheza bila yeye dhidi ya Wolaitta Dicha.

 

Katika mchezo wa kwanza hapa nyumbani dhidi ya Wolaitta Dicha ya Ethiopia kwenye Kombe la Shirik­isho Afrika hatua ya mtoano, Lwan­damina alikuwepo kwenye benchi wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Lwandamina aliyeondoka nchini mapema wiki hii, juzi Jumatano wakati Yanga ikitoka sare ya 1-1 na Singida United kwenye mch­ezo wa Ligi Kuu Bara, yeye alikuwa nchini Zambia akikaa jukwaani na kuishuhudia timu yake mpya za Zes­co ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lusaka Dynamos.

 

Pamoja na kuondoka kwake Yanga alikuwa ni moja kati ya makocha am­bao walichangia kukuza vipaji vya wachezaji wengi na kuweza kufika hapo walipo sasa.

Pia ni mmoja kati ya mako­cha wa kigeni ambao wanastahili kupongezwa kutokana na aina ya ufundishaji wake pamoja na falsafa yake ya kuweza kuwaamini vijana.

 

Mzambia huyo alifanikiwa ku­watumia vijana katika kikosi chake ambao awali hawakuwa wakipewa nafasi ndani ya kikosi hicho na wen­gine aliweza kuwasajili baada ya kubaini uwezo wao. Mfano Yohana Nkomola na Ramadhani Kabwili am­bao walitoka Serengeti Boys.

 

Kocha huyo alikuwa akiwapa na­fasi vijana hao pamoja na wengine kikosini hapo na walipambana kweli na hawakuweza kumuangusha.

Kwa msimu huu, vijana wengi nda­ni ya kikosi cha Yanga wamepewa nafasi kubwa baada ya wale wazoe­fu kuwa nje wakiuguza majeraha.

Kwa muda mrefu, imekuwa ngumu sana kwa timu hizi kubwa za Simba na Yanga kuweza kuwaamini vijana na kufikia hatua mpaka wakaweza kutumika katika michuano ya ki­mataifa lakini Mzambia huyo aliweza kufanya hivyo na kufika hapa wali­posasa.

 

Baada ya kocha kuondoka bado Yanga ina kibarua kizito kuhakikisha inajipanga sawa kwa kupata matokeo kwa michezo ambayo iko mbele yao bila hivyo itakuwa ngumu kwao kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara.

 

Licha ya kuondoka kwa kocha huyo ndani ya Yanga, viongozi wa timu hiyo wanapaswa kujipanga na kujijenga kisaikolojia kwa kuhakikisha timu yao inafanya kweli kwenye michuano iliyopo mbele yao hasa upande wa ki­mataifa ambapo katika mchezo wao wa awali walifanya vyema.

 

Tunafahamu Yanga inapitia kipindi kigumu kutokana na kuwa na lundo la majeruhi ambao wapo nje kwa muda mrefu wakijiuguza na kulaz­imika kuwatumia vijana ambao ha­wana uzoefu kwenye michuano ya kimataifa.

Sasa pamoja na hilo inatakiwa ku­jiamini kuwa inaweza kufanya vyema kwa kupitia haohao vijana ili iwe mfano kwa timu zingine kutoogopa kuwatumia.

 

Hivyo kocha ajaye anaweza kuwa na falsafa yake pengine ya kuende­lea kuwatumia au kuwaweka kando ili wajifunze zaidi lakini tumeona umuhimui wao kikosini.

Mwisho nimtakie kila kheri Lwan­damina na mafanikio mema katika majukumu mapya huko aliko, hakika Yanga itamkumbuka mchango wake katika klabu yao.

NA PHILLIP NKINI

Comments are closed.