The House of Favourite Newspapers

Msama Awaonya Vinara Wizi Kazi za Wasanii

0
Msama Promotions
Mkurugenzi wa Msama Promotions, wasimamizi na wasambazaji wa kazi za Muziki wa Injili, Alex Mwita Msama, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

MKURUGENZI wa Msama Promotions, wasimamizi na wasambazaji wa kazi za Muziki wa Injili, Alex Mwita Msama, amewataka wauzaji wa CD feki kuacha mara moja kwani siku zao za kuwakamata zinahesabika.

 

Msama aliwataja baadhi ya vinara anaowajua kuwa ndiyo wamekuwa wakisumbua hasa katika uuzaji na utengenezaji wa CD feki za kazi za wasanii kutoka katika mikoa ya Dar, Morogoro na Mwanza.

 

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Msama alisema kuwa siku na saa ya kuwakamata wezi wa kazi za wasanii haziko mbali kwani tayari wamekwishafahamika sehemu walipo na wanapozalishia CD feki zinafahamika.

 

Alisema serikali inatengeneza mazingira safi na wafanyabiashara waaminifu wanaofuata utaratibu sahihi, ikiwemo ulipaji wa kodi kwa wakati na hivyo kampuni yake itaendelea kuhakikisha kazi za wasanii zinalindwa na kuheshimika.

 

Pia, katika kuonyesha msisitizo, Msama alisema: “Serikali ya awamu ya tano ni serikali ya kazi, hivyo haina chuki na mfanyabiashara yeyote anayefuata utaratibu wa kawaida ikiwemo kulipa kodi na mambo mengine ya kufanana na hayo.

 

Nirudie tena wito wangu kwamba sasa biashara haramu ya kazi za wasanii imetosha, kuna baadhi ya mapapa wa kurudufisha na kuuza CD feki katika mikoa mbalimbali kama ya Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza. Tutahakikisha tunawakamata wote; kuna watu wananitumia meseji na kunitaka nikutane nao sitaki. Ninamshukuru Mkuu wa Polisi nchini, Simon Sirro, kwa kuwa tayari kutoa askari ambao tutashirikiana nao kuwakamata maharamia wa kazi za wasanii.

 

Tukiwaondoa wezi wa kazi za wasanii serikali itakusanya kodi halali. Kila mmoja awapige vita wachuuzi, wezi na maharamia wanaoiba kazi za sanaa kwa kuchoma CD feki, kwani kwa kufanya hivyo wananyonya jasho la wasanii na kuiingizia hasara serikali kwa kutolipa kodi halali. Sisi kama wasimamizi na wasambazaji wa kazi za sanaa tumeazimia kufanya ufuatiliaji kwa oparesheni maalum ambayo haina siku wala saa.”

 

NA DENIS MTIMA/GPL

Leave A Reply